2921; Mimi na wewe.

Rafiki yangu mpendwa,
Ninapokuita rafiki, simaanishi kuwa na wajibu wa kukufanya ujisikie vizuri.
Bali namaanisha upendo mkubwa nilionao kwako wenye nia ya kuhakikisha unapata kile hasa unachotaka.

Na hilo halitakuwa rahisi, ndiyo maana upo hapa.
Lengo la ujumbe huu wa leo ni kufafanua mahusiano yangu mimi na wewe.

Mahusiano makuu ya mimi na wewe ni mimi ni kocha wako wewe.
Ukocha ni neno moja, lakini linabeba maana kubwa ndani yake.

Mimi kama kocha wako, wajibu wangu wa kwanza ni wewe.
Napaswa kujua kile unachotaka na kisha kukusimamia kwa karibu kuhakikisha unakipata kweli.

Katika kuhakikisha kweli unapata kile unachotaka, nawajibika kukamilisha yafuatayo;

  1. Kukuwezesha kuiona picha kubwa badala ya kusongwa na yale yaliyo mbele yako.
    Ni rahisi sana kutekwa na mambo madogo madogo yanayokuzunguka na kulisahau lengo lako kubwa. Kila wakati napaswa kukukumbusha lengo lako kuu.

  2. Nakusaidia kuweka umakini wako kwenye kile unachofanya.
    Tunaishi kwenye zama zenye kila aina ya usumbufu. Ni rahisi kutekwa umakini wako na kuhangaika na yasiyo na tija wako. Nawajibika kuhakikisha unaweka umakini wako wote kwenye mipango sahihi ya kukufikisha kwenye lengo lako kuu.

  3. Nakusukuma uende hatua ya ziada, ufanye zaidi ya ulivyozoea.
    Binadamu huwa tunapenda mazoea na hayo ndiyo kikwazo cha mafanikio makubwa. Ni wajibu wangu kukusukuma utoke kwenye mazoea yoyote uliyonayo ili ufanye mambo mapya na tofauti yanayokufikisha kwenye malengo yako makubwa.

  4. Nakueleza ukweli kama ulivyo bila ya kukuficha au kukuonea aibu.
    Watu wengi wanaokuzunguka wanajua ukweli mwingi kuhusu wewe lakini hawakuambii, kwa sababu ukweli unauma na hawataki kukuumiza. Nawajibika kukuambia ukweli kama ulivyo, hata kama unauma, maana ndiyo dawa ya kufika unakotaka kufika.

  5. Nakusaidia kuona mambo madogo madogo unayoweza kuyapuuza.
    Katika kuyapambania malengo yako makubwa, kuna mambo madogo madogo unayoweza kuyapuuza halafu baadaye yakaja kuwa kikwazo kwako. Sitaruhusu hilo litokee kwako, utayazingatia yote mugimu.

  6. Nakusikiliza.
    Wakati mwingine unachohitaji siyo ushauri wala kuambiwa chochote, bali mtu tu wa kukusikiliza. Kuyaeleza matatizo na changamoto zako kwa mtu ambaye hatakuhukumu hata kama umekosea vipi, ni nusu ya kuyatatua. Nawajibika kukusikiliza bila ya kukuhukumu kwa namna yoyote ile.

  7. Ni meneja wako wa masoko, mauzo na mafunzo kwenye biashara yako.
    Kama umewahi kufanya kazi ya kuajiriwa popote pale, ulikuwa unasimamiwa utekeleze majukumu fulani. Na ulikuwa unayatekeleza kweli kwa sababu ya usimamizi uliokuwepo. Lakini kwenye biashara yako wewe ndiye bosi, huna wa kukusimamia, hivyo hata usipofanya majukumu fulani, hakuna wa kukuwajibisha. Hilo linakaribisha uzembe na kupelekea kushindwa. Mimi ni meneja wako, ambaye nakusimamia kwa karibu kuhakikisha unatekeleza kweli yale unayopaswa kutekeleza ili biashara yako ikue. Na maeneo makubwa muhimu ninayokusimamia kwa karibu ni masoko, MAUZO, mafunzo na kujenga timu. Hayo lazima ufanye hasa.

  8. Ni menta wako, mshirika wako na rafiki yako wa karibu.
    Nawajibika kukuonyesha njia sahihi na kuwa shabiki wako namba moja kwenye kile unachopambania. Sikufanyi ujisikie vizuri kwa kukudanganya, bali nakufanya uuone ukweli ulivyo na uweze kuukabili ili kupata ushindi mkubwa.

  9. Nahakikisha ndoto ulizonazo zinakuwa uhalisia.
    Haijalishi una ndoto kubwa kiasi gani, ni wajibu wangu kuhakikisha zinatimia. Kitendo cha kuwa na ndoto fulani ni kwa sababu zinawezekana kwako. Mimi nipo kuhakikisha huziki ndoto zako, bali unazipambania usiku na mchana, kwenye jua na mvua na kwa machozi, jasho na damu mpaka kweli uzifikie ndoto zako kubwa.

  10. Nafurahia na wewe pale unapofikia ndoto zako.
    Kuna watu wachache mno kwenye maisha yako watakaofurahi pale unapofanikiwa. Kwa nje wanaweza kuonekana kufurahi, lakini kwa ndani wanakuwa na wivu na wanakuombea sana ushindwe. Mafanikio yako ni maumivu kwa wale wanaokuzunguka, maana unafanya waonekane ni wazembe. Hivyo kadiri unavyofanikiwa, ndivyo unavyowapoteza watu wako wa karibu. Mimi nipo na wewe kwa kila mafanikio unayoyapata, nikifurahia na kutaka ufanikiwe zaidi. Hata kama mafanikio yako ni makubwa kuliko yangu, sitakuwa na wivu nayo, badala yake nitayafurahia zaidi na kutaka uendelee kufanikiwa zaidi. Kwa kuwa wajibu wangu wa kwanza ni wewe, mafanikio yako ni yangu na hivyo nitayafurahia kweli kutoka ndani yangu.

Huu ni mkataba wangu mimi na wewe, ndivyo tutakavyokwenda pamoja.
Tutazingatia vipengele hivi kumi kama vilivyo na bila ya kuvunja chochote.
Viandike vipengele hivi kwa kauli timilifu kwako kwa namna ninavyowajibika kwako.
Kisha twende tukae kwenye mchakato kamili bila kuyumba.
Tunachohitaji nu kufanya tu kilicho sahihi kwa msimamo.
Matokeo makubwa na mazuri yatakuja kwa wakati wake.

Nipo hapa, kwa ajili yako, hakuna mahali naenda.
Tuzingatie vipengele hivi, tutafika mbali.
Rejea vipengele hivi kumi kila siku ili usipoteze dira.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe