2995; Ongoza.

Rafiki yangu mpendwa,
Viongozi huwa wana kazi kuu moja, ambayo ni kuongoza.
Na ili kuongoza vyema, huwa wanaondoa kila aina ya mashaka wanayokuwa nayo.
Wanajitoa kweli kweli kwenye kile ambacho wanakifanya.

Viongozi bora misimamo yao huwa inajulikana wazi.
Kama wapo ndani basi wapo ndani moja kwa moja.
Hawawi mguu mmoja ndani na nguu mwingine nje.
Wanaweza kufanya makosa mbalimbali kupitia maamuzi wanayofanya, lakini hayo hayawaondoi kwenye kujitoa hasa kufikia kile wanachotaka.

Viongozi bora wanajua ili waaminike na watu, wanapaswa kuamini sana kile wanachosimamia.
Wanajua watu hawataki sana kuamini anachoamini kiongozi, bali wanatama kiongozi awe anaamini kweli kile anachoamini.
Ni imani yake isiyoyumbishwa ndiyo inawavutia watu kuja kwake na kuwafanya waendelee kuwa naye.

Wewe ni kiongozi kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yako.
Lakini eneo kuu ni biashara.
Mafanikio ya biashara yako yanategemea sana uongozi wako.
Usipokuwa kiongozi imara, huwezi kujenga timu imara na biashara yenye mafanikio.

Kila unapoona biashara inayoshindwa kukua, jua wazi kilichokosekana ni uongozi imara.
Biashara inaweza kuwa na wazo zuri na ikawa na wateja wenye uhitaji, lakini bila ya uongozi imara, haiwezi kukua.
Changamoto nyingi zinazotokana na ukuaji wa biashara huwa zinaanzia kwenye kukosekana kwa uongozi imara.

Kushindwa kujenga mfumo imara wa kuiendesha biashara ni kukosekana kwa uongozi mzuri.
Uongozi mzuri huwa na maono makubwa yanayomsukuma mtu kuweka mfumo wa kuhakikisha maono hayo yanaendelea hata kama hayupo.

Kushindwa kujenga timu imara ya kuendesha biashara ni kukosekana kwa uongozi mzuri.
Uongozi mzuri huwa unawaweka watu sahihi kwenye mfumo wa biashara na kuhakikisha wanafanya kile wanachopaswa kufanya.
Uongozi mbovu huwaacha watu wajiendee vile wanavyotaka wao wenyewe.
Hilo hupelekea watu wengi wazuri kupotea, kwa kukosa uongozi.

Na pia kushindwa kujenga wateja waaminifu kwenye biashara, ambao wanasababisha mauzo makubwa ni kukosekana kwa uongozi mzuri.
Wateja wanakaa pale ambapo wanathaminiwa na wanaona mwanga mkubwa mbele.

Kama unataka kujenga biashara yenye mafanikio makubwa, neno ni moja tu; ONGOZA.
Kila unapokwama na kukutana na changamoto jiulize ni wapi umeshindwa kuongoza vizuri.
Utaona na kuweza kuchukua hatua sahihi.

Uongozi bora siyo kuwafanya watu wajisikie vizuri kwa kuwaambia wanachotaka kusikia na kuwaacha wafanye wanachotaka kufanya.
Uongozi bora ni kuwafanya watu wafanikiwe kwa kuwaambia wanachopaswa kusikia na kuwafanya wafanye wasichotaka kufanya, lakini ni muhimu kwao.

Kuwa kiongozi bora kwa kuongoza.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe