2986; Wewe na ndoto yako kubwa.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwa bahati nzuri sana, kila mmoja wetu tayari ana ndoto kubwa ya maisha yake.

Ila kwa bahati mbaya, wengi hawathubutu kuzipambania ndoto hizo, kutokana na aina ya watu ambao wanawazunguka.

Wewe unapaswa kuijua na kuipambania ndoto yako bila kujali kitu kingine chochote.

Ndoto yako kubwa inapaswa kuwa kipaumbele namba moja kwako.
Unapaswa kuipambania kila siku bila kuchoka wala kukatishwa tamaa.

Usiruhusu mtu yeyote au kitu chochote kusimama kati yako na ndoto yako kubwa.
Kuwa tayari kusambaratisha yeyote au chochote kinachokuwa kikwazo kwako.

Kwenye hii safari ya kupigania ndoto zako, unahitaji watu ambao wanakuunga mkono na kukufanya kuwa bora zaidi.
Wa kukukatisha tamaa na kukufanya uanguke tayari wapo wengi, huhitaji wa ziada kwenye hilo.

Ieleweke wazi kwamba hutamruhusu mtu yeyote au kitu chochote kikuzuie kufikia ndoto yako kubwa.
Watu wakuone ni mtu poa na usiye na mengi pale wanapoheshimu ndoto zako na kukusaidia kuzifikia.
Lakini wale wanaokuwa kikwazo kwa ndoto zako, wafanye wayaone makucha yako halisi, wasambaratishe vibaya sana.

Zoezi la kufikia ndoto kubwa za maisha siyo rahisi hata kidogo, ndiyo maana wengi hawazifikii, kwa sababu wanataka kuonekana wema na kumfurahisha kila mtu.

Hatua ya kwanza na muhimu kwa wewe kufikia ndoto yako kubwa ni kutokujali.
Hupaswi kujali kingine chochote isipokuwa ndoto zako ambazo ndiyo kipaumbele cha kwanza kwako.

Hupaswi kujali hata kidogo watu wanakuchukuliaje au wanajisikiaje kuhusu wewe kupambania ndoto yako kubwa.
Siyo wajibu wako kuwapangia watu wakuchukulieje au wajisikieje, hayo ni majukumu yao binafsi.
Jukumu lako kubwa ni ndoto yako.

Huenda kwa kusoma hapa unajiambia hiyo ni roho mbaya kutokujali kingine chochote isipokuwa ndoto yako.
Na jibu ni kweli, kwa sababu kwa aina ya jamii tunazoishi, huwezi kufanikiwa bila kuonekana una roho mbaya.
Tafsiri ya roho mbaya kwa jamii ni mtu anayekwenda kinyume na matakwa ya wengine kwenye jamii.
Sasa kama haupo tayari kwenda kinyume na matakwa hayo, huwezi pia kufikia ndoto yako kubwa.

Hivyo kama unasikia watu wanasema una roho mbaya, badala ya kuumia unatakiwa kufurahi. Kwa sababu ni kiashiria kwamba umeweka kipaumbele kwenye ndoto zako na kupuuza mengine.
Lakini kama kweli unazipambania ndoto zako, hutapata hata muda wa kujua wengine wanakusemaje.

Hili la kutokujali haimaanishi kuwaumiza watu kwa makusudi.
Kutokujali kunaenda mpaka kutojisumbua na watu kwenye mambo yasiyohusika na ndoto yako kubwa.
Pia kunaendana na kuwajua watu mapema na kuwachuja, kwa kuwaondoa wote wasiokuwa na mchango kwa ndoto yako kubwa.

Katika kupambania ndoto yako kubwa, kuwa tayari kumpoteza mtu yeyote au kitu chochote kinachokuwa kikwazo kwako.
Haijalishi ni nani na mmetoka naye wapi, kama hana tena heshima kwa ndoto kubwa ya maisha yako, anapaswa kuonyeshwa ulipo mlango wa kutokea.

Pata picha unavuka kwa mtumbwi mto wenye mamba wakali.
Una dakika chache za kuvuka kwa haraka kabla hujashambuliwa na kuwa kitoweo.
Unakazana kupiga makasia kwenye mtumbwi wako ili kuvuka haraka.
Ila kwa bahati mbaya sana, mtu uliyeambatana naye yeye anakazana kutoboa mtumbwi huo.
Unajua kabisa anachofanya ni hujuma na hivyo unajua anachostahili.
Haijalishi ni nani, yeyote anayezuia harakati za mtumbwi kufika upande wa pili ni adui na anafaa kuwa chakula cha mamba.
Mtu wa aina hiyo anapaswa kutoswa majini ili mtumbwi uweze kuendelea.
Hivyo ndivyo ilivyo kwenye kuzipambania ndoto yako kubwa.
Kuna watu wengi sana unatakiwa kuwatosa kwenye maji waliwe na mamba ili uweze kuendelea na safari yako.

Haya siyo mambo rahisi kufanya.
Na hapo tunarudi kwenye msingi wetu muhimu; RAHISI SIYO SAHIHI NA SAHIHI SIYO RAHISI.
Ni wewe tu uchague kama unataka kufikia ndoto yako kubwa na kuwa tayari kujitoa kwa kila namna au unataka kwenda na maisha bila kujisumbua.
Elewa tu ni maamuzi gani unafanya ili matokeo yanapokuja yasikushangaze.

Nimalizie kwa kujibu kitu unaweza kuwa unajiuliza, kwa nini nasema ndoto yako kubwa ndiyo inapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwako na siyo familia au watu wengine wa karibu?
Jibu ni hili, bila ya wewe kupambania na kufikia ndoto yako kubwa, huwatendei haki watu wengine wote kwenye maisha yako.
Hata kama unasema unawapenda kiasi gani, kama hufikii ndoto yako kubwa, unakuwa umejipunja wewe mwenyewe na hata wao pia.

Utakuwa na manufaa kwako, kwa wengine na hata kwa dunia nzima kama utapambania na kufikia ndoto yako kubwa.
Hiyo ndiyo sababu inapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kabisa kwako.

Wewe na ndoto yako ndiyo vitu pekee ambavyo havipaswi kutenganishwa kwa namna yoyote ile.
Ila vingine, kuwa tayari kuvisambaratisha kama vinaingia kati yako na ndoto yako kubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe