2952; Hili basi linaenda wapi?

Rafiki yangu mpendwa,
Pata picha una safari yako ya kwenda eneo fulani.
Unafika stendi ya mabasi na kukata tiketi ya safari yako na kuelekezwa basi unalopaswa kupanda.
Unakwenda kwenye basi na muda siyo mrefu dereva anawasha gari kuondoka.
Kujihakikishia safari yako, unamuuliza dereva swali; “hili basi linaenda wapi?”
Dereva anakuangalia kwa umakini na kukujibu; “kusema kweli sijui basi linakokwenda.”

Kwa akili timamu, kitu cha kwanza utakachotaka kufanya ni kushuka kwenye basi hilo kabla hujaendelea kupotea.
Kabla hujataka kujua imekuwaje dereva kutojua mwelekeo wa safari, utataka kwanza usiendelee kupotea.
Na kwa hayo utakuwa sahihi.

Sasa tutoke kwenye mfano na tuje kwenye uhalisia na kumhoji dereva wewe.
Hiyo biashara unayoendesha, inaelekea wapi?
Ni maono yapi makubwa uliyonayo kwenye biashara unayofanya au nyingine yoyote.
Unajiona wapi kila baada ya muda fulani?
Kama huwezi kujijibu hayo maswali kwa uhakika, upo kwenye njia ambayo hujui kama ni sahihi au la.
Na huko ni kupoteza muda mwingi sana.

Ni lazima ujue kwa hakika kabisa hiyo biashara yako inaenda wapi.
Lazima ujue kila baada ya muda fulani itakuwa imefikia hatua fulani.
Yajue hayo yote kwa uhakika kabisa kwako na kaa kwenye njia sahihi ya kufika kule unakotaka kufika.

Biashara yako inaenda wapi na kila baada ya muda inakuwa wapi ndiyo kitu cha kuanza nacho kwenye safari yako.
Maana hayo ndiyo yataamua kila kinachopaswa kufanyika na kutokufanyika kwenye biashara hiyo.
Haina haja ya kuwa na mbio kama haupo kwenye njia sahihi.

Maono, malengo, mikakati na hatua za kuchukua ni sehemu muhimu ya safari yako ya kibiashara.
Hupaswi kufanya lolote kwa kubahatisha, bali unapaswa kuwa na mipango na mikakati unayofuata ili kufikia malengo na maono.

Unakosa shauku na hamasa au unahangaika na usumbufu usio na tija kwako ni matokeo ya kutokujua ni wapi kazi au biashara watu wanafanya zinaelekea.

Tumia biashara kama chombo cha kukufikisha kwenye yale maono makubwa uliyonayo kwenye maisha yako.
Na usikubali kuyumbishwa na chochote katika kuyapambania maono hayo unayokuwa nayo.

Watu wengi wapo kwenye biashara ambazo hawajui zinaelekea wapi hasa.
Hawawezi kupima ni hatua gani ambazo biashara hiyo inapiga kadiri inavyokwenda.
Hayo ndiyo yanayosababisha watu kukosa msukumo mkubwa wa kuzipambania biashara zao.
Hawajui ni matokeo gani ya kuvuna na kwa wakati gani kutoka kwenye biashara zao.

Hilo linawafanya wanabaki kuwa watumwa wa hizo biashara, kila wakati wakiwa wametingwa sana na uendeshaji wa biashara ambao unawategemea kwa asilimia 100.

Kama ambavyo utashuka haraka kwenye basi ambalo hujui linaenda wapi, ndivyo unavyopaswa kujitafakari haraka na kujua biashara yako inaelekea wapi.
Yajue wazi maono na mikakati iliyopo.
Kisha kaa kwenye mchakato sahihi wenye matokeo ya kila hatua unayotaka kufikia kupitia biashara hiyo.

Ukiamshwa usingizini na kuulizwa biashara yako inaenda wapi, unapaswa kuweza kujibu swali hilo kwa haraka na uhakika mkubwa.
Kama hutaweza kujibu hilo swali, unazurura tu na biashara yako, hakuna unakokwenda.

Usikubali kupoteza muda.
Jua kwa hakika unakokwenda ili ujisukume kupambana kwa kila namna kufika huko.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe