2946; Wasaidie kufanya maamuzi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kama ulikuwa hujui, moja ya wajibu wako mkubwa ni kuwasaidia watu kufanya maamuzi.
Kwa sababu watu wengi hawana ujasiri wa kutosha kufanya maamuzi yao wenyewe.
Siyo kwamba hawajui wanachotaka, wanajua sana, ila uthubutu wa kuamua ndiyo wamekosa.

Kama wewe unataka mambo yako yaende na usikwamishwe na yeyote au chochote, kuwa tayari kuwafanyia watu maamuzi.

Ili uweze kuwafanyia watu maamuzi, lazima ujue nini hasa wanachotaka.
Na ili uweze kujua kile ambacho watu wanataka hasa, unapaswa kuweka umakini mkubwa kwao.
Watu huwa wanadhihirisha wazi kile wanachotaka, hata kama hawakisemi moja kwa moja.
Matendo yao huwa yanaongea kwa sauti kuliko maneno.

Nitakupa mifano miwili, halafu utaendelea kujionea mwenyewe mifano mingine mingi inayokuzunguka.

Mfano wa kwanza ni kwenye mauzo. Anakuja mtu kwenye kile unachouza, anauliza maswali mbalimbali, anakijaribu kabisa, kinamfaa, lakini bado hafanyi maamuzi ya kununua.
Anakuambia wacha azunguke kwanza aone.
Huyu mtu anataka kununua, ila anashindwa kufanya maamuzi, kwa sababu bado ana wasiwasi.
Wajibu wako ni kumsaidia mara moja kufanya maamuzi.
Msaidie asiende kuhangaika bure huko pengine.
Mpe kile anachotaka kwa namna ambayo ni bora kabisa kwake na atakushukuru sana.
Wateja wengi wanahangaika kwa sababu kumekosekana wauzaji bora na wanaojua wajibu wao.

Mfano wa pili ni kwenye kuajiri.
Una mfanyakazi ambaye kila wakati anakupa changamoto.
Kila wakati anachelewa na kila makosa yanayojitokeza yanasababishwa na yeye.
Umekaa naye chini sana kumwelekeza, lakini hakuna kinachobadilika. Anachukua hatua siku chache, ila baadaye anarudi kwenye mazoea yake yanayoleta changamoto nyingi.
Huyu anahitaji sana umsaidie kufanya maamuzi.
Haitaki au haipendi hiyo kazi, ila hana uthubutu wa kusema hilo wazi.
Badala yake anafanya kwa vitendo.
Unachopaswa ni kumsaidia aachane na hiyo kazi, yaani kumfukuza kazi.
Unaweza kuwa unamwacha kwa sababu unamwonea huruma kwamba atakosa kazi, huku yeye akizidi kukushangaa kwa nini huchukui hatua.
Maana wanakuwa wameichoka hasa hiyo kazi, ila tu hawathubutu kuamua.
Ukiwasaidia kuamua, wao wenyewe watajisikia ahueni.
Unakuwa umewapa nafasi ya kwenda kutafuta na kufanya kingine wanachopenda au kujali zaidi.

Kwa mifano hiyo miwili nadhani umepata picha ya mingine mingi ambapo watu wanashindwa kufanya maamuzi.
Lakini hii haimaanishi sasa unakuwa wajibu wako kuwaamulia watu mambo yao.
Fanya hivyo kwa yale mambo yanayokuhusu moja kwa moja, ambapo watu kutokuamua kunakukwamisha.
Yasiyokuhusu achana nayo, jali biashara zako.

Unachotakiwa kujua ni kwamba watu kukubaliana na wewe haimaanishi kwamba watafanya.
Wengi wasio na uthubutu wa kuamua, huwa pia hawana uthubutu wa kukataa.
Hivyo watakubaliana na wewe kirahisi kabisa, lakini hawatatekeleza kile walichokubali, hata uwafanye nini.
Badala ya kushangazwa kwa nini watu wakubali kitu halafu wasifanye, wewe jua wanashindwa kufanya maamuzi.
Wasaidie kufanya maamuzi sahihi ili mambo yako yasikwame.

Kama una mtoto mdogo, ambaye siku nzima hajala chochote na kila unapojaribu kumlisha anakataa, hutamwambia, haina shida, utakula utakapotaka.
Utamlazimisha ale, kwa sababu unajua anapaswa kula, la sivyo ataleta matatizo zaidi.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kwenda na wale wote unaojihusisha nao, kuwa tayari kuwafanyia maamuzi pale wanapokukwamisha.
Kwa sababu wengi hawana uthubutu wa kufanya maamuzi wao wenyewe.

Usilalamike tena watu wanakukwamisha.
Umeshajua wanaogopa kufanya maamuzi.
Wafanyie maamuzi ili mambo yako yaweze kwenda.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe