3004; Malengo na sababu.

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa tunachukulia wanaoshindwa kwenye maisha kama watu ambao hawana malengo yoyote.
Na wanaofanikiwa kwenye maisha tunaona ndiyo wenye malengo.

Kwa kifupi tunachodhani ni tofauti ya wanaoshindwa na wanaofanikiwa ni malengo.
Lakini huo siyo ukweli, karibu kila mtu ana malengo fulani.
Malengo hayo yanaweza kuwa madogo au makubwa, lakini yanakuwepo.

Ukweli ni kwamba, kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa siyo malengo bali ni sababu.
Wanaofanikiwa ni wale wanaokuwa na sababu kubwa na nyingi za kufanya kile wanachopaswa kufanya.
Ni sababu hizo ndiyo zinazowawezesha kuendelea na safari hata pale wanapokutana na magumu au changamoto mbalimbali.

Japokuwa watu wote wanakuwa na malengo, msukumo wa kufikia malengo hayo haufanani kwa watu wote, hata waliopo kwenye eneo moja na wanafanya kitu kimoja.

Sababu za kwa nini mtu afanye kitu zina maana na mchango mkubwa kwa watu kuweza kuyafikia malengo yao.

Nietzche aliwahi kunukuliwa akisema; mtu mwenye kwa nini kubwa kwa kile anachotaka anaweza kukabiliana na changamoto yoyote anayokutana nayo.
Ni zile sababu za msingi ulizonazo ndizo zinazokusukuma kufikia malengo yako.

Sababu pia zinakupa nguvu ya kuweza kuyapambania malengo uliyonayo.
Nikikuambia ubebe mfuko wa sementi wenye kilo 50 na ukimbie nao kwa umbali fulani utaona hilo ni zoezi gumu na usiloweza.
Lakini ikitokea mtu wa karibu yako, mwenye kilo 50 anaumwa na anatakiwa kuwahishwa mahali kwa haraka, utakuwa tayari kumbeba na kukimbia naye.
Hapa tunaona jinsi ambavyo sababu inakupa nguvu za kuweza kuvuka magumu yote.

Watu wanaoweka malengo na kushindwa kuyafanyia kazi, siyo kwa sababu malengo hayo siyo sahihi, ila ni kwa sababu wanakosa sababu za kuwasukuma.
Chukua mfano wa zoezi la kuwapigia simu wateja. Watu wengi huwa wanaleta visingizio mbalimbali kwa nini zoezi hilo haliwezekani.
Lakini kama kuna kitu wanakipata moja kwa moja kwa kuchukua hatua, wanapata msukumo wa kuchukua hatua.

Zipi sababu zako wewe kufikia malengo yako?
Kama ambavyo tumeona, malengo kila mtu anayo. Ila sababu za kufikia malengo hayo ndiyo zinatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
Swali ni je wewe ni sababu gani zinazokusukuma kwenye malengo yako makubwa?
Nini kinakufanya uwe tayarj kuteseka katika kuyafikia malengo yako?
Shirikisha kwenye sehemu ya maoni hapo chini.

Watu wanaweza kufundishwa na kusaidiwa jinsi ya kuweka malengo yoyote makubwa waliyonayo.
Lakini hakuna mtu anaweza kupewa sababu za kwa nini afikie malengo fulani.
Sababu huwa zinaanzia ndani ya mtu mwenyewe.
Na kama ndani hakuna sababu za msingi kwa mtu kupambania malengo yake, hakuna namna ataweza kuyafikia.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe