2974; Umekufa au hutaki.

Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya vitu muhimu unavyohitaji sana kwenye safari yako ya mafanikio ni msimamo usioyumbishwa.
Na msimamo huo haupaswi tu kuwa kwenye yale unayotaka, bali pia kwenye yale unayoahidi.

Unapaswa kufanya neno lako kuwa sheria.
Kwamba ukiahidi unatekeleza kama ulivyoahidi na siyo kuanza kuleta sababu.

Unahitaji kuwa na nidhamu ya hali ya juu sana ya kujisukuma kufanya kila ulichoahidi kwa namna ulivyoahidi.
Hilo litakujengea sifa ya kipekee na kufanya uaminike zaidi.

Japokuwa nidhamu na msimamo vinahitajika kwenye kila eneo, kuna eneo moja ambapo hivyo vina nguvu kubwa sana kwako.
Eneo hilo ni kwenye kujali sana muda.
Pale unapokubaliana na wengie kwenye jambo fulani, unapaswa kujali sana muda.
Unapaswa kutekeleza kwa muda mliokubaliana bila ya kuleta sababu.

Kama unataka uheshimike na kuaminiwa na kila mtu, wahi popote unakopaswa kuwa na pia tekeleza majukumu yako kwa wakati.
Hili ni jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wako kabisa.
Lakini wengi wamekuwa hawawezi kulitekeleza.

Watu wengi huwa ni wachelewaji kwenye kila miadi wanayokuwa nayo.
Na zaidi wanashindwa kutekeleza kitu ndani ya muda wanaopaswa kutekeleza, kama walivyoahidi au kupangiwa.

Na watu hao huwa hawana hata wasiwasi wowote, watakuja wamechelewa wakiwa tayari wana sababu kwa nini wamechelewa.
Watajitahidi kupangilia sababu zao ili kuonyesha kweli ni muhimu.

Lakini watu makini huwa hawazipi uzito sababu zozote ambazo mtu anazitoa pale anaposhindwa kukamilisha kile anachopaswa kukamilisha, iwe ni kuwahi mahali au kukamilisha majukumu fulani.

Watu makini wanajua kuna sababu mbili pekee za watu kushindwa kutekeleza wanachopaswa kutekeleza; wamekufa au hawataki.
Sababu nyingine yoyote tofauti na hizo mbili ni ya kujifanganya tu, haina mashiko yoyote.

Ili uweze kujenga imani na heshima kubwa kwa wengine, unapaswa pia kutumia sababu hizo mbili; umekufa au hutaki.
Yaani inakuwa hivi, pale unapoahidi au kutegemewa kwenye kitu fulani, unakifanya kweli kama ulivyoahidi au unavyotegemewa.
Ikitokea hujafanya, basi watu wajue wazi ni kwa sababu moja kati ya hizo mbili, umekufa au hutaki.

Kama umekufa, hilo linakuwa wazi, halihitaji maelezo.
Na kama hutaki, unaeleza wazi kwamba umeshindwa kufanya kama ulivyoahidi au ulivyotegemewa kwa sababu hutaki. Unawaeleza watu hilo kwa uwazi kabisa, na wala huhitaji kutetea zaidi.

Ni rahisi na inawapunguzia watu usumbufu unapoeleza hutaki kuliko unapotoa sababu nyingine zozote.
Sasa kama unaona siyo sahihi kuwaambia watu sababu ni hutaki, unajua cha kufanya, tekeleza kama ulivyoahidi au kutegemewa.

Kama inakuuma au hujisikii vizuri kuwaambia watu kwamba sababu ni hujataka, peleka maumivu hayo kwenye kutekeleza.
Tekeleza na watu wajionee na siyo kutengeneza sababu ambazo hazina mashiko.

Unapochelewa mahali kisha kueleza sababu ni umekutana na foleni, unadhani unamdanganya nani kwa mfano? Watu makini wanajua kama kweli ungekuwa unataka kuwahi, ungetoka mapema ili foleni isiwe kikwazo kwako.
Lakini kwa sababu hujataka sana kuwahi, umetoka kwa muda ambao foleni inakuchelewesha.

Unaposhindwa kutekeleza kile ulichoahidi na kuja na sababu nyingi za kwa nini umeshindwa, unadhani nani anazipa uzito?
Watu makini wanajua sababu ya kushindwa kutekeleza ni kwa sababu una vipaumbele vingine muhimu zaidi ya hilo uliloshindwa.

Utaona watu wanakuitikia na kuona umewapanga kwa sababu zako, lakini walio makini wanakuchora tu, na wanakuhukumu kwa hayo.
Wanajua wakati mwingine hawawezi tena kukutegemea kwa mambo ya aina hiyo.

Kwa kila jambo unalofanya watu wanalitumia kukuhukumu.
Ni bora ujiumize kwa nidhamu kali kabisa ili uhukumiwe vizuri na kuheshimiwa na kuaminiwa.
Kuliko ujisikie vizuri kwa kukosa nidhamu halafu uhukumiwe vibaya kwa kudharauliwa na kutokuaminiwa.

Huwezi kupata mafanikio makubwa kwenye maisha kama huna nidhamu kali binafsi, ambayo haileti sababu bali matokeo.
Huwezi kuheshimiwa na kuaminika kama huwezi kutekeleza mambo kwa wakati.

Simamia kwa ukali sana maeneo haya mawili; nidhamu binafsi na kujali muda, usiwe wa kukimbilia kutoa sababu kwenye maeneo hayo.
Hilo litakuwezesha kujenga sifa kubwa itakayokupa chochote unachotaka.

Msimamo wako uwe wazi kabisa, watu wakiona hujafanya kile ulichoahidi au unachopaswa, wajue wazi ni labda umekufa au hutaki.
Ifahamike hivyo na usiongeze sababu nyingine yoyote.
Jitese kwenye kukamilisha hilo, maana hakuna namna nyingine.

Ingekuwa sababu zinaleta mafanikio, kila mtu angekuwa na mafanikio makubwa.
Kwa sababu kila mtu ni mtoaji mzuri wa sababu.
Lakini tunajua vyema, sababu hazijawahi kuzalisha matokeo.
Usiwe mtu wa kutoa sababu, kuwa mtu wa kuzalisha matokeo, kuwa mtu wa kuwajibika.
Lazimika kwenda hatua ya ziada ili kutekeleza uliyoahidi au kukamilisha unayopaswa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe