2987; Hatua tano za kutatua tatizo lolote.

Rafiki yangu mpendwa,
Matatizo ni sehemu ya maisha.
Kadiri ndoto zako zinavyokuwa kubwa, ndivyo pia matatizo unayokutana nayo yanavyokuwa makubwa.
Hapa tunakwenda kujifunza hatua tano za uhakika za kutatua tatizo lolote lile.

Hatua ya kwanza ni kulijua tatizo.
Ipo kauli inayosema kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua.
Kwa kujua tu kwamba kuna tatizo, unakuwa hatua ya mbele zaidi maana wengi hukataa uwepo wa tatizo.
Tatizo ni pale matokeo yanapokuwa tofauti na matarajio.
Hivyo kulijua tatizo ni kuanza na kujiuliza ni matokeo gani uliyoyataka na yapi ambayo umeyapata.
Kumbuka matokeo halisi yanapokuwa tofauti na matarajio yaliyokuwepo, kuna tatizo.

Hatua ya pili ni kujua chanzo au kisababishi cha tatizo.
Kila kitu kwenye maisha kinasababishwa.
Na kwa bahati mbaya au nzuri, matatizo yote kwenye maisha yetu yanasababishwa na watu, iwe ni sisi wenyewe au wengine.
Kujua chanzo au sababu ya tatizo unapaswa kujiuliza ni kitu gani watu wanafanya au hawafanyi na kupelekea tatizo kutokea.
Ni hivyo tu, tatizo litatokana na vitu ambavyo watu wanafanya au kushindwa kufanya. Ukichunguza hayo mawili utaweza kujua chanzo halisi kwa kila tatizo.

Hatua ya tatu ni kujua nini cha kufanya ili kutatua tatizo.
Baada ya kujua chanzo au kisababishi cha tatizo, kinachofuata ni utatuzi wa tatizo.
Kwenye kutatua tatizo, unapaswa kujiuliza nini cha kufanya ili kupata matokeo unayotarajia.
Umeshajua nini watu wanafanya au hawafanyi hivyo kusababisha tatizo.
Hivyo hatua ya utatuzi siyo ngumu, ni kufanya watu waache kufanya vitu fulani au waanze kufanya vitu fulani ili kuondokana na tatizo husika.

Hatua ya nne ni kupima usahihi wa suluhisho ulilochagua.
Kwa haraka unaweza kuwa umepata suluhisho la tatizo, lakini kabla hujalifanyia kazi unapaswa kujiuliza kama kwa kufanya hicho ulichopanga kufanya utapata matokeo unayotaka kufanya.
Kama jibu ni ndiyo basi unaendelea kufanya.
Kama jibu ni hapana unajiuliza kwa nini, kisha kuja na mapendekezo mengine.
Utaendelea kujiuliza swali hilo kwa kila pendekezo mpaka upate lile ambalo ni sahihi kabisa, linalokupa matokeo unayotaka kupata.

Hatua ya tano ni kufanyia kazi suluhisho ulilopata.
Katika kufanyia kazi unayapima matokeo na kulinganisha na matarajio.
Kama matokeo yanaendana na matarajio basi umeweza kulitatua tatizo.
Kama matokeo yanatofautiana na matarajio bado una tatizo.
Na kama bado una tatizo, rudi kwenye hatua ya kwanza na rudia mchakato mzima.

Kwa kufuata natua hizi nne kwa uhakika, utaweza kutatua kila tatizo ulilonalo.
Na kama kwa hatua hizi nne unashindwa kutatua tatizo lolote lile basi huenda hujalijua tatizo au ulilonalo siyo tatizo bali hali unayopaswa kuishi nayo.

Kama unataka kufanikiwa kwenye maisha, hupaswi kuyakimbia matatizo, bali unapaswa kuyakabili.
Yakabili matatizo uliyonayo na utakuwa imara na kuweza kufikia malengo makubwa uliyonayo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe