2902; Mipango kabla na baada ya fedha.
Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye unakuwa na mipango mizuri kabla hujawa na fedha, ila ukishakuwa nazo mipango hiyo inayeyuka.
Watu wamekuwa wanasema wazi kwamba wakiwa hawana fedha wanakuwa na mipango mizuri. Ila wakishazipata fedha wanasahau mipango hiyo mizuri.
Wanazitumia mpaka zinaisha ndiyo wanakuja kuikumbuka mipango yao.
Iko hivi rafiki, ukiwa huna fedha akili yako inakuwa na utulivu mkubwa kwenye mambo yanayohusu fedha.
Unapangilia mambo yako vizuri kabisa na kwa mantiki.
Unapopata fedha, unapoteza mantiki na kuanza kutawaliwa na hisia. Yanakuja mawazo mengine mapya kabisa, ambayo yanaweza kuonekana ni sahihi kuliko yale uliyokuwa nayo awali.
Kwa kuwa mantiki imewekwa pembeni na hisia ndiyo zinatawala, mawazo mazuri uliyokuwa nayo awali yanasahaulika na unaendeshwa kwa mihemko unayokuwa nayo wakati una fedha.
Kuondokana na changamoto hii, unapaswa kuwa na msimamo mkali sana.
Mawazo yote mazuri unayokuwa nayo kabla hujawa na fedha, ndiyo hayo hayo unapaswa kuyatekeleza pale unapopata fedha.
Usibadili mawazo yako baada ya kuwa na fedha, hata ushawishike mawazo mapya ni mazuri kiasi gani.
Wewe endelea kusimamia mawazo uliyokuwa nayo awali, yanakuwa ni mazuri kuliko yanayokujia ukishakuwa na fedha.
Ukiwa huna fedha, hakuna watu watakaokushauri juu ya fedha, hivyo unafikiri kwa akili yako mwenyewe.
Ukiwa na fedha kila mtu anajifanya ni mshauri mzuri kwako juu ya fedha, ushauri wao mwingi unakuwa siyo sahihi kwako.
Hivyo epuka kuchukua ushauri unaoupata wakati una fedha, badala yake tekeleza mawazo uliyokuwa nayo kabla hata hujawa na fedha.
Ni zoezi gumu, lakini ambalo linawezekana kabisa.
Kuwa na msimamo mzuri kwenye hilo na utaweza kufanya makubwa.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe