2937; Kinachohesabika kama kazi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye kurasa za nyuma tumeshirikishana dhana ya thamani ya muda wako na mpangilio wa masaa 16 ya kazi kwenye siku.

Pamoja na watu kufanyia kazi hayo, bado kuna wengi ambao wanachanganya inapokuja kwenye swala la kazi.
Wengi hudhani chochote wanachofanya kwenye muda wao ni kazi.

Masaa 16 unayoyaripotia kama muda wa kazi kwenye siku yako, unapaswa kuyagawa kwenye makundi mawili.
Kundi la kwanza ni masaa 10 ya uzalishaji. Huo ni muda ambao unafanya yale yenye tija kwenye malengo na mipango yako.
Kundi la pili ni masaa 6 ya majukumu ya kawaida. Haya ni yale ambayo hayana mchango wa moja kwa moja kwenye malengo na mipango yako, lakini yanapaswa kufanywa.

Sasa basi, kwenye siku yetu na muda hasa wa kazi, kinachohesabika kama kazi ni kile kinachochangia kufikia malengo na mipango.
Mengine yote, haijalishi umeyafanya kwa nguvu na muda gani, hayahesabiki kama kazi.

Pangilia vizuri muda wako wa kazi, hasa ule ambao ni wa uzalishaji.
Na katika muda huo, fanya majukumu sahihi tu.
Fanya yale yanayokusogeza karibu zaidi na malengo na mipango uliyonayo.
Ni kwa njia hiyo ndiyo utaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Muda wako unawindwa sana,
Ni rahisi kujishawishi kwamba umefanya kazi kwa sababu tu umekuwa ‘bize’ siku nzima.
Unaweza kuwa bize utakavyo, lakini kama unayofanya hayana mchango kwenye malengo na mipango uliyonayo, uliyofanya hayatahesabika kama kazi.

Linda sana muda wako,
Kuwa bahili wa muda wako,
Upeleke muda huo kwenye majukumu yanayokupeleka kwenye malengo na mipango.
Mengine nje ya hayo hayapaswi kufanyika ndani ya muda wako wa uzalishaji.

Inapokuja kwenye kutumia muda wako vizuri, neno HAPANA lina nguvu kubwa sana.
Sema hapana kwa mengi mazuri yanayoonekana unaweza kutafanya, ili ubaki na machache yaliyo bora sana yanayokupeleka kwenye malengo na mipango uliyonayo.

Usichanganye tena kuwa ‘bize’ na kufanya kazi.
Kazi ni kile kinachochangia kwenye malengo na mipango yako.
Yape hayo kipaumbele cha kwanza.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe