2976; Muda na usumbufu.

Rafiki yangu mpendwa,
Inapokuja kwenye muda, msimamo wangu uko wazi mara zote, tatizo letu siyo muda, bali kile tunachofanya na muda tulionao.
Ninaamini, bila ya shaka yoyote kwamba muda tunao mwingi, ila tu tunautumia vibaya.
Kwamba tatizo kubwa la muda tulilonalo, siyo kwamba muda ni wa uhaba, bali tunao mwingi mpaka tunautumia vibaya.

Sasa kuna watu ambao wamekuwa wanaona hilo haliendani na uhalisia.
Wakiona ni mambo chanya tu ya kujiambia ili kujipa moyo, lakini uhalisia muda ni tatizo.
Kila mtu, ndani ya fikra zake anaamini muda ndiyo hautoshi. Anaona anahitaji kupata muda zaidi ili kukamilisha mengi aliyopanga.

Na hapo ndipo ninaporudi kwenye msimamo kwamba huhitaji muda zaidi, bali unachohitaji ni kupunguza usumbufu mwingi unaokuzunguka.
Hapo kwenye usumbufu ndipo pia wengi hawaelewi.
Wengi huona kwa kuwa hawafanyi mambo ya kupoteza muda, kama kuperuzi mitandao, kufuatilia habari na kubisha, basi hawana usumbufu.

Rafiki, iko hivi, usumbufu kwenye muda siyo tu kufanya mambo yasiyo sahihi, bali pia kufanya yaliyo sahihi lakini yasiyo na tija.
Yaani kukosa vipaumbele.

Kwa mfano kama una vitu 10 unavyopaswa kufanya kwenye siku yako, kisha unaanza kushambulia chochote kati ya hivyo kumi, unahangaika na usumbufu na utapoteza muda mwingi sana.

Unachotakiwa ni kuyaoroshesha kwanza mambo hayo kumi, kupangilia yapi ndiyo muhimu zaidi kuliko mengine, kisha kuanza kufanya yale yaliyo muhimu zaidi kabla ya ambayo siyo muhimu.
Na kila jambo lipangie muda wa kulifanya, maana changamoto nyingine ya muda ni jukumu lolote hujaza muda uliopo wa kulifanya.

Kwa kupangilia mambo kwa vipaumbele na kupangilia kila jambo kwa muda wake itasaidia sana kuondokana na usumbufu kwenye maisha na hivyo muda wako kutosha.

Kuna mambo mengine muhimu sana ya kukumbushana kwenye muda.

1. Franz Kafka amewahi kusema, “maana ya maisha ni kwamba yana mwisho.” Hili ni jambo rahisi kusahau, tujikumbushe mara kwa mara ili tusipotese muda kwenye mambo yasiyo na tija.

2. Tunapotesa muda mwingi kufanya mambo ambayo hatuyapendi, mambo ambayo hayatakuwa na umuhimu wowote miaka 10 ijayo. Mambo mengi yanaweza kuonekana muhimu sasa, lakini hebu jiulize miaka 10 ijayo yatakuwa na umuhimu kiasi gani?

3. Tunatumia muda wetu wa mapumziko kwa vitu ambavyo havitupi pumziko la kweli. Mfano kuperuzi mitandao ya kijamii, unaweza kuona umepumzika, lakini kwa uhalisia unajikuta umejichosha zaidi kwa yale uliyofuatilia.

4. Tunayaishi maisha yetu kama vile siku zetu hazina mwisho. Tunaruhusu vitu ambavyo hatuvipendi vitawale maisha yetu. Siku zinayoyoma na tunakuja kushtuka maisha yamefika ukingoni na hatujayafurahia.

5. Tunapaswa kuanza kuyafurahia maisha yetu sasa, siyo kwa sababu tuna kila kitu, bali kwa sababu tuna uhuru wa kuchagua tutumieje muda wetu na hivyo tumechagua kuutumia kwa mambo yenye tija kwetu.
Japo wengine kwa nje wanaweza kuona kama tunajitesa na hatuyafurahii maisha kwa namna tunatumia muda wetu, lakini sisi ndiyo tunaojua nini muhimu kwetu na wapi tunataka kufika.

Inapokuja kwenye muda, ukishafuata tu mkumbo umekwisha.
Utakuwa ‘bize’ muda wote huku hauna makubwa unayokamilisha.
Kataa kufuata mkumbo au kufanya mambo kwa mazoea.
Hoji kila unachoanza kufanya kama ndiyo kitu muhimu zaidi.
Kwamba kama ungekuwa na siku moja ya kuishi, je bado ungekifanya?
Kama jibu ni hapana acha kukifanya mara moja.
Peleka muda wako kwa yale yaliyo muhimu zaidi, yale ambayo hata kama ingekuwa siku yako ya mwisho hapa duniani, bado ungeyafanya.

Muda unaopeleka kwenye mambo yasiyo muhimu ndiyo unaokukwamisha kwenye yale yaliyo muhimu zaidi.
Tukae huko kwenye umuhimu na tija na muda tulionao utatosha sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe