2988; Una machaguo matatu.

Rafiki yangu mpendwa,
Inapokuja kwenye kuajiri kwenye biashara, una machaguo matatu.

Chaguo la kwanza ni kutafuta wafanyakazi ambao tayari ni bora kabisa kisha kuwaajiri hao na wakakupa matokeo makubwa na mazuri sana.
Changamoto ya chaguo hili ni uhaba na gharama, wafanyakazi walio bora ni adimu sana kupatikana na hata wakipatikana huwa wanataka kulipwa mshahara mkubwa, kitu ambacho kitaongeza sana gharama za biashara.
Hili siyo chaguo sahihi kwa biashara ambazo ndiyo zinakua.

Chaguo la pili ni kuajiri watu ambao wana uwezo wa kuwa bora ndani yao, kisha kuwaendeleza ili kuweza kufikia ubora wa hali ya juu na kuzalisha matokeo bora.
Changamoto ya chaguo hili ni kuweza kuwajua wenye uwezo wa kuwa bora na kuwa na uvumilivu wakati wa kuwafanya kuwa bora.
Watu wenye uwezo wa kuwa bora ndani yao ni wale ambao ni wanyenyekevu, wapo tayari kujifunza, ni waaminifu, wachapa kazi na wenye ung’ang’anizi.
Ili chaguo hili lifanye kazi vizuri, lazima  uwe na mfumo bora wa kutoa mafunzo endelevu kwa wafanyakazi wako.
Ni lazima uwekeze muda kwenye kuwajenga watu kuwa bora.

Chaguo la tatu ni sala.
Kwenye chaguo hili unaajiri yeyote anayepatikana kwa urahisi, ambaye hana cha kufanya, halafu unasali kwamba unatumaini watu hao watafanya kazi nzuri.
Kwenye chaguo hili unakuwa huchagui walio bora kwa sababu huwezu kumudu na wala huwaendelezi kuwa bora kwa sababu huna mpango wowote wa mafunzo.
Unachukua yeyote rahisi kupatikana na kwenda naye hivyo hivyo bila kufanya mafunzo yoyote.
Matokeo ya chaguo hili huwa ni kuwa na wafanyakazi wasiojiweza, wasiozalisha matokeo na ambao pia hawakai kwa muda mrefu.

Swali ni je wewe umekuwa unatumia chaguo gani kati ya hayo matatu?
Kwa walio wengi, hasa biashara ndogo na za kati, chagua namba tatu ndiyo linatumika sana.
Na hilo ndiyo chanzo cha matatizo na changamoto zote za wafanyakazi kwenye biashara.
Wafanyabiashara wanakuwa hawapo tayari kuwekeza fedha kupata wafanyakazi walio bora au kuwekeza muda kutengeneza walio bora kwa kuwa na mpango wa mafunzo endelevu.
Matokeo yake ni kujikuta wanabaki na wafanyakazi wasiojiweza kwa lolote na wanaokuwa mzigo mkubwa kwa biashara na kuizuia isikue.

Wewe chagua namba mbili, ajiri watu wenye uwezo wa kuwa bora kwa sifa za tofauti walizonazo, kisha wekeza gharama na muda kuyatengeneza kuwa bora kwa mafunzo endelevu utakayokuwa unawapatia.

Kama unataka biashara yako iwe bora, lazima uwe na watu ambao ni bora pia.
Kama huwezi kumudu kuwaajiri ambao tayari ni bora, huna budi kuajiri wenye uwezo wa kuwa bora na kuwatengeneza kuwa bora.
Kamwe usitumie mkakati wa sala na matumaini.
Vitu huwa haviwi vizuri vyenyewe, bali vinatengenezwa kuwa vigumu.

Kama umeajiri ndugu yako ambaye hana kazi ya kufanya halafu huna mpango wowote wa mafunzo kwake, unajua nini biashara yako inakwenda kupata, majanga makubwa.
Mara nyingi changamoto za biashara kuwa ngumu na timu kutokuzalisha vizuri ni za kujitakia kulingana na chaguo tulilofanya.
Kwa vyovyote vile, chaguo namba tatu halifai kwa yeyote makini anayetaka kujenga biashara yenye mafanikio.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe