2926; Nipe masaa yangu 16.

Rafiki yangu mpendwa,
Utakumbuka kwenye ukurasa wa 2926 nilikueleza kwa kina uhusiano wangu mimi na wewe na namna tunavyokwenda.
Kwenye vipengele 10 nilivyoeleza, kipengele namba 7 kilieleza kwamba mimi ni meneja wako.
Meneja wako kwenye masomo, mauzo na mafunzo.

Wajibu wa meneja ni kuhakikisha mambo yanafanyika, licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali.
Mameneja wamekuwa wanahitajika kwa sababu watu kwa utashi wao wenyewe siyo rahisi kufanya yale wanayopaswa kufanya, ambayo yana manufaa kwao.
Kwa asili watu ni wavivu na wazembe na watafanya kila kitu kukwepa kufanya majukumu muhimu ambayo pia huwa ni magumu.

Majukumu ya masoko, mauzo na mafunzo ni makubwa na magumu.
Hivyo wengi wamekuwa wanayakwepa na kukimbilia kufanya majukumu mengine rahisi, ambayo hayana tija yoyote.

Wajibu wangu ni kuhakikisha wewe huyakimbii majukumu hayo muhimu na kuhangaika na yasiyo na tija.

Sababu kubwa ambayo watu wamekuwa wanatumia kushindwa kufanya yaliyo muhimu ni muda.
Wengi wamekuwa wanasema hawana muda.

Lakini mimi binafsi, ninaamini bila ya shaka yoyote kwamba kila mtu ana muda wa kutosha kufanya majukumu muhimu.
Kama mtu anasema hana muda, maana yake anatumia muda wake vibaya kwa mambo yasiyokuwa muhimu.

Sasa ili kuhakikisha wewe hujidanganyi kwa sababu hiyo ya muda, nataka unipe masaa yangu 16 ya siku.
Nataka ratiba yako ya saa kwa saa kwa masaa 16 ya siku ambayo ndiyo ya kufanya kazi kwako.

Masaa hayo yanaanza saa 10 alfajiri na kimalizika saa mbili usiku.
Hivyo ninachotaka ni uniandikie kila saa unafanya nini.
Yaani saa 10 mpaka 11 alfajiri unafanya nini. 11 mpaka 12 asubuhi, na kwenda hivyo mpaka saa moja kwenda saa mbili usiku.

Utaandika orodha yote ya masaa hayo 16 na kile unachofanya kwenye kila saa.

Sasa kabla hujakimbilia kujaza majukumu kwenye hayo masaa yako, ujikumbushe kwenye ukurasa wa 2925 thamani ya muda wako. Na kwa KISIMA CHA MAARIFA, kiwango cha chini cha thamani ya muda wako ni Tsh laki 1.

Hivyo unapoandika kitu unafanya kwenye hiyo orodha yako ya masaa, hakikisha kweli kina thamani sahihi ya muda wako.

Hebu fanya hivyo rafiki yangu na utaona jinsi ambavyo tatizo la muda kwako litajipatia ufumbuzi wa haraka.

Na uelewe vizuri, hutaandika hayo kujifurahisha, kwamba useme utafanya kitu fulani halafu ufanye kingine tofauti.
Kwani kuna wakati nitakupigia simu kwenye muda wowote na unipe ushahidi wa kile unafanya wakati huo, ukilinganisha na ratiba uliyoandika.

Lakini pia tathmini unayotoa mwisho wa siku inapaswa kuakisi ratiba uliyoshirikisha ya siku nzima.

Mchanganuo wa matumizi ya masaa yako 16 utaushirikisha kwenye kundi la Bilionea Mafunzoni kila siku.
Tuanzie hapo na kukaa kwenye hilo kwa uhakika na changamoto ya muda itakwisha yenyewe.

Na kama unaona nitakuwa nakubana sana na kumiliki muda wako wote, kumbuka una masaa 8, kati ya saa 2 usiku na saa 10 alfajiri. Hayo yatumie vile utakavyo mwenyewe, sitayaingilia.
Ila masaa 16, hayo nataka niyaone moja kwa moja unayatumiaje.

Ukianza kuuthamini muda wako kwa namna inavyostahili na kuweka vyema vipaumbele vyako, utaweza kufanya yote yaliyo muhimu kwako.
Nisichotaka ni wewe kuendelea kujifanganya na kauli maarufu kama huna muda.
Muda unao ni namna umekuwa unautumia ndiyo imekuwa changamoto kwako.

Kwa kuupa muda wako thamani sahihi na kuupangilia saa kwa saa, utaweza kufanya makubwa sana.

Kama utakuwa makini, utagundua hiki nakueleza hapa siyo kitu kipya.
Kwenye moja ya semina zetu za mwaka, miaka 3 au 4 iliyopita nilishirikisha mpaka mwongozo wa masaa 168 kwa wiki. Nilikupa karatasi yenye masaa hayo yote ya wiki na wewe ulichopaswa kufanya ni kujaza jukumu husika kwenye muda husika.
Rejea kwenye masomo yako ya semina na upate ule mpango uuboreshe na kuufanyia kazi.

Anza leo kunipa mpangilio kamili wa masaa yako 16 ya kazi na fuata mpangilio huo bila kuyumba.
Moja ya kanuni muhimu za mafanikio ni kuweka mipango na kisha kufanyia kazi mipango hiyo.
Hivyo hapa pangilia masaa yako 16 ya siku na fuata mpango huo kwa nidhamu kubwa bila ya kuuvunja.

Kumbuka tumeshakubaliana biashara yako ndiyi kupaumbele cha kwanza kwako.
Sasa nipe mpangilio wa masaa yako 16 ya kazi na tutajionea wazi vipaumbele vyako ni vipi.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe