2934; Akili za mkulima.

Rafiki yangu mpendwa,
Wengi wetu tumepitia familia ambazo zilikuwa zinajihusisha na kilimo.
Hivyo tuna uelewa fulani juu ya kilimo.

Tunajua kabisa kwamba mkulima hapaswi kula mbegu.
Hata njaa ikimkamata kiasi gani, mkulima makini anajua mbegu hailiwi, maana ndiyo kitu cha kumvusha kipindi kijacho.

Lakini pia mkulima anajua hata mavuno yawe makubwa kiasi gani, msimu unapoanza lazima arudi kulima.
Hata kama alivuna mpaka akakosa pa kuweka mazao, hajiambii hatalima tena kwenye msimu unaofuata. Analima kama kawaida.

Halafu kuna subira ya kupanda, kupalilia na kuvuna. Mkulima mwenye akili anajua kabisa hupandi leo ukavuna kesho. Kila kitu kina muda wake na hata ufanye nini, ni lazima usubiri muda husika.

Hapa kuna mafunzo mengi sana ya kibiashara tunayojifunza kwenye ukulima.
Naweza kusema, matatizo mengi ambayo watu wanayapata kwenye biashara yanaanzia kwenye kukiuka kanuni na ukulima.

Pale mfanyabiashara anapokula mtaji, hapo ni sawa na mkulima kula mbegu. Biashara nyingi zimekufa kwa wafanyabiashara kula mtaji kwa kujua au kutokujua.

Pale mfanyabiashara anapoanzisha mkakati fulani, ila anaukatisha haraka kwa sababu haoni matokeo. Labda ni mkakati wa masoko au mauzo. Anauanza kwa nguvu, ila anaishia njiani kwa sababu matokeo hayaji. Hapo anakuwa amekosa subira ya mkulima kwenye kupanda na kuvuna.

Halafu kuna hali ya wafanyabiashara kuridhika haraka. Anapoanza anakazana kutafuta wateja na kuwapa huduma nzuri. Akishakuwa na wateja wengi anaacha kutafuta wapya na waliopo anawapa huduma mbovu. Kinachotokea ni biashara kupoteza wateja na kufa.

Hii ni mifano michache sana ya jinsi misingi ya kilimo inavyoweza kutumika kwenye biashara. Na jinsi ambavyo kukiuka misingi hiyo kuna madhara makubwa.

Kwa changamoto yoyote unayoipitia kibiashara, jiulize mkulima angefanyaje katika hali hiyo. Pia jiulize ni msingi upi wa ukulima umeuvunja mpaka ukaingia kwenye changamoto hiyo?

Rudi kwenye misingi ya kilimo na utaweza kujenga biashara yenye mafanikio makubwa.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe