2942; Naendelea vizuri.

Rafiki yangu mpendwa,
Kupata utulivu wa maisha na kupunguza kushauriwa na kila mtu ambaye hujamwomba ushauri, mambo yako mengi binafsi usiyaeleze kwa kila mtu.

Kwa hakika kabisa, maeneo haya matatu usiyaweke wazi kwa kila mtu; afya, fedha na mahusiano.
Haya ni maeneo nyeti sana kwako na ambayo unapaswa kuwa na tahadhari kubwa watu gani unaowaruhusu wajue kinachoendelea kwenye maeneo hayo.

Chagua kwa umakini sana ni watu gani utakaokuwa unawaeleza kuhusu maeneo hayo na wengine wote wanapokuuliza kuhusu maeneo hayo unawajibu; “Naendelea vizuri”, halafu usiongeze neno hata moja.

Watu wengi wanaokuwa wanataka kujua kuhusu maendeleo yako kwenye maeneo hayo, hakuna msaada wowote wa maana wanaoweza kukupa kwenye hayo maeneo. Zaidi tu wanaweza kufurahi ndani yao pale unapokuwa na matatizo kwenye hayo maeneo.
Na hata wasiofurahi, hujitahidi kuona wanakua na msaada, hata kama wanachotaka kufanya hakiwezi kuwa na msaada.
Watakupa ushauri ambao hujawaomba na watasisitiza ufanye vitu ambavyo havina tija yoyote.

Tuchukue mfano kwenye eneo la afya. Kama una ugonjwa wowote sugu, kadiri watu wengi watakavyojua kuhusu hilo ndivyo utakavyokosa utulivu wa kukabiliana na changamoto hiyo. Kwani kila mmoja atakuwa na ushauri wake wa nini ufanye juu ya hilo, wakati hawana utaalamu wowote.
Mashauri utakayoyapata kutoka kwa wengi yatakuwa yanakinzana na yatakuchanganya, hutajua hata nini ufanye.

Kwa kuchagua kuwajibu wengi kwamba unaendelea vizuri, unapunguza hayo mashauri ya kukuchanganya.
Hili halimaanishi kwamba unaficha maradhi, badala yake unachagua kueleza kwa wachache ambao wanaweza kukushauri vyema na siyo kila mtu.

Una changamoto zozote za kiafya, usimweleze kila mtu, badala yake chagua wachache ambao wana uelewa na wanaweza kukushauri vyema. Wengine waeleze unaendelea vizuri, itakupunguzia mengi yasiyo na tija.

Mahusiano yako yanapitia changamoto mbalimbali, siyo kila mtu anapaswa kujua. Wajulishe wachache ambao wanaweza kukusaidia kuvuka changamoto hizo. Wengine waambie unaendelea vizuri.

Na kwenye fedha, kuanzia kipato chako, mipango yako na changamoto zako za kifedha, usimweleze kila mtu. Bali chagua watu unaowaamini na wanaokuelewa na kuweza kukusaidia upige hatua kwenye eneo hilo ndiyo uwaeleze. Wengine wote wajibu unaendelea vizuri.

Sehemu kubwa ya watu wanaotaka kujua maendeleo yako kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yako hawana uwezo wa kukusaidia kwenye mambo hayo. Hivyo wanaweza kuishia kukushauri isivyo vyema, kitu ambacho kinaweza kuwa hatari, hasa pale wanaofanya hivyo wanapokuwa watu wa karibu.
Na pia kuna wengi wanaofurahia pale unapokuwa kwenye changamoto mbalimbali, hivyo wanapoulizia unaendeleaje, siyo kwa kutaka kukusaidia, bali kufurahia magumu unayokuwa unapitia.

Kadiri watu wanavyojua mambo machache kuhusu wewe, ndivyo unavyowanyima nafasi ya kukusumbua, iwe ni kwa wema au kwa ubaya.
Hivyo hakikisha unadhibiti kwa kina nani anajua nini kuhusu wewe.
Kama umekuwa unaanika wazi kila kitu kuhusu wewe na kwa kila mtu, unajitengenezea matatizo mengi.

Kipindi cha nyuma nilipokuwa kwenye mkutano na watu na unafika wakati wa kula, nilikuwa nikieleza watu kuhusu ulaji wangu, nakula mara ngapi kwa siku na nini nakula na nini sili. Utaratibu huo wa ulaji kwangu ni tofauti kabisa na ilivyozoeleka. Hivyo niliona ni njia ya kuwasaidia watu kuboresha ulaji wao ili pia kuboresha afya zao na kudhibiti nguvu, umakini na uzito wa mwili.
Lakini nilikuwa naishia kushauriwa, ushauri ambao sijaomba na kubishiwa na watu wasiokuwa na uelewa.
Nililazimika kutumia nguvu nyingi kuwaelewesha watu kilicho sahihi, lakini niliishia tu kujichosha bure.
Siku hizi nimekuwa na uelewa mzuri, ninapojikuta kwenye hali kama hiyo naangalia kipi bora kufanya ili nisilazimike kueleza msimamo wangu ulipo. Hivyo natafuta sababu ya kutokuwepo kwenye eneo hilo au naamua kuungana nao.
Nimegundua kuacha kubishana na watu kwenye maeneo hayo kunaokoa nguvu zangu nyingi ambazo naweza kuzipeleka maeneo mengine sahihi.

Kwenye KISIMA CHA MAARIFA tunajenga jamii sahihi inayoweza kusaidiana na kushirikiana kwenye mambo yote muhimu na kwa tija. Nje ya jamii hii, chagua kwa tahadhari kubwa nani unawaeleza yanayoendelea kwenye maisha yako.
Hata baadhi ya watu wa karibu sana unaweza kuepuka kuwaambia baadhi ya mambo yako, kwa sababu hakuna namna wanaweza kuyasaidia, lakini pia unakuwa unawaweka kwenye wasiwasi mkubwa na ambao utazidisha tatizo kwako.

Magumu na changamoto ni vitu ambavyo tutaendelea kuwa navyo kila siku. Tunapaswa kuchagua kwa umakini watu gani tunawashirikisha kwa undani yale tunayopitia. Kisha wengine wote tunawajibu kwamba tunaendelea vizuri.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe