2981; Fanya kinachopaswa kufanyika.

Rafiki yangu mpendwa,
Ili uweze kupata matokeo makubwa unayoyataka, lazima ufanye mambo mapya, makubwa na magumu.
Na ili uweze kufanya mambo hayo magumu, lazima ujitoe kafara.

Unapaswa kufanya kinachopaswa kufanyika na siyo unachotaka kufanya au unachoweza kufanya.
Unapaswa ujitoe kupitiliza na siyo kujiwekea ukomo wa nini unaweza na nini huwezi.

Ni mambo magumu yanayokutaka uteseke sana kwenye kuyafanya.
Lakini hata ukiyafanya kwa kuteseka, bado haimaanishi mafanikio yako ni uhakika.

Na hapo ndipo wengi hukwama.
Wengi hujiambia vipi kama wakijitoa sana na bado wasipate wanachotegemea, si watakuwa wamejitesa bure?

Wote walioshindwa ndiyo huwa wanawaza hivyo na ndiyo maana wameishia kushindwa.

Waliofanikiwa huwa wanawaza tofauti.
Wanawaza kwamba wajibu wao ni kujitoa kwa kila namna kwenye kufanya kile wanachopaswa kufanya, bila kujali matokeo yatakujaje.
Wanajua kilicho kwenye udhibiti wao ni hatua wanazochukua na siyo matokeo yanayokuja.

Wanaofanikiwa kuna nyakati wanajitoa kweli kweli na bado hawapati matokeo bora.
Lakini kwa kuwa hawakati tamaa, kwa kuendelea kufanya wanakuja kukutana na matokeo bora kabisa baadaye.

Hakuna matokeo yoyote makubwa ambayo yamewahi kupatikana kwa kufanya vitu vya kawaida.
Mafanikio yoyote yale yanataka mtu ujitoe sana kafara, uache vitu unavyopenda na ujiumize hasa.
Machozi, jasho na damu huwa vinaambatana na mafanikio yoyote makubwa.
Kama unafikiri kuna namna ya kukwepa haya na bado ukapata mafanikio makubwa, unajidanganya.

Maisha ni kuchagua mateso,
Kuwa tajiri kuna mateso yake, katika kuutafuta, kuutunza na hata kuukuza utajiri.
Na hata kuwa masikini pia kuna mateso yake, kuishi kwa kukosa yale muhimu unayotaka.
Tofauti kwenye maisha zinaletwa na mateso gani ambayo mtu yupo tayari kuyavumilia.

Pale unapotaka kitu chochote kile kwenye maisha yako, kuwa tayari kujitoa kupitiliza katika kukiendea.
Usijizuie wala kujionea huruma, jitoe hasa kwa kuhakikisha unafanya kila unachopaswa kufanya.
Usijali matokeo gani yatakuja, wewe fanya kwanza.

Ili uweze hilo ni lazima uache kujali watu wanasema au kukuchukuliaje.
Watu wa kawaida huwa wana tabia ya kuwacheka wale wanaojaribu makubwa halafu wakashindwa.
Sasa kama utajali hilo, hakuna chochote kikubwa utakachoweza kufanya, kwa sababu watu wa kawaida huwa hawana kazi nyingine zaidi ya kuhangaika na mambo ya wengine.

Wewe jali mambo yako, fanya unachopaswa kufanya bila kujali unaumia kiasi gani au wengine wanakuchekaje.
Kuna siku utakuwa unachekelea, wakati wao wanalia.
Na pia kumbuka, wengi wanaokucheka pale unaposhindwa, wanatumia hiyo kama fursa ya kujipooza na mateso makali wanayokuwa wanapitia.

Hakuna mtu mwenye furaha na maisha yake anafurahia kushindwa kwa mtu mwingine.
Hivyo badala ya kuwazingatia watu wa aina hiyo na ukaacha kufanya unapaswa uwaonee huruma kwa mateso makali wanayopitia, kiasi kwamba raha pekee kwao ni kuona wengine nao wanateseka.

Hata wale unaoona wanatumia nguvu nyingi sana kuonyesha wana furaha, labda kuweka mambo yasiyo halisi kwenye mitandao ya kijamii, kufanya starehe kupitiliza na mengine, hawafanyi hivyo kwa sababu wana furaha sana, bali wanafanya hivyo kwa sababu wanataka kuficha mateso makali wanayopitia.

Zote hizo ni sababu za msingi sana kwa nini unapaswa kujitoa kweli kwenye kile unachotaka bila kujali wengine wanafanya nini au wanakuchukuliaje.
Huwa wanasema mafanikio ni kama tai, mara nyingi utalazimika kuruka mwenyewe hata kama mazingira ni hatarishi kiasi gani.

Ingekuwa rahisi kila mtu angefanya na ingekosa thamani.
Ni ngumu ndiyo maana wengi hawafanyi na thamani yake inakuwa kubwa.
Usitake iwe rahisi, bali pambana wewe uwe mgumu.

Endelea kufanya kila kinachopaswa kufanyika. Ndiyo njia pekee ya kujenga na kutunza mafanikio makubwa unayoyataka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe