2848; Lengo, Sifa, Maboresho.
Hivyo ni vitu vitatu vinavyoweza kukufanya kuwa kiongozi bora kabisa kutokea.
Ni vitu unavyopaswa kuvifanya kwako na kwa wote unaowaongoza.
Kwanza unaanza na lengo, nini hasa unachotaka kupata? Au matokeo gani yanapaswa kupatikana?
Lengo lazima liwe wazi na kueleweka na wote wanaohusika.
Na liweze kuelezewa kwa sentensi moja.
Kuwa na lengo ni hatua moja, kulifanyia kazi lengo ni hatua nyingine muhimu.
Hivyo kuweza kuliandika lengo kwa sentensi moja ni ili uweze kujikumbusha kila mara.
Kila baada ya saa moja, chukua dakika moja kujikumbusha lengo lako kuu.
Kisha angalia kime unachofanya kwa muda huo kama kinachangia kulifikia lengo.
Kama kinachangia unaendelea kufanya, kama hakina mchango unaacha kufanya.
Katika kufanyia kazi lengo, kuna matokeo ya aina mbili.
Moja ni ushindi, kukamilisha lengo kama ulivyoweka. Hapo unahitaji sifa kwa kuweza kufikia lengo na kisha kujisukuma kwa kuweka lengo jingine na kulifanyia kazi.
Sifa ni muhimu ili upate msukumo wa kuendelea kufanya.
Matokeo mengine ni kushindwa, kupata matokeo ambayo ni tofauti na matarajio.
Hapa unapaswa kufanya maboresho ili kuchukua hatua sahihi kuliendea lengo.
Wengi katika hali kama hii hukata tamaa na kuachana na lengo. Lakini wewe usiwe hivyo, badala yake jitathmini, wapi umekosea, kisha fanya maboresho na ulifanyie kazi lengo kwa uhakika zaidi.
Kwa kufanya haya matatu mara zote, lazima utapata mafanikio makubwa unayotaka. Maana kufanikisha lengo hakukufanyi uzembee na kushindwa lengo hakukufanyi ukate tamaa.
Haya matatu unayofanya kwako ndiyo pia unapaswa kuyafanya kwa wale unaowaongoza.
Kwanza unawasaidia kuweka lengo katika yale wanayofanyia kazi. Usiwawekee lengo, bali wasaidie waweke lengo, muhimu ni wazalishe matokeo yanayohitajika.
Pili wasifie pale wanapofanya vizuri kwenye malengo waliyojiwekea. Unapowasifia wanajisikia vizuri na kuendelea kufanya kwa ubora.
Tatu wasaidie kuboresha pale wanapofanya vibaya. Usiwakatishe tamaa na kuwaonyesha hawawezi, bali wafanye waone ni njia gani bora kwao kufanya ili wapate matokeo wanayoyataka.
Hatua za kuchukua;
Weka lengo na tumia sifa pale mambo yanapokwenda vizuri na maboresho pale mambo yanapokwenda vibaya. Kila wakati kuwa kwenye mchakato huo, kwako mwenyewe na kwa wote unaowaongoza.
Tafakari;
Sababu za watu kushindwa ni kwanza kutokujua nini hasa wanachotaka (kukosa lengo), kutokupata sifa pale wanapofanya vizuri (kwa kutokujua) na kukata tamaa pale wanapofanya vibaya (kwa kutokujua maboresho ya kufanya).
Wewe umeshajua umuhimu wa hayo matatu, yazingatie.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed
asante sana,,,,ukurasa muhimu huu kwa wanaotaka kuondoka kisima cha maarifa kwa kua wanaona ugumu wa malengo kufikiwa.
kila mtu asome hili muhimu sana.
LikeLike