3003; Piga makofi tafadhali.

Rafiki yangu mpendwa,
Wengi wetu tumelelewa kwenye mazingira ambayo hatujafundishwa kutambua, kuthamini na kusifia juhudi na hatua wanazopiga wengine.

Pale tunapoona kuna wengine wamefanikiwa kuliko sisi kwenye jambo lolote lile, tunatafuta sababu ya kubeza uwezo ambao mtu ametumia kupata alichopata.

Na hapo ndipo chuki zote dhidi ya watu waliofanikiwa zinapoanzia.
Watu hutafuta kila namna ya kujifariji kwamba kutokufanikiwa kwao hakutokani na uzembe na uvivu wao, bali mambo ya nje.
Inapoonekana kuna wengine kwenye hali kama zao wamefanikiwa, wanatafuta cha kuonyesha kwa watu hao ambacho siyo sawa.

Utasikia mabaya mengi ya wale waliofanikiwa yakisemwa na wasiofanikiwa.
Sehemu kubwa ya mabaya yanayosemwa huwa hata siyo ya kweli au sahihi.
Yanakuwa ni sehemu tu ya wale walioshindwa kujifariji.

Ukweli ni kwamba, kama kuna mtu amepiga hatua ambazo wewe hujapiga, unapaswa kuwa mnyenyekevu na kujifunza kutoka kwa watu hao.
Unapaswa kuweka pembeni yote yanayosemwa kuhusu watu hao na wewe kuwa na mtazamo chanya wa kujifunza na kuchukua hatua.

Unapokutana na mtu ambaye amefanikiwa kuliko wewe kwenye jambo lolote, unapaswa kupiga makofi na kufurahia kwamba unapata fursa ya kwenda kujifunza vitu ambavyo hukuwa unavijua hapo awali.
Na kama tayari ulikuwa unavijua, bado hujavifanyia kazi kwa uhakika.
Hivyo kukutana na aliyefanyia kazi, inakuwa fursa kubwa na nzuri kwako kujifunza.

Umekutana na mtu ambaye ana utajiri mkubwa kuliko wewe, simama na upige makofi. Kisha jiulize amewezaje kupata utajiri huo?
Achana na hadithi za kwenye jamii kwamba amerithi utajiri, au ametumia njia zisizo halali.
Hata kama kweli hayo yapo, mbona kuna wengine wengi ambao wamepitia hali kama hizo na hawajawa na utajiri?
Lazima ufike mahali ukubali kwamba kuna uwezo wa tofauti ambao mtu anakuwa nao na kuutumia katika kupata matokeo bora.

Umekutana na mtu ambaye amejenga biashara inayojiendesha vizuri na kwa faida, simama na upige makofi. Kisha jiulize amewezaje kupiga hatua hizo.
Kutakuwa na hadithi nyingi kuhusu mtu huyo, kwamba alipata bahati fulani au kuna njia zisizo sahihi ambazo ametumia.
Hata kama hayo yana ukweli fulani, turudi kwenye msingi, kwamba wapo wengi ambao wamepitia hali kama hizo lakini hawajaweza kupiga hatua za aina hiyo.
Hivyo kuna mengi ya kujifunza kwa yeyote aliyepiga hatua kubwa.

Mwisho simama na ujipigie makofi wewe mwenyewe.
Kuna hatua ambazo umeshaweza kupiga mpaka sasa, hatua ambazo wapo wengine wengi waliozishindwa.
Lakini pia kuna magumu na changamoto mbalimbali ambazo umeshapitia, lakini hujakubali ziwe kikwazo kwako kuendelea kuyapambania mafanikio yako.

Kwa hatua hizo ambazo umeshapiga, ni ushahidi dhahiri kwamba utazidi kupata mafanikio makubwa kama utaendelea kukaa kwenye mchakato.

Mafanikio ya aina yoyote ile ni magumu.
Unapokutana na yeyote aliyepiga hatua za mafanikio, kubali, thamini na sifia hatua hizo.
Kisha kuwa mnyenyekevu na jifunze kwa mtu huyo na ukachukue hatua kwa yale unayojifunza.
Kwa kufanya hivyo utaweza kuona fursa zaidi na namna ya kuzitumia kupiga hatua kubwa zaidi.

Je ni jambo gani kwako binafsi unalojikubali na kujisifia kwa hatua ulizopiga kwenye hii safari ya mafanikio?
Tushirikishe kwenye maoni hapo chini ili tuweze kukupigia makofi na kujifunza zaidi kutoka kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe