2978; Biashara rahisi kufanya.

Rafiki yangu mpendwa,
Swali la ni biashara gani rahisi kwa mtu kufanya ni swali ambalo nimekuwa naulizwa kila mara na watu.
Kipindi cha nyuma nilikuwa nakazana kuwaelewesha watu ni biashara gani zinaweza kuwafaa watu kulingana na hali wanazokuwa nazo.

Lakini kwa uzoefu ambao nimeshajijengea mpaka sasa kwenye biashara, nimeachana kabisa na kushauri watu kuhusu biashara rahisi kwao kufanya.
Mtu anapokuja kwangu na swali ipi biashara rahisi kufanya, namwambia sijui, ili tu kuepusha ubishani kama nitamweleza urahisi siyo kigezo sahihi cha kuingia kwenye biashara.

Halafu kuna wale wanaokuja na wazo la biashara tayari, wakitaka ushauri wa ziada. Ninapowauliza kwa nini wamechagua biashara husika na wakanijibu ni rahisi, nao naangalia namna ya kuachana nao kwa usalama kabla hatujaingia kwenye ubishani.
Siyo kwamba hoja ninayokuwa nayo haiwezi kustahimili ubishani, bali ni ubishani ambao hauwezi kuzaa matunda, maana bado watu watakabi na kile walichokuja nacho.

Iko hivi rafiki, kwenye maisha kuna vitu rahisi na vitu sahihi.
Kwa bahari mbaya sana, vitu sahihi huwa siyo rahisi na vitu rahisi pia siyo sahihi.

Biashara ambayo ni rahisi ni biashara ambayo siyo sahihi kwako kufanya.
Kwa sababu kila mjinga atakimbilia kufanya biashara hiyo.
Na unawajua wajinga, watakimbilia kufanya mambo rahisi kwenye ushindani wa kibiashara kama kupunguza bei, kitu kinachowaathiri wote.

Kila biashara huwa zina matatizo na changamoto mbalimbali. Ni matatizo hayo ndiyo yanayotengeneza fursa kwenye biashara husika.
Kadiri biashara inavyokuwa na matatizo na changamoto nyingi, ndivyo pia inavyokuwa na fursa kubwa.
Lakini pia ndivyo wengi wanakimbia kufanya biashara hiyo na hivyo ushindani kuwa mchache.

Hili ndiyo tunaloona kwenye hizi zama za maendeleo makubwa ya teknolojia. Baadhi ya biashara zimevamiwa sana na wengi kwa sababu ya urahisi uliopo kwenye kuzifanya.
Sasa na wewe ukizikimbilia kwa sababu ya urahisi wake, unakuwa umepeleka shingo yako kwenye shoka.

Kwa kila biashara unayofanya, hakikisha kuna kitu cha tofauti unachopeleka kwenye biashara hiyo, kitu ambacho wengine hawapo tayari kukiweka.
Hakikisha kuna ugumu ambao wengine wanauona na unawatisha, wakati wewe unauona na kuweza kuutatua.

Swali unaloweza kuwa nalo ni vipi kama biashara unayoipenda sana ndiyo ambayo pia ni rahisi kufanya na kila mtu anakimbilia kuifanya?
Kwanza hakikisha ndiyo unaipenda kweli na siyo unachanganywa na urahisi wake.
Halafu sasa, kama utaingia kuifanya, jua kuna anguko ambalo biashara hiyo itapitia na baada ya hapo wale wenye nguvu ndivyo wataendelea.
Hivyo wewe jenga nguvu ambayo itakuwezesha kuendelea baada ya anguko.

Ninachosema ni watu wanaweza kukimbilia kwenye biashara kwa sababu ni rahisi na wakakimbilia kushusha bei kama njia ya kushindana.
Kila mtu anashusha bei na hatimaye hakuna anayetengeneza faida. Kinachotokea ni anguko ambalo linawaondoa kabisa walio dhaifu.
Ukiwa imara utavuka anguko hilo na kuendelea kuwa imara.

Jambo la muhimu sana, kama mfanyabiashara usilalamikie ugumu wa biashara, badala yake ufurahie.
Ni ugumu wa biashara ndiyo unaokupa wewe fursa.
Ni ugumu huo ndiyo unawazuia wajinga wasiingie kwenye hiyo biashara na kuja kuivuruga.
Biashara sahihi huwa zinakuwa ni ngumu na biashara sahihi kwako ni ile ambayo ugumu wake kwako ni rahisi kuukabili kuliko wengine walio wengi.

Jikumbushe kila mara, rahisi na sahihi. Ikiwa rahisi siyo sahihi na ikiwa sahihi siyo rahisi. Utaepuka mengi ya kukupotezea muda kama utazingatia kanuni hii muhimu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe