2841; Uchawi na ushirikina.

Hadithi tulizokuwa tunajifunza utotoni zilikuwa na maana kubwa ambayo haikuwa rahisi kwa akili zetu za utoto kung’amua.

Moja ya hadithi hizo ni SIZITAKI MBICHI HIZI. Kama unakumbuka, sungura aliona ndizi na kuzipenda. Akaanza kuzirukia, lakini hakuzifikia.
Akaruka na kuruka tena, lakini wapi.
Baada ya kuhangaika sana bila mafanikio, akajiambia hata hivyo ndizi zenyewe ni mbichi na hivyo hazitaki.

Huo ndiyo uhalisia kwenye maisha yetu ya kila siku.
Watu wanapenda kupata vitu fulani.
Wanapambana sana kuvipata, lakini kwa sababu ya ugumu wa kupatikana kwa vitu hivyo, wanaishia kuvikosa.
Mwisho wanaamua kuvibeza vitu hivyo.

Huhitaji kwenda mbali kuelewa hilo, wewe anza tu na mfano wa fedha.
Kila mtu anapenda fedha na ana mahitaji na fedha.
Lakini watu wanapohangaika na fedha na wasizipate, wanaamua kuzibeza na kuwachukia wale walionazo.

Hapo ndipo utawasikia wakisema pesa siyo kila kitu, pesa hainunui furaha au matajiri ni watu wenye roho mbaya.
Hizo zote ni kauli ambazo hazina maana yoyote zaidi tu ya kujifariji kama sungura aliyekosa.

Ukisema pesa hainunui furaha, kwani umasikini unanunua furaha? Au ni wapi uliambiwa pesa inanunua furaha? Hilo swala la pesa na furaha vimetokana wapi pamoja? Ukiwa na njaa na unataka kula, hutatumia furaha kununua chakula, bali utatumia fedha. Kuweka pamoja fedha na furaha ni njia ya wazembe kujifariji.

Kadhalika kauli kwamba matajiri wana roho mbaya. Hivi kuna watu wenye roho mbaya kama masikini?
Hivi hujawahi kujiuliza kwa nini visa vya ushirikina na kulogana vipo zaidi kwa masikini kuliko matajiri?
Kile kinaitwa uchawi na ushirikina ni hali ya roho mbaya tu baina ya watu. Hakuna nguvu yoyote ya ziada kwenye hayo zaidi ya roho mbaya.
Kwa mfano kwenye ajira, pale mtu mmoja anapofanya hujuma mwenzake asipande cheo, huo ndiyo uchawi. Na akili za kimasikini zinachochea zaidi hilo kuliko mengine.

Kuchukia utajiri kwa sababu umeukosa haifanyi utajiri kuwa kitu kibaya, bali kunakufanya uwe mchawi na mshirikina.
Kama unafurahia pale matajiri au waliokuzidi wanapata matatizo, huo ndiyo uchawi na ushirikina wenyewe.

Hatua ya kuchukua;
Pitia mambo yote ambayo unayachukia au kujifariji siyo kila kitu. Kisha ona ni kwa namna gani uliyataka ila ukayakosa. Sasa acha kujifariji, badala yake jifunze kwa wale ambao wameshayapata ili na wewe uweze kuyapata pia.

Tafakari;
Kuchukia kitu ambacho hujakipata hakukufanyi wewe kuwa mtakatifu sana. Badala yake kunakugeuza kuwa mchawi na mshirikina.
Kama kuna kitu umekitaka sana ila unakikosa, endelea kukipambania, vitu vizuri siyo rahisi.
Na kuvichukia ulivyovikosa haikusaidii kwenye kuvipata.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji