2977; Furahia kushindwa.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye safari ya mafanikio ambayo tupo, hakuna kitu kizuri ambacho kila mmoja anakitaka kama ushindi.

Tunapenda sana ushindi, uwe ni mdogo mdogo au mkubwa, kwa sababu ni kiashiria kizuri kwamba tunaelekea kule tunakotaka kufika.

Japokuwa kushinda kunaleta hali ya kujisikia vizuri wakati huo wa ushindi, huwa pia kunaleta hali ya mazoea, kujiamini kupitiliza na kudumaa.

Ushindi unaleta mazoea kwa sababu mtu anaendelea kurudia yale yale yaliyompa ushindi, kitu kinachokuja kumpa anguko kubwa.

Kujiamini kupitiliza kunakotokana na ushindi ni pale mtu anapoona kwa kuwa amepata ushindi kwenye jambo moja, basi anaweza kupata ushindi kwenye kila jambo. Hiyo hupelekea kujaribu vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wao na kupata anguko.

Ushindi pia unaleta kudumaa, kwani mtu anaposhinda anaona tayari anajua kila kitu na hahitaji tena kujifunza wala kujaribu vitu vipya. Ni udumavu huo ndiyo unaopelekea anguko kubwa la baadaye.

Upande wa pili wa kushinda ni kushindwa.
Hakuna anayependa kushindwa, kwa sababu huwa kunaonekana ni kiashiria cha uvivu, uzembe na ujinga.
Lakini kushindwa kuna faida zake, ambazo ni ustahimilivu, unyenyekevu na mabadiliko.

Kushindwa kunamjengea mtu ustahimilivu wa kuvuka magumu anayokutana nayo ili aweze kupata anachotaka. Anayeshindwa anakuwa imara zaidi kuliko anayeshinda.

Unyenyekevu ni zao jingine muhimu la kushindwa, ambapo watu wanakumbushwa kwamba pamoja na jitihada unazoweza kuweka, bado kuna mambo nje ya uwezo wako yanaweza kuathiri ushindi wako. Unyenyekevu unakufanya uweze kujifunza na kuendelea kuwa bora.

Kushindwa pia kunaleta hali ya mabadiliko. Kwa kufanya kitu kwa namna fulani na hatimaye ukashindwa, inakulazimu kuangalia nini kimesababisha ushindwe na hapo kubadili baadhi ya vitu ili kuweza kupata ushindi baadaye.

Kushindwa pia ni kiashiria kwamba unajaribu vitu vipya na vikubwa. Maana kama unapata ushindi kila mara, ni dhahiri unafanya vitu vidogo na vya kawaida.

Furahia kushindwa, jiwekee malengo na mipango mikubwa ambayo unaweza kushindwa na hilo litakupa funzo kubwa.
Na pale unaposhinda, haraka sana weka malengo mengine makubwa zaidi badala ya kubaki kwenye ushindi huo ambao utakufanya uwe mzembe.

Tunapenda sana ushindi, lakini kwa bahati mbaya sana hakuna tunachojifunza kwenye ushindi, zaidi ya kujenga uzembe.
Tufurahie kushindwa, maana ndipo penye somo kubwa sana kwetu.
Ni kushindwa ndipo panatusukuma tuwe bora zaidi ya tulivyokuwa.

Unaposhinda usiridhike na kujipa usingizi mnono, badala yake badili lengo liwe kubwa zaidi ili likusukume na kukunyima usingizi.

Nimalizie kwa usemi huu maarufu sana ambao huwa unasema nyakati ngumu huwa zinatengeneza watu imara, watu hao imara wanatengeneza nyakati rahisi, nyakati hizo rahisi zinatengeneza watu dhaifu na watu hao dhaifu wanatengeneza nyakati ngumu.

Ushindi mfululizo ni laana, siyo baraka. Inahitaji mtu uweze kupuuza sana ushindi ndiyo uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe