2982; Kupangiwa cha kufanya.

Rafiki yangu mpendwa,
Tunajua maisha ni magumu na yana changamoto za kila aina.
Lakini sehemu kubwa ya ugumu wa maisha huwa tunaisababisha sisi wenyewe.
Hasa kutokana na matarajio tunayokuwa nayo kwenye yale tunayofanya.

Kwenye kila eneo la maisha, ugumu na urahisi huwa vinapishana.
Chochote ambacho tunakifanya kwa urahisi huwa kinakuwa kigumu na chochote ambacho tunakifanya kwa ugumu huwa kirahisi.

Tuchukue mfano wa biashara, watu wengi huwa wanaingia kwenye biashara kwa kuona itakuwa kitu rahisi kwao kufanya.
Wanaona watakuwa huru kufanya kile wanachotaka kwa namna wanavyotaka.
Wengi hujinasibu kabisa kwamba hakutakuwa na wa kuwapangia nini wafanye.

Mtazamo huo unafanya mambo yawe magumu sana.
Kwa sababu mtu anaianza biashara kama vile tayari ameshafanikiwa.
Akichagua nini afanye na nini asifanye.
Na kuona hakuna anayepaswa kumpangia kitu cha kufanya.

Matokeo ya hayo ni mambo kuwa magumu na hata biashara kushindwa.
Kushindwa kuweka juhudi sahihi kunakopelekea matokeo bora yasipatikane.

Kwa sababu mtu anapokuwa kwenye biashara anakuwa bosi wake mwenyewe, ambaye anaamua yeye mwenyewe atumieje muda wake, ni muhimu sana akawa na nidhamu kali binafsi.

Mtu anayeingia kwenye biashara na kuwa tayari kutoa muda wake kwa kila jambo bila kujali umuhimu wake, anayetaka kumfurahisha kila mtu, hawezi kupata mafanikio makubwa.

Ni yule anayekuwa mgumu kwake yeye mwenyewe, akijisimamia kufanya yaliyo sahihi na muhimu hata kama siyo anayopendelea kufanya ndiye anayefanikiwa.

Tumekuwa tunaona watu wengi wakifanya vizuri wanapokuwa wameajiriwa, kwa sababu wanapangiwa cha kufanya na kulazimika kukifanya hata kama hawataki.

Lakini watu hao hao wakienda kujiajiri wenyewe au kufanya biashara wanashindwa vibaya kwa sababu wanakuwa hawana wa kuwapangia cha kufanya na wao wenyewe hawawezi kujisukuma wafanye magumu wasiyoyapenda.
Hilo linafanya wahangaike na yaliyo rahisi na yasiyo na tija, kitu kinachopelekea kushindwa.

Kama mfanyabiashara mwenye uhuru na muda wako, hakikisha unaweza kujipangia kufanya mambo magumu na usiyoyapenda na kuyafanya kwa viwango vya juu kabisa.
Kama huliwezi hilo peke yako, tafuta mtu (Kocha) au watu (Kikundi cha uwajibikaji au bodi) ambao watakupangia cha kufanya na utafanya bila ya ubishi.

Kabla ya kuingia kwenye biashara, kila mtu huona biashara ni rahisi na mafanikio ni ya uhakika.
Lakini kila mtu anapoingia kwenye biashara mambo yanabadilika, zinakuwa ngumu na mafanikio hayaonekani.
Tatizo linaanzia kwenye kuingia na mtazamo huo wa urahisi na hivyo kufanya kila kitu kwa urahisi.
Matokeo yake ni unazalishwa ugumu ambao unakuwa ni kikwazo kikubwa.

Ukitaka mambo yako yaende kirahisi, anza kwa kuwa mgumu kwako wewe mwenyewe.
Hilo litakusukuma kufanya yaliyo magumu na sahihi badala ya kukimbilia yaliyo rahisi.

Na kama unajitapa hutaki kupangiwa cha kufanya, kwa sehemu kubwa umeshapotea.
Kinachoweza kukuokoa ni nidhamu kali binafsi, nidhamu ambayo wengine wanaona unajitesa.
Nje na hapo hutoboi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe