2999; Mlango wa kutokea.

Rafiki yangu mpendwa,
Kazi ya kujenga timu ambayo ndiyo kipaumbele chetu kikubwa kwa sasa siyo kazi rahisi.
Ina changamoto za kila aina.
Kuna makosa madogo madogo ambayo ukiyafanya yanakuwa kikwazo kikubwa kwako kujenga timu bora.

Ili kuepuka makosa hayo kwenye kujenga timu, ni muhimu kuwa na hatua unazozifuata kwenye zoezi zima.
Zipo hatua tano muhimu za kufuata kwenye zoezi la kujenga timu ili kupunguza changamoto mbalimbali zinazojitokeza.

Hatua ya kwanza ni kuajiri kwa mchakato sahihi.
Hapa unapaswa kutangaza nafasi za kazi, kuwataka watu watume maombi na kuwafanyia usaili.
Kosa kubwa ambalo watu hufanya kwenye hatua hii ni kuajiri watu wa karibu wanaowajua, tena kwa kigezo kwamba hawana cha kufanya. Mwishowe wanakuja kupata matokeo mabaya, kwa sababu hao wasiokuwa na cha kufanya, hushindwa kufanya wanachopaswa kufanya.

Hatua ya pili ni kuwapa majukumu ya kazi wale ambao wameshinda kwenye usaili.
Hapa unapaswa kuwaambia kwa hakika nini wanapaswa kufanya na wanapimwaje kwenye ufanyaji.
Kila unayemwajiri ayaelewe majukumu yake vizuri na jinsi ya kuyatekeleza.

Hatua ya tatu ni kuwapa mafunzo ya kutekeleza majukumu yao.
Pamoja na kuwapa majukumu, bado kuna ambao yatakuwa magumu kwao kutekeleza.
Hivyo unapaswa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wako ya jinsi ya kutekeleza majukumu yao kwa viwango vya juu.

Hatua ya nne ni kupima matokeo ya yale wanayofanya na kuwasaidia namna ya kuboresha ili kupata matokeo bora zaidi.
Wapo wafanyakazi ambao pamoja na kuchukua hatua, bado matokeo watakayopata yanakuwa siyo mazuri.
Kwa kuwa wewe tayari una uzoefu kwenye biashara yako, wasaidie kwa kuwaelekeza namna ya kuboresha ufanyaji wao.
Hapa unaenda hatua ya ziada ya kuhakikisha huwapotezi watu ambao wanaweza kuwa bora.

Hatua ya tano ni kuwaonyesha mlango wa kutokea.
Kama utafuata hatua zote nne hapo juu, lakini bado mfanyakazi akashindwa kufanya kile anachopaswa kufanya, kuna hatua moja tu ya kuchukua, ambayo ni kumwonyesha mlango wa kutokea, yaani kumfukuza kazi.
Hii ndiyo hatua ngumu kabisa na ambayo wengi huikwepa.
Mwishowe wanabaki na watu wengi kwenye biashara, ambao hawana uzalishaji wala ufanisi wowote.
Watu hao wanaishia kuwa mzigo kwenye biashara, kitu kinachoigharimu sana biashara.

Kama umemwajiri mfanyakazi kwa mchakato sahihi.
Ukamweleza kwa kina majukumu anayopaswa kutekeleza.
Ukampa mafunzo ya namna ya kutekeleza majukumu yao.
Ukamfuatilia kwenye utendaji na kumsaidia kuboresha zaidi.
Lakini bado akawa anashindwa kutekeleza majukumu yake.
Hatua sahihi ni kumwondoa mfanyakazi huyo kwenye biashara.

Huwa kuna hali ya kuamua kuwaacha wafanyakazi wa aina hiyo kwa kuamini huenda watabadilika.
Lakini hicho huwa hakitokei, kadiri wanavyoendelea kubaki ndivyo wanavyofanya uharibifu mkubwa kwenye kazi na hata kwa wengine pia.

Inakuwa vigumu kuchukua hatua ya kuwaondoa wafanyakazi wasiofaa kama hukutumia mchakato sahihi kwenye kuwaajiri.
Kama uliajiri watu wa karibu ambao hawana cha kufanya, itakuwa vigumu kuwaondoa kwa sababu hawatakuwa na cha kwenda kufanya.
Utawaonea huruma wataenda wapi, lakini huruma haitakuwa na manufaa kibiashara.

Upo kwenye biashara kufikia maono makubwa uliyonayo.
Kila aliyepo kwenye biashara hiyo anapaswa kuwa na mchango kwenye kuyafikia hayo maono.
Ambaye hana mchango anapaswa kuonyeshwa mlango wa kutokea ili asiwe kikwazo cha kufikiwa kwa maono yaliyopo.

Kuwaondoa watu wasiofaa kwenye biashara, siyo tu manufaa kwa biashara husika, bali pia ni manufaa kwa watu wenyewe.
Hakuna kitu kinawaumiza na kuwadumaza watu kama kuwa kwenye kazi ambayo hawawezi kuifanya vizuri.
Wakati mwingine inakuwa ni kazi isiyoendana na vipaji vyao au uwezo walio nao.
Kwa kuendelea kukaa kwenye biashara hiyo wanakuwa wanapoteza muda, kwa sababu hakuna hatua zozote wanazopiga.
Kuwaondoa inawasaidia kwenda kufanya kile kilicho sahihi kwao.

Zoezi la kujenga timu ni mchakato endelevu ambapo kama hatua hizo muhimu zifafuatwa, tutaweza kujenga timu imara.
Ni zoezi linalohitaji muda na uvumilivu kwa sababu utawapitia wengi wasio sahihi kabla hujawafikia wachache sahihi.

Kadiri unavyokwenda na huo mchakato unajifunza baadhi ya tabia zinazokuwepo kwa wale wanaokuja kufanya vizuri.
Moja ya tabia hizo ni kuwa na msukumo wa ndani wa kufaka kufanikiwa, hivyo kuwa tayari kujisukuma zaidi kwenye kazi.

Kwenye biashara, ukiwa na timu sahihi una uhakika wa kufanya makubwa sana.
Weka juhudi kubwa kwenye kujenga timu sahihi na matokeo yatakwenda kuwa mazuri sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe