2962; Weka dau lako hapa.

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa sishauri mtu yeyote mwenye akili timamu acheze kamari au michezo mingine ya kubahatisha, ambayo kwangu yote hayo ni kitu kimoja.

Lakini mcheza kamari au michezo hiyo ya kubahatisha akisikia hayo, anakimbilia kukuambia kwenye maisha kila kitu ni kamari. Hapo akimaanisha hakuna chochote ambacho kina uhakika wa asilimia 100.

Ni kweli hakuna chenye uhakika wa asilimia 100 kwenye maisha, lakini bado kucheza kamari siyo sahihi kwa vipimo vyovyote vile.
Na kama unaendelea kusisitiza kwamba maisha ni kamari, basi unapaswa kuweka dau lako sehemu moja tu.

Sehemu hiyo ni wewe binafsi.
Jiwekee dau la kuweza kuyajenga maisha yako na kufikia mafanikio makubwa unayoyataka.

Weka kazi kubwa kwako binafsi na kwenye kile unachofanya na hapo utajiweka kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa.

Japokuwa hakuna chochote chenye uhakika kwenye maisha, kuweka juhudi kubwa sana kwako binafsi na kujipa muda wa kutosha, unajiweka kwenye nafasi kubwa na nzuri sana ya kufanikiwa.

Uzuri ni kwamba, unapoweka dau kwako mwenyewe, unakuwa na udhibiti mkubwa wa matokeo unayoweza kuyapata.

Ni J. P. Getty aliyewahi kusema kanuni ya uhakika ya mafanikio kwenye maisha ni kujua kwa hakika kile unachotaka, kujua gharama unayopaswa kulipa ili kupata unachotaka kisha kukubali kulipa gharama hiyo.

Kuweka dau kwako mwenyewe ndiyo kulipa gharama ya kupata kile unachotaka.
Uzuri ni dau lako unaliweka mahali ambapo unakuwa na udhibiti mkubwa na hivyo kuweza kupata matokeo mazuri.

Jikubali, jiamini na weka kila ulichonacho kwenye kupata kile unachotaka.
Jitoe kweli na ingia mzima mzima, usijaribu wala kubahatisha, wewe fanya.

Weka dau lako lote kwako binafsi na usihangaike na kingine chochote.
Umakini wako wote uweke kwako na kile unachofanya, kuhakikisha huna sababu yoyote ya kujizuia wewe binafsi.

Utakutana na magumu na changamoto mbalimbali, lakini kama hutakata tamaa, mbele ya safari utakutana na mazuri na yenye ubora.
Ni wewe tu uwe na imani na msimamo wa hapo ulipoweka dau lako.

Weka kila kitu ulichonacho kwenye kile unachotaka na dunia itakupisha ukipate.
Amini bila ya shaka yoyote kwamba utapata unachotaka na hata upitie nini, utakuwa na nguvu ya kuendelea na safari mpaka upate unachotaka.

Watu wengi wanaokuzunguka hawajui wapi wanataka kufika na wala hawapo tayari kulipa gharama za mafanikio.
Hao ndiyo utawakuta wakihangaika na kila aina ya kamari na kukimbizana na kila fursa mpya inayojitokeza.
Waepuke sana watu hao, wana nguvu kubwa ya kukurudisha nyuma.

Kitendo tu cha kujua kile unachotaka na gharama za kulipa unakuwa mbele sana kuliko wengi wanaohangaika na mengi yasiyokuwa na tija.

Inachukua muda mpaka kupata kile unachotaka, lakini ni muda ambao unakuwa umeuwekeza vyema.
Kwa wewe kukomaa na kile unachotana bila kuhangaika na mengine, utakuwa na muda sawa na wanaoshindwa, ila wao wanakuwa wameutawanya muda wao kwenye vitu vingi visivyo na tija.

Hilo neno TIJA ni la kuzingatia sana kwako. Muda ni rasilimali haba na yenye ukomo. Usiupoteze kwa kuhangaika na kamari nyingine ambazo ni za hasara kwako.
Kamari yako ni moja tu, kuweka dau lako lote kwako binafsi na kile unachotaka.

Ukishaweka dau lako, ni wewe kuinamisha kichwa chini na kuweka kazi ya uhakika kwa muda mrefu bila kukata tamaa.
Nasema uweke kichwa chini kwa sababu ukikinyanyua tu, unaanza kuona kamari nyingine zenye ushawishi lakini zisizokuwa na manufaa kwako.

Weka dau lako lote kwako mwenyewe, hata kama hutapata kile unachotaka, bado hutabaki pale unapokuwa umeanzia. Kuna hatua kubwa unazokuwa umezipiga kwenye maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe