2983; Ongeza kasi ili kuwa imara.

Rafiki yangu mpendwa,
Kama umewahi kuendesha baiskeli unajua kitu kimoja, kama inayumba yumba, ili kuifanya iwe na mwendo imara na wa utulivu, unapaswa kuongeza kasi zaidi.
Ndiyo kwa kuiweka baiskeli kwenye mwendo wa kasi kubwa, unaipa utulivu na uimara mkubwa kwenye mwendo wake.

Hivyo pia ndivyo kwenye maeneo mengi ya maisha yetu, kama tunataka uimara, tunapaswa kuongeza kasi zaidi.

Chukua mfano wa biashara, kinachofanya biashara ziwe na changamoto nyingi na hata kufa ni kasi ndogo inayokuwepo kwenye biashara hizo.
Kwa kasi hiyo ndogo, wamiliki wa biashara hizo hujikuta wanasumbuliwa na usumbufu mwingi hivyo kuondoa umakini wao kwenye biashara hizo.
Hilo linatoa mwanya kwa biashara hizo kualika changamoto nyingi na hata kupelekea anguko.

Hata ushindani kwenye biashara, huwa unakuwa mkali kwenye biashara zinazoendeshwa kwa kasi ndogo.
Kasi inapokuwa kubwa, wale wasio imara huwa wanakimbia wenyewe na hivyo kupunguza ushindani.

Lakini pia hilo linaenda mpaka kwenye ukuaji wa timu. Biashara zisizokuwa na timu au ambazo timu yake ni ndogo huwa zinakuwa dhaifu na kwenye hatari ya kushindwa.
Lakini biashara zenye timu kubwa na nzuri, inayofanya kazi kwa mfumo sahihi, inakuwa imara na kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Kinachofanya kasi ilete uimara ni umakini mkubwa ambao mtu anauweka kwenye kitu pale kasi inapokuwa kubwa.
Kasi inapokuwa ndogo, umakini unagawanyika na usumbufu kuingilia.
Lakini kasi inapokuwa kubwa, umakini unakusanywa na usumbufu unawekwa pembeni.

Chochote ambacho siyo imara kwenye maisha yako, jiulize ni kasi gani unayoweza kuiongeza kwenye kitu hicho ili kukifanya imara zaidi.
Ongeza kasi bila kuhofia, kwa sababu kasi hiyo inajenga uimara mkubwa unaochangia ukuaji mkubwa pia.

Kwenye biashara;
Ongeza kasi ya ukuaji,
Ongeza kasi ya kujifunza,
Ongeza kasi ya malengo,
Ongeza kasi ya kuchukua hatua mpya,
Ongeza kasi ya kuajiri,
Ongeza kasi ya kuwahudumia wateja,
Ongeza kasi ya kutafuta wateja wapya,
Ongeza kasi ya kufuatilia wateja,
Ongeza kasi ya kujaribu vitu vipya,
Ongeza kasi ya kuitangaza biashara.

Kasi ni nguvu inayohitajika sana ili kufanya vitu kuwa na uimara mkubwa wa asili.
Wengi huhifia kwamba kasi inakuwa na hatari ya anguko.
Lakini hiyo itatokana na kasi ya kiholela.
Ongeza kasi iliyopangiliwa na utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.

Kila umapokuwa njia panda na hujui nini cha kufanya, anza kwa kuongeza kasi, itakufanya ujue kwa haraka unachopaswa kufanya na hivyo kuendelea au kubadilika kulingana na hali inayokuwepo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe