2924; Kata Tamaa.
Rafiki yangu mpendwa,
Leo nakupa ruhusa ambayo umekuwa unajinyima kwa muda mrefu.
Ruhusa ya kukata tamaa na kuachana na baadhi ya vitu, hata kama unavitaka sana.
Umezoea kupata mafunzo yanayokuhamasisha usikate tamaa, upambane mpaka tone la mwisho ili kupata ushindi.
Umekuwa unapewa mifano ya watu ambao hawakukata tamaa licha ya kukutana na magumu na hata kushindwa.
Pamoja na kupata maarifa na hamasa hizo, bado kwa upande wako umekuwa huna msukumo mkubwa wa ndani juu ya baadhi ya vitu.
Unaweza kuwa unavitaka sana hivyo vitu, lakini huwezi kujisukuma mwenyewe kuvifikia.
Ni mpaka upate hamasa na msukumo wa nje.
Sasa hivyo ni vitu ambavyo huwa havidumu kwa muda mrefu.
Na hapo ndipo ninapokutaka ukate tamaa na kuachana na vitu hivyo.
Kama kuna kitu unataka na unafanya, ila hauna msukumo mkubwa sana ndani yako wa kukifanya licha ya kukutana na magumu au changamoto, basi achana nacho, kata tamaa.
Kama ukihamasishwa au kusukumwa na wengine unafanya, ila hamasa au msukumo huo ukiisha unarudi kwenye kutokufanya, usijisumbue na kitu hicho, hutatoboa nacho.
Kama unafanya kitu kwa mategemeo ya kupata furaha baada ya kukikamilisha au kupata matokeo pia unajidanganya. Unaweza kukamilisha kweli au kupata matokeo, lakini furaha utakayokuwa umeipata haitadumu kwa muda mrefu. Kitu ambacho kitakukatisha tamaa sana na kuona umeyapoteza maisha yako.
Sasa ni bora ukate tamaa mapema kabla hujaja kupata maumivu makuu.
Rafiki,
Nyuki hawasubiri kuhamasishwa ndiyo watengeneze asali.
Ng’ombe hawasubiri kuhamasishwa ndiyo watoe maziwa.
Kuku hawasubiri kuhamasishwa ndiyo watage mayai.
Viumbe wote hao na wengine wengi, wanazalisha wanayozalisha kwa sababu ndiyo asili kwao na siyo kwa kusubiri hamasa au msukumo wa nje.
Je kwako wewe ni kitu gani una hamasa na msukumo wa ndani kufanya?
Kitu gani ambacho husubiri usukumwe au kuhamasishwa ndiyo ufanye?
Hapo ndipo penye mafanikio yako makubwa.
Kwingine tofauti na hapo unapoteza tu muda, ni bora ukate tamaa mapema ili uachane na yasiyo sahihi kwako na kwenda kwenye yaliyo sahihi.
Umekuwa unasikia hadithi kwamba Thomas Edison alishindwa zaidi ya mara elfu 10 kabla ya kufanikiwa kugundua taa ya umeme.
Unadhani angekuwa anasubiri hamasa na msukumo wa nje angetoboa?
Yaelewe kwa undani haya mambo unayojifunza ili usijidanganye na kujipoteza.
Mahali pengine tunaambiwa maabara ya Thomas Edison iliwaka moto. Hiyo ilikuwa maabara yenye ugunduzi wake mwingi, hivyo alikuwa anapoteza kila kitu.
Unajua alichukuliaje kuungua kwa maabara yake?
Alimwambia kijana wake; “Nenda kamwite mama yako, hatakuja kuona moto mkubwa kama huu kwenye maisha yake.”
Dah!
Je wewe una mtazamo, hamasa na msukumo wa ndani kama huo?
Kama jibu ni hapana, kata tamaa, achana na kitu hicho.
Hakuna ubaya wala dhambi yoyote kuachana na kitu ambacho huna msukumo mkubwa ndani yako wa kukifanya.
Ukishaona huwezi kufanya kitu mpaka uhamasishwe, kusukumwa na kutishiwa.
Ukishaona unafanya kitu ukitegemea furaha baada ya kukimamilisha.
Kata tamaa, achana na kitu hicho.
Hakitaweza kukupa mafanikio unayoyataka.
Nyuki hapotezi muda kumshawishi nzi kwamba asali ni bora kuliko kinyesi.
Na wala nzi hamwonei wivu nyuki kwa sababu anahangaika na asali wakati yeye anahangaika na kinyesi.
Kila mmoja anafanya kile chenye msukumo mkubwa ndani yake.
Hicho pia ndiyo unapaswa kufanya na maisha yako.
Tofauti na hapo, kata tamaa, acha.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Nimependa sana nilipokuwa nasoma makala hii kwakweli Kila mmoja anafanya kile chenye msukumo mkubwa ndani yake.
Hicho pia ndiyo unapaswa kufanya na maisha yako.
Tofauti na hapo, kata tamaa, acha.
LikeLike
Kabisa, haina haja ya kujitesa.
LikeLike