2993; Ukiondoka, siyo kwa sababu hizi mbili.

Rafiki yangu mpendwa,
Tangu nimeanza huduma hii ya ukocha, kuna watu wengi sana ambao wameshapita na kuondoka.
Wapo ambao niliwaondoa mimi mwenyewe na wapo ambao waliondoka wao wenyewe.

Niliowaondoa sababu kuu ni moja tu, kushindwa kukaa kwenye mchakato ambao tumekubaliana, licha ya kuelekezwa kwa kila namna. Pamoja na kupewa kila fursa ya kujirekebisha, bado walishindwa kufanya hivyo.

Kwa walioondoka wao wenyewe wana sababu zao binafsi, wapo walioahidi wanakaa pembeni kwa muda halafu watarudi na wengine walieleza wametosheka na yale waliyojifunza. Na pia wapo walioeleza hawataki tena kujitesa na mchakato tulionao.

Katika hii safari ya mafanikio makubwa tuliyonayo, mabadiliko ya watu yataendelea.
Wapo ambao nitaendelea kuwaondoa na sababu pekee ya kuwaondoa itaendelea kuwa kutokukaa kwenye mchakato kamili wa safari hii.

Halafu wapo wale watakaoamua kuondoka wenyewe, kwa sababu zao mbalimbali.
Kuna sababu nyingi za watu kuondoka ambazo siwezi kuzizuia, lakini kitu kimoja ambacho nimejiwekea ni hakuna atakayeondoka kwa sababu kubwa mbili.

Sababu ya kwanza ni kunishinda kwenye ufanyaji wa kazi. Moja ya sababu zinazoweza kuwafanya watu kuachana na kocha wao ni pale wanapomzidi kwenye ufanyaji wa kazi, yaani wanakuwa wanafanya kazi kuliko kocha wao.
Hilo sitaliruhusu kwangu, nitahakikisha kila wakati ninafanya kazi kuliko wote ambao wapo kwenye huduma yangu.
Yaani hata ujisukume kufanya kazi kwa juhudi kiasi gani, bado nitahakikisha ukiniangalia unaona bado hujanifikia kwenye ufanyaji wa kazi.
Ahadi niliyojiwekea ni mara zote nitaweka juhudi kubwa kwenye kazi kuliko wengine wote.
Na hili siyo tu kushindana nani anaweza kufanya kazi sana, bali kuhakikisha kila unaponiangalia unaona bado hujafanya vya kutosha.
Hilo litakusukuma ufanye zaidi na zaidi na hivyo uone bado hujafika mwisho wa kupiga hatua zaidi.
Ninachojua ni nikizembea kwenye kazi, utaona hakuna tena jipya na hivyo kuwa na sababu ya msingi ya kuondoka.
Hivyo kwenye huu ufanyaji wangu wa kazi bado sijafika mwisho na wala sitafika mwisho, kila mara nitahakikisha nafanya zaidi ya wengine wote.
Kwa kifupi kwa upande wa ufanyaji kazi, bado sijafanya, hivyo kama umekuwa unashangaa nafanyaje yote, bado utahitaji kukaa hapa ushangae zaidi, maana mchezo ndiyo kwanza unaanza.

Sababu ya pili ni kunishinda kwenye kujifunza. Sababu nyingine kubwa inayowafanya watu kuachana na makocha wao ni pale wanapoona hawana tena cha kujifunza kutoka kwa makocha wao.
Hicho ni kitu ambacho kamwe sitakuja kukiruhusu kwangu.
Ahadi nyingine niliyojiwekea ni kuwashinda wengine wote kwenye kujifunza.
Hivyo haijalishi unajifunza kiasi gani, bado nitaendelea kujifunza kuliko wewe.
Haijalishi unajua kiasi gani, bado ukija kwangu nitahakikisha una vitu vya kujifunza.
Pamoja na mengi ambayo nimeshajifunza, bado nitaendelea kujifunza zaidi na zaidi.
Kama umekuwa unashangaa najifunzaje yote hayo, bado hujaona kitu, nitahakikisha kila ukija kwangu kuna kitu unajifunza.
Nitaendelea kuhakikisha hata kama ni maongezi ya kawaida tu tunafanya, unaondoka na mambo ya maana ya kwenda kufanyia kazi na ukanufaika.
Kwa namna hiyo, utaendelea kuwa hapa kama bado unataka kujifunza na kuwa bora.

Sikuelezi haya kukushawishi ubaki au kukuzuia usiondoke.
Nayaeleza haya hapa kwa sababu kubwa mbili.
Moja ni kuweka kumbukumbu sawa, ili kila mmoja aelewe yupo hapa kwa sababu gani. Na kubwa ni hizo mbili, kujifunza na kuchukua hatua, yaani kuweka kazi hasa.
Mbili ni kuendelea kukupa msukumo wa kujifunza na kuweka kazi, kwa kukuhakikishia kwamba kama tayari unao msukumo wa ndani, basi umepata mahali sahihi wa kujipima.

Siku moja nilikuwa na maongezi na mkurugenzi mkuu wa kampuni moja kubwa yenye matawi kwenye nchi zaidi ya 8, Afrika na Uarabuni.
Katika mazungumzo yetu, sijui tulifikaje kwenye ufanyaji wa kazi, nikamwambia kwa kujivunia kwamba mimi siku yangu huwa inaanza saa tisa usiku kila siku. Nikamuuliza wewe umeanza siku yako saa ngapi? Akanijibu sijalala kabisa. Ah, kwa kweli nilipata msukumo mkubwa zaidi.
Japo sitakuwa na kesha kwa muda mrefu kama yeye, lakini nitahakikisha kwenye kila muda ninaoweka kwenye kazi, naweka kazi ya maana hasa.

Kwenye eneo la kujifunza, huwa naona najifunza kwa kasi kubwa. Kwa usomaji wa vitabu kwa muda mrefu nilikuwa nasoma vitabu 2 kwa wiki, baadaye nikaona wengi ninaojifunza kwao wanasoma kitabu kimoja kwa siku. Nimefika kwenye kusoma kitabu kimoja kwa siku, nimekutana na mtu mwingine ninayependa kujifunza zaidi kwake, ambaye anaitwa Tyler Cowen, ambaye anasoma zaidi ya vitabu vitano kwa siku.
Kadhalika kwenye usikilizaji wa vitabu, nimekuwa msikilizaji wa vitabu vilivyosomwa (Audio Books) kwa miaka mingi. Na kipindi chote nimekuwa nasikiliza kwa kasi ya kawaida. Nikaona kuna watu wanasikiliza kwa kasi mara mbili, nikaanza kufanya hivyo, japo mwanzo ilinitaka niongeze zaidi umakini.
Nilichokuja kushangaa ni kuna watu wanasikiliza vitabu kwa kasi mara 3 zaidi ya kawaida. Kwa kweli hilo lilinivutia sana, nikaona kumbe hata kama naona nafanya kwa juu kiasi gani, kuna ambao wanafanya kwa juu zaidi.

Ahadi yangu kwenye maisha imekuwa hii, nitawaruhusu watu wanizidi kwenye kila kitu isipokuwa vitu viwili; kazi na kujifunza.
Mara zote nitahakikisha nafanya kazi kuliko wengine wote na pia ninajifunza kuliko wengine.
Na ndiyo maana muda wangu wote ambao sijalala (ambao ni masaa 18 kwa siku), nakuwa nafanya kazi au najifunza, hakuna kingine nje ya hapo.

Na ushauri wangu mkubwa kwako ni waruhusu watu wakuzidi kwenye mambo mengine yote isipokuwa hayo mawili; kazi na kujifunza. Fanya kazi kwa juhudi kubwa kuliko wote na pia jifunze zaidi ya wengine wote.
Hilo lianzie kwenye timu yako na kwenda kwa washindani wako.
Litakupa fursa ya kufika kwenye mafanikio makubwa na kudumu hapo kwa muda mrefu.

Nimalizie kwa kukukumbusha kwamba haijalishi utafanya kazi kwa juhudi kiasi gani na kujifunza kwa wingi kiasi gani, kila mara utaniona niko mbele yako.
Na pale utakapokuwa mbele yangu kwenye hayo mawili, itabidi majukumu yabadilike na mimi ndiye nije kujifunza kutoka kwako.
Itabidi ujiue ili hilo litokee, nakuahidi hivyo.

Tuendelee na mapambano, mambo bado kabisa.
Na hii izidi kuchochea moto ndani yako, utakaokufanya ufanye zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe