2965; Siamini.

Rafiki yangu mpendwa,
Kumekuwa na sababu moja pendwa kwa watu wengi wanaoshindwa kufanya yale wanayopaswa kufanya.

Sababu hiyo ni; “SIna muda.”
Karibu kila mtu anatumia kauli hiyo kama sababu ya kushindwa kufanya makubwa.

Lakini niseme ukweli kabisa, mimi siamini kabisa kwamba hakuna muda.
Naamini bila ya shaka yoyote kwamba muda tayari upo.
Najua kwamba muda huwa haupatikani, bali unatengwa.

Kila mmoja wetu ana masaa 24 pekee kwa siku. Hakuna aliyeongezewa au kupunguziwa.
Hiyo ina maana kwamba iwe unafanya makubwa au madogo, muda wako wa siku ni ule ule.

Siiamini sababu ya sina muda kwa sababu nina uhakika kila mtu kwenye siku yake kuna muda mwingi anaoupoteza.
Katika masaa 24 ya siku, kuna muda ambao mtu anapoteza kwa kufanya mambo yasiyokuwa na mchango kwenye mafanikio anayoyatafuta.

Mtu anasema kwa kujiamini kabisa kwamba hana muda.
Lakini mtu huyo huyo unamkuta akizurura kwenye mitandao ya kijamii na wakati mwingine akibishana mambo yasiyokuwa na tija kabisa.

Ujumbe wangu kwako leo ni wewe kuikataa sababu unayojipa ya kwamba huna muda.
Kila unapotoa sababu ya mambo yako kutokwenda vizuri ni kukosa muda, ifute haraka.
Jiambie wazi kwamba muda unao mwingi tu, ni jinsi ya kuupangilia ndiyo kunakupa changamoto.

Kwenye maisha na mafanikio, unaweza kuzalisha sababu au ukazalisha matokeo.
Kwa wengi, sababu ni rahisi kuzalisha, lakini chochote rahisi huwa hakina manufaa. Ni bora uwe mtu wa kuzalisha matokeo, ni njia ngumu, lakini yenye matokeo mazuri.

Kataa sababu unayojipa kwamba huna muda.
Dhibiti na pangilia vizuri muda ambao tayari unao.
Ndani ya masaa yako 24 una nguvu ya kufanya makubwa na yatakayoacha alama hapa duniani.
Muda unao, utumie vizuri.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe