2991; Tutashinda.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye hii safari ya ubilionea, ni lazima tupate ushindi.
Na hilo litawezekana kama tu tutaufanya mchakato wa safari hii kuwa kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yetu.
Safari yenyewe siyo rahisi, lakini kwa kuifanya kuwa kipaumbele cha kwanza, tunajiweka kwenye nafasi ya kushinda.

Kuna mambo mengi yanayotaka muda, nguvu na umakini wetu. Mengi yataonekana kuwa muhimu sana.
Kama tutayapa mambo hayo kipaumbele kuliko mchakato wetu, tayari tunakuwa tumekubali kushindwa.

Tunajipa uhakika wa kushinda kwa sababu tunatimiza vigezo vikubwa vitatu kwenye huu mchakato.

Kwanza kabisa tumejitoa moja kwa moja kwenye huu mchakato. Ndiyo kipaumbele namba moja kwetu na hatutauacha hata iweje. Hata tukutane na magumu kiasi gani, hatutaacha huu mchakato kwa sababu tumejitoa kweli kweli, hatuna mbadala mwingine.
Hebu fikiria, utakosaje ushindi kama huna mbadala? Ni lazima ushinde au ufe ukiwa unapambana, kitu ambacho ni ushindi pia.

Mbili ni kuupenda kweli mchakato, kutoka ndani ya mioyo yetu.
Hatukai kwenye huu mchakato ili kuonekana, wala hatukai kwa kuigiza na kufuata mkumbo.
Bali tunakaa kwenye huu mchakato kwa sababu tunaupenda kweli kweli.
Ndiyo kitu pekee ambacho tupo tayari kuendelea kukifanya kwenye maisha yetu, bila kujali matokeo au tumefika ngazi gani.
Ushindi kwetu ni matokeo tu, lakini mchakato ni sehemu ya maisha yetu, ambapo tutaendelea nao kwa maisha yote, iwe tumeshinda au la.
Mchakato kwetu ni kama pumzi, ndiyo maana tunajiambia ushindi ni lazima.
Hakuna siku unasema umechoka kupumua na hivyo upumzimke.
Kama unatama kupumzika kwenye mchakato, umeshajiondoa kwenye ushindi.

Tatu ni uaminifu, hatufanyi tu kwa ajili yetu, bali tunafanya kutimiza ahadi yetu kwa wale tunaoambatana nao.
Tumekubaliana kusafiri pamoja kwenye hii safari, tunashirikiana kwa mambo mbalimbali, watu wamejitoa kwa ajili yetu, hivyo ni wajibu wetu pia kujitoa kwa ajili yao.
Hata pale unapoona wewe binafsi hutaki tena kukaa kwenye mchakato, hebu kuwa mwaminifu kwa wale waliokuamini na kukushirikisha mengi muhimu, hebu fanya kwa ajili yao.
Kwenye safari yetu tuna Kocha na pia tuna klabu zetu. Hata pale unapoona hutaki tena kufanya, hebu fanya kwa ajili ya Kocha na Klabu, hebu kumbuka jinsi watu hao wamewahi kujitoa kwa ajili yako na hebu tamani usiwaangushe.
Kwa kuwa mwaminifu kwa wale unaoambatana nao, unalazimika kufanya hata kama hutaki na hilo ndiyo linalokupa uhakika wa ushindi.

Kunaweza kuwa na sababu mbalimbali zinazotaka kukusababisha usikae kwenye mchakato, kama utazingatia hayo matatu, hutaipa sababu yoyote nguvu ya kukuzuia.
Na kama kuna sababu yoyote ile itakayoweza kukutoa kwenye mchakato, basi mchakato siyo kipaumbele cha kwanza kwako na hutaweza kupata ushindi.

Kukaa mguu mmoja nje na mguu mwingine ndani, kusikilizia kama kuna dalili za ushindi au la haitakusaidia. Utashindwa vibaya sana na utakuwa umepoteza muda, nguvu, umakini na maisha yako.
Ushindi unakutaka ujitoe mzima mzima, hata kama wakati mwingine hutaki, inakulazimu kufanya kwa ajili ya wengine, lakini mwisho wa siku unanufaika sana wewe.

Na kama kuna kitu kingine unachokipenda zaidi ya mchakato, kama unajiambia ukishashinda hutaendelea tena na mchakato, hutashinda. Yaani hilo lifakuwa kikwazo kikubwa mno kwako kupata ushindi unaoutaka.
Kama unauona mchakato mzima ni mateso, umeshashindwa kabla hata ya kuanza.
Kama unatafuta njia ya kuutoroka mchakato, umeshashindwa vibaya sana.

Kuna wengi wanajikuta kwenye huu mchakato kwa kufuata mkumbo, wakiwa hawajui ni kwa kiasi gani wanahitajika kujitoa kukaa kwenye huo mchakato.

Ushindi utakuwa ni wa uhakika kabisa kwako kama mchakato utakuwa kipaumbele cha kwanza kabisa kwako, utaupenda sana mchakato kutoka ndani yako na hata kama hujisikii kuendelea kukaa kwenye mchakato, unafanya kwa heshima ya wengine ulioambatana nao au kuwaahidi.
Nje ya nayo usijidanganye kwamba utaweza kupata ushindi.

Andika kwenye maoni hapo chini kwa nini wewe una uhakika kwamba utashinda.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe