2944; Usifanyie kazi ushauri huu, kwanza.

Rafiki yangu mpendwa,
Kabla sijakushauri kitu chochote, huwa kwanza nakifanyia kazi ili kujua uwezekano wake na changamoto zake.
Hivyo ninapokushauri ufanye au usifanye kitu fulani, nakuwa tayari najua nini unakwenda kukabiliana nacho.

Sasa kuna kitu ambacho ndiyo nimeanza kukifanya na bado sijawa na matokeo yake, hasa kwa upande wa changamoto.
Hivyo kwa utaratibu wangu nisingepaswa kukuambia.
Ila kumekuwa na msukumo mkubwa kwangu wa kukushirikisha.

Hivyo nakushirikisha kama sehemu ya wewe kuona nini kinawezekana, ila siyo uanze kufanyia kazi mara moja.

Kabla ya kwenda kwenye kitu hicho, kwanza nikushirikishe jinsi nilivyokifikia.
Kwa miaka mingi nimekuwa nafanya mambo mengi kwa pamoja na nimekuwa naweza kuzalisha matokeo mengi na makubwa, ushahidi upo wazi kwenye matokeo mengi ambayo nimeshazalisha.
Lakini baada ya kutafakari kwa kina, nimeona nimekuwa natawanya nguvu zangu kwenye mambo mengi na kupata matokeo mazuri.
Ila kama nataka kupata matokeo bora kabisa, napaswa kukusanya nguvu hizo kwenye mambo machache.
Kama ambavyo jua likitawanyika kinatoa mwangaza, ila likikusanywa linawasha moto.

Hivyo basi nikachukua nafasi ya kupunguza mambo ninayofanya na kubaki na matatu tu; KUSOMA, KUANDIKA na KUKOCHI.
Hatua hiyo niliyochukua ghafla ikanifanya niwe na muda mwingi kuliko nilivyowahi kuzoea.
Nikafurahia muda huo mwingi, lakini ndani ya muda mfupi nikagundua muda huo unajazwa na vitu visivyokuwa na tija.
Ndiyo ni vitu vizuri, lakini haviwezi kunifikisha kwenye ubora ambao ulinisukuma kufanya maamuzi hayo.

Hivyo nikaona kuna maamuzi mengine makubwa zaidi ninayopaswa kufanya, ya kuhakikisha maamuzi niliyofanya awali yanakuwa na tija.
Na hapo ndipo nilipofikia maamuzi ambayo nakwenda kukushirikisha hapa, ambayo sikushauri uyafanyie kazi kwa sasa.

Kwa miaka mingi nimekuwa nakushirikisha code ya muda ambayo tumekuwa tunatumia.
Code hiyo ni 16/6/50; masaa 16 ya kazi kwa siku, siku 6 za kazi kwenye wiki (siku moja ya mapumziko) na wiki 50 za kufanya kazi kwa mwaka (2 za kupumzika).
Code hii inakupa masaa 16 × 6 × 50 = 4,800 kwa mwaka.
Ukigawa masaa hayo kwa muda wa kawaida wa kazi kwa wiki ambao ni masaa 40, unapata wiki 120 za kazi kwa mwaka.
Na ukigawa wiki hizo kwa wiki 48 ambazo ndiyo za kazi kwa mwaka kwa wengi, unapata miaka 2 na nusu.
Ina maana ukiishi code ya 16/6/50 kwa ukamilifu, kila ndani ya mwaka mmoja, unakuwa na miaka 2.5 ya kazi. Unakuwa na uzalishaji mara mbili zaidi ya wengine.

Lakini hiyo ni code ambayo kwa haraka sana imeniingiza kwenye changamoto za matumizi mabaya ya muda nilipoamua kuachana na mengi na kwenda na machache.
Hivyo nimelazimika kuanza code mpya.
Code hiyo ni 18/7/52; masaa 18 ya kufanya kazi kwa siku, siku 7 za kazi kwa wiki na wiki 52 za kazi kwa mwaka. Maana yake hakuna mapumziko kabisa.
Code hii inanipa masaa; 18 × 7 × 52 = 6,552.
Ukigawa masaa hayo kwa muda wa kawaida wa kazi kwa wiki ambao ni masaa 40, unapata wiki 163.8 za kazi kwa mwaka.
Na ukigawa wiki hizo kwa wiki 48 ambazo ndiyo za kazi kwa mwaka kwa wengi, unapata miaka 3.4.
Ina maana ukiishi code ya 16/6/50 kwa ukamilifu, kila ndani ya mwaka mmoja, unakuwa na miaka 3.4 ya kazi. Unakuwa na uzalishaji mara tatu zaidi ya wengine.

Umeona tofauti ya code hizo mbili, ni karibu mwaka mzima wa ziada.
Sasa kama itafanyiwa kazi vizuri, kitu ambacho ndiyo naendelea nacho, kwa hakika matokeo hayawezi kuwa ya kawaida.

Sasa kwa nini sikushauri ufanyie kazi hiyo code kwa sasa?

Kwanza utambue hayo masaa 18 siyo ya kuwa macho (tayari hilo unafanya) ni ya kufanya kazi na siyo mengine nje ya kazi (kitu ambacho hakuna wengi wanaweza kufanya).

Sababu ni nyingi, lakini chache za msingi ninazoziona kwa haraka ni;

  1. Kuna hatari ya kuharibu afya yako, kuanzia ya mwili kwa kupata maradhi, ya akili kwa kupata msongo na ya kiroho kwa kupata uchoshi.

  2. Kuna hatari ya kuvunja mahusiano yako mengi, hasa yale ya karibu kama ya ndoa, ndugu na marafiki.

  3. Kuna hatari ya kuonekana mtu usiyefaa kijamii kwa sababu huchanganani na watu kwenye mambo yao, iwe ni sherehe, misiba na matukio mengine.

Hizi ni hatari kubwa sana ambazo zinaambatana na hiyo code na madhara yake yanaweza kuwa makubwa.

Tuseme labda umeamua kuwa kichwa ngumu, licha ya kukushauri usifanyie kazi ushauri huu, wewe ukaamua uufanyie kazi, kuna mambo ya kufanya yatakayokuepusha na hizo hatari hapo juu;

  1. Kuwa na KWA NINI KUBWA, kwa nini uwe tayari kujitesa kwa viwango vya juu wakati ungeweza kwenda kawaida tu? Bila kwa nini kubwa sana, hutaenda mbali kabla hujarudi kwenye mazoea. Kama unaielewa vyema huduma tuliyopo, kuwa bilionea siyo kazi ndogo, hivyo tayari hiyo ni KWA NINI KUBWA.

  2. Zungukwa na watu sahihi wanaokuelewa na siyo wasiokuelewa na kukusema kwa mabadiliko yako. Kwa bahati mbaya sana wale wanaokuzunguka hawatakuelewa kabisa. Hivyo unahitaji kutafuta watu watakaokuelewa. Na kama upo kwenye huduma hizi, klabu za BM na za KISIMA CHA MAARIFA ni sehemu sahihi ya kuungana na wachache wanaoweza kukuelewa.

  3. Kuwa na ngozi ngumu sana, inayoweza kuvumilia kila aina ya mishale utakayoipata kutoka kwa wengi. Kwa kifupi ni uwe na uwezo wa kutokujali nani anafikiria au kusema nini juu ya maamuzi ya maisha yako. Uwe tayari kushindwa bila kukata tamaa. Na hili linahitaji uwe na falsafa bora kabisa unayoiishi na kuiamini. Na kama upo kwenye hii huduma kwa uhakika, falsafa ya KISIMA CHA MAARIFA, ukiishi kwa ukamilifu wake, hakuna kitakachoweza kukuteteresha.

Haya ni maamuzi magumu na makubwa ambayo sikushauri uyafanye kwa sasa, maana yatatikisa sana maisha yako.
Lakini kama tayari maisha yako yapo kwenye mtikisiko, hakuna ubaya kujaribu hili, kwa kuzingatia tahadhari ambazo nimeshakupa.

Ukijaribu na ukaumia, kitu ambacho lazima kitokee, kabla hujanilaumu nimekushauri nini, rudi usome hapa.
Sijariku kukimbia uwajibikaji, bali nakueleza wazi kila kitu jinsi kilivyo.

Na kama unashangazwa hayo masaa 18 ya siku nayatumiaje, kwa upana nimeyagawa hivi;
Masaa 5 ya kusoma.
Masaa 5 ya kuandika.
Masaa 6 ya kukochi.
Masaa 2 ya mengineyo, ambayo yanahusisha kazi lakini siyo hizo kuu tatu, mfano kujibu vitu mbalimbali.
Muda gani wa kufanya nini inategemea zaidi na siku, lakini napambana kwa kila namna mlinganyo huo wa siku uwepo.
Ndiyo nimelianza hili, uzalishaji na ufanisi unazidi kuwa juu, ila sijajua kwa mbeleni mambo yataendaje.
Mimi mwenyewe nina shauku ya kujua zaidi.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe