2960; Usiwauzie, wafundishe.

Rafiki yangu mpendwa,
Mauzo yanakuwa magumu kwa wengi kwa sababu wamekuwa wakikazana kuwalazimisha watu kununua.
Wanachosahau watu hao ni kwamba hakuna mteja anayependa kuona amelazimishwa kununua.

Kuuza ni kufundisha na kufundisha ni kuuza.
Wauzaji ambao wamekuwa wanaweka mbele kipaumbele cha kufundisha badala ya kuuza, wamekuwa wanaingiza kipato kikubwa sana.

Wafundishe wateja wako jinsi ambavyo unachouza kina manufaa kwao. Wajengee picha ya kitaswira kwenye akili zao ambayo wanajiona kabisa wakiwa na matokeo tofauti kwa kutumia unachouza.

Wafundishe wateja wako juhudi kubwa mnazoweka ili kuhakikisha wanapata kile ambacho wanaahidiwa. Wateja wanaweza wasielewe ni kazi kubwa kiasi gani inayowekwa kwenye kile wanachonunua na hivyo kutokukipa uzito mkubwa.
Lakini kwa kuwafundisha wanaelewa vizuri na wanajenga uaminifu mkubwa kwenye biashara.

Wakati mwingine wateja wanaweza kuwa tayari kulipa zaidi pale wanapojua nini hasa kinachofanyika kwenye kile wanachonunua.

Kama mteja hajawa tayari kununua kwako, jiulize ni kitu gani ambacho bado hujawafundisha na wakaelewa. Ukishajua hilo, unaweza kuboresha zaidi mchakato wako mzima wa mauzo, kwa kuhakikisha watu wanapata elimu sahihi itakayowasaidia kufanya maamuzi.

Mteja aliyeelimika ni mteja mzuri sana kununua, anakuwa mwaminifu na balozi mzuri wa biashara yako.
Ni wajibu wako kibiashara kuwaelimisha wateja wako wote kuhusu biashara yako na manufaa wanayokwenda kupata kwa kununua kwako.

Kuna mambo mengi kuhusu biashara zetu ambayo tunayachukulia poa kwa sababu tayari tumeshayazoea.
Lakini kwa upande wa wateja hawaoni kile tunachoona na mengi hawana uelewa sahihi kuhusu biashara yako.
Unapojenga msimamo wa kufundisha na kuonyesha, unajenga imani kwa wengi zaidi.

Ni kitu gani kikubwa unachowafundisha wateja wako ili washawishike kununua kwako?
Ni kwa namna gani wateja wanaona tofauti wakinunua kwako wanapolinganisha na kununua kwa wengine?
Hayo ni maswali ya kujiuliza kila wakati na kujipa majibu sahihi, kama unataka kufanya mauzo makubwa.

Kumbuka, usiuze bali fundisha, usiseme bali onyesha.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe