2943; Watakusumbua sana.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yako huwa unajiwekea vigezo vya watu wa aina gani ujihusishe nao.

Vigezo hivyo huwa vinategemea kile unachofanya na watu sahihi wa kuwalenga.

Mara kwa mara huwa unakutana na watu ambao hawakidhi vigezo ulivyoweka, lakini bado wanataka kushirikiana na wewe. Wanasisitiza sana ya kwamba wanahitaji nafasi hiyo.

Hapo unaweza kuingia huruma na kulegeza viwango ulivyojiwekea ili uweze kumpa mtu huyo nafasi.

Na hapo ndipo unapotengeneza tatizo ambalo litakusumbua sana kwenye maisha yako.

Kwani watu wote ambao unawalegezea viwango ndiyo huwa wanaishia kuwa wasumbufu sana kwako.

Hawatazingatia sala kuthamini kile unachowapa.
Na mbaya zaidi hawatafuata utaratibu uliopo, hivyo kutengeneza changamoto nyingi zaidi.

Watu ambao unalegeza viwango vyako ili uweze kushirikiana nao huwa wanaishia kukusumbua sana.

Hawa ni wateja ambao hawawezi kumudu bei iliyopo, wanakuomba sana punguzo na wewe unaona uwapunguzie ili mweze kwenda pamoja.
Unampunguzia na kinachofuata ni usumbufu mkubwa sana ambao hukuwa unautegemea.
Wateja wa aina hiyo huwa hawalipi kwa wakati na hata wanapolipa wanakulazimisha ufanye vitu tofauti na ambavyo umepanga kufanya.
Wanaona kwa kuwa wanakulipa, basi wanayo haki ya kukutumikisha vile wanavyotaka wao.
Ni mtazamo wa aina hiyo ndiyo unaokuletea usumbufu mkubwa.

Na pia ni wafanyakazi ambao hawawezi au hawataki kufuata utaratibu uliopo kwenye kazi.
Hawa huwa na utaratibu wao wenyewe, ambao huishia kuwavuruga wote wanaoshirikiana nao.
Inaweza kuwa ni mfanyakazi ambaye mara zote anachelewa kazini, au kwenye utendaji wake hazingatii viwango vilivyowekwa.
Wafanyakazi wa aina hiyo huwa wanaleta usumbufu mkubwa.
Unaweza kuendelea nao kwa sababu ya kitu fulani umeona kwao, lakini hizo tabia zake zitakukwamisha sana.

Kuondokana na usumbufu huu, tumia vizuri neno HAPANA.
Kama kuna mtu anataka mshirikiane ila hajakidhi vigezo ulivyojiwekea, mjibu hapana, haitawezekana.
Hata wakubembeleze kiasi gani watabadilika ili kuendana na vigezo vyako, ukisema ndiyo na kuvunja vigezo vyako unakuwa umenua matatizo ambayo yatakusumbua.

Kwa kutumia neno hapana kuna wengi utawakosa, ambao wataenda kwa washindani wako.
Hilo siyo jambo la kuhofia, badala yake ni la kufurahia, kwa sababu unakuwa umehamisha usumbufu kutoka kwako kwenda kwa washindani wako.

Kwa yeyote au chochote ambacho kipo chini ya viwango ulivyojiwekea, jibu ni HAPANA.
Badala ya kushusha viwango vyako ili kumpata kila mtu, unapaswa kupeleka nguvu zako kwenye kuwapata walio bora na wenye vigezo ulivyoweka.

Dunia ina utele, ondokana na fikra za uhaba kwamba watu wazuri hawapo. Ni wewe kuweka utulivu na msimamo katika kusimamia vigezo vyako bila kuvivunja kwa namna yoyote ile.

Kabla hujawaonea watu huruma na kulegeza vigezo ulivyoweka, jionee wewe mwenyewe huruma kwa matatizo unayokwenda kujitengenezea.
Ukiwa na huruma kwako mwenyewe na kutokutaka kupata usumbufu mkubwa, neno HAPANA ni rafiki yako wa karibu.

Kuna sababu ya kuwepo kwa vigezo mbalimbali vinapopaswa kufanyiwa kazi.
Ni pale unapokwenda kinyume na vigezo hivyo ndiyo unazalisha matatizo makubwa.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe