3005; Wewe na biashara.

Rafiki yangu mpendwa,
Changamoto nyingi ambazo watu wanakutana nazo kwenye biashara, chanzo chake ni watu kushindwa kujitofautisha na biashara zao.
Kwa sababu wanamiliki biashara, basi wanadhani biashara hizo ni wao na hivyo kufanya chochote wanachojisikia kwenye biashara hizo.

Hizo fikra kwamba wao ndiyo biashara na wanaweza kufanya chochote wanachotaka zimekuwa kikwazo kikubwa sana kwa watu kufanikiwa kwenye biashara.
Kwani watu hufanya maamuzi kwa tamaa zao wenyewe, ambayo huwa na madhara makubwa kwenye biashara.

Eneo ambalo biashara zimekuwa zinaathirika sana ni eneo la fedha.
Wamiliki wa biashara hudhani kwa kuwa biashara ni zao, basi fedha zote zilizopo kwenye biashara ni zao pia na wanaweza kuzitumia watakavyo.
Hapo ndipo matatizo makubwa huanzia na kupelekea biashara kushindwa vibaya sana.

Wewe na biashara yako ni viumbe wawili tofauti kabisa.
Hata serikali, kisheria inatambua biashara kama kitu kinachojitegemea.
Kudhani wewe na biashara yako ni kitu kimoja ni kuibemenda, kuidumaza ishindwe kukua.

Uhusiano wako na biashara ni huu; wewe umeikopesha biashara mtaji na biashara inakulipa mtaji huo kwa faida inayotengenezwa.
Hiyo ina maana kwamba, fedha pekee unayoweza kuitoa kwenye biashara ni faida.
Na hapo ni kama unaweza kukokotoa faida kwa uhakika.
Tofauti na hapo, kama unatoa fedha kwenye biashara kiholela, jua tu hiyo biashara itakufa, hakuna namna itaweza kutoboa.

Biashara yoyote ile inayoendeshwa kwa misingi sahihi, ambayo inauza kitu chenye uhitaji kwa watu, ina nafasi kubwa ya kufanikiwa kama itafanywa kwa umakini, kama taratibu zote za kuendesha biashara zitafuatwa.

Maeneo muhimu ya kuzingatia ili biashara iweze kufanikiwa ni kuzijua namba za biashara na kuzisimamia kwa uhakika. Kuwa na mfuno bora wa kuiendesha biashara. Kujenga timu imara ya kuendesha biashara na kufanya mauzo makubwa.

Fedha ya kwenye biashara inapaswa kuheshimiwa sana na kila mtu, haipaswi kuchukuliwa kiholela, hata na mmiliki wa biashara.
Muda na juhudi za kazi zinapaswa kuwekwa na kila anayehusika kwenye biashara. Watu hawapaswi kufanya vitu vile wanavyojisikia wenyewe.

Unajua kwa nini watu wanaotoka kwenye ajira na kwenda kuanza biashara zao wenyewe huwa wanashindwa sana kibiashara?
Kwa sababu wanashindwa kuhamisha nidhamu ya kwenye ajira kupeleka kwenye biashara.
Wakati kwenye ajira walikuwa wanawahi kazini kila siku bila kuchelewa wala kukosa, kwenye biashara zao wanafika muda wanaotaka na wakiwa na changamoto kidogo hawaendi kabisa.

Wakati watu wakiwa kwenye ajira na hawana fedha, hawawezi kuchukua fedha ya taasisi vile wanavyojisikia wao wenyewe. Lakini kwenye biashara zao, wakiwa na shida kidogo tu ya fedha, wanachukua kwenye biashara bila kujali.

Vifo vya biashara nyingi vinatokana na uyatima wa biashara.
Yaani biashara inakuwa kama mtoto yatima, ambaye hakuna anayemjali.
Kuanzia mmiliki mwenyewe ambaye anafanya kila kitu jinsi anavyojisikia, mpaka kwa wafanyakazi ambao wanatafuta njia ya kupata zaidi kwa kufanya kidogo.

Kama unamiliki biashara na unatoa fedha kwenye biashara hiyo vile unavyojisikia haitaweza kutoboa.
Kama unamiliki biashara na unafungua na kufunga vile unavyojisikia wewe ni tatizo kubwa.
Kama unamiliki biashara yenye wafanyakazi na unawaacha wafanye vile wanavyojisikia wao, kifo cha biashara hiyo hakiepukiki.
Ili biashara ifanikiwe, inapaswa kuheshimiwa sana na kila aliyepo kwenye biashara hiyo, kuanzia mmiliki, wafanyakazi mpaka wateja.

Biashara ambayo haiheshimiwi itakufa tu.
Serikali zimekuwa na njia za kulazimisha watu waziheshimu biashara ili iweze kukusanya kodi yake, lakini watu wamekuwa na njia za kukwepa hilo.
Wanafanya kwa nia njema ya kupungua gharama za biashara, lakini wanaishia kuziumiza biashara kwa sababu hazina mtetezi.
Wanafanya vile wanavyotaka na kujisikia kitu kinachopelekea biashara hizo kufa.

Kwenye programu yetu ya bilionea mafunzoni, mimi Kocha wako nimechagu kuwa mtetezi wa biashara yako, dhidi yako wewe mwenyewe.
Wajibu wangu ni kuhakikisha hiyo biashara yako inaheshimiwa na kila mtu, kwa kuanza na wewe mwenyewe kisha wote wanaohusika.
Ninakuwa mkali sana kwako wewe na kwa wengine wote ambao wanaihujumu biashara kwa kwenda kinyume na misingi sahihi ya kuiendesha biashara.
Nahakikisha misingi yote inazingatiwa na kila aliyepo kwenye biashara.
Bila hivyo, hakuna biashara itakayotoboa.

Ichukulie biashara yako kama ajira kwenye kampuni kubwa kabisa nchini au hata duniani.
Chukulia wewe umeajiriwa pale kama mkurugenzi mkuu (CEO) na wajibu wako ni kuleta matokeo bora.
Kama huleti matokeo bora, bodi ya wakurugenzi itakufukuza muda wowote.
Kama mwajiriwa wa kampuni kubwa, huwezi kufanya mambo vile unavyojisikia wewe, utafuata misingi na taratibu zilizopo.
Huwezi kuamua lini uende na lini usiende kazini.
Huwezi kujichukulia fedha kwenye biashara vile unavyotaka wewe.
Na huwezi kumwajiri mtoto wa shangazi yako kwa sababu hana kazi ya kufanya.
Sijui unaipata picha hapo?

Hivi ndivyo tunavyokwenda kwenye programu yetu ya Bilionea Mafunzoni;

1. Wewe ndiye mkurugenzi mkuu (CEO) wa biashara yako ambaye umeajiriwa na biashara kwa lengo la kuifikisha kwenye ubilionea.

2. Klabu yako ya Bilionea Mafunzoni ndiyo bodi ya wakurugenzi kwenye biashara yako, ambayo inahakikisha biashara inaendeshwa kwa misingi sahihi na malengo yaliyopo yanafanyiwa kazi.

3. Kocha ndiye mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi kwenye biashara yako, ambaye pamoja na bodi wanayo mamlaka ya kukuwajibisha wewe mkurugenzi mkuu wa biashara kwa yale yanayoendelea.

Huu ni uwajibikaji wa juu kabisa kwenye biashara ambao ukizingatiwa lazima biashara itakuwa na mafanikio makubwa.
Pokea hili kwa mikono miwili na kulifurahia kwa sababu linakuzuia wewe mwenyewe usiwe kikwazo kwa biashara yako.
Na kama unaona ni jambo usiloweza, kwa kuona ni kukubali kuteswa kwa ajili ya biashara yako mwenyewe, basi jua hiyo biashara haina maisha marefu.
Ukiwa na bahati sana utaenda nayo kwa udumavu katika kipindi cha uhai wako.
Lakini baada ya kifo chako, hata kabla ya arobaini yako, shida zitakuwa zimeanza kujitokeza na biashara kukufuata kaburini.

Hicho ni kitu ambacho hatutakiruhusu kwenye programu hii ya Bilionea Mafunzoni.
Tutakuondoa haraka sana kama huwezi kuwa na nidhamu hii ya msingi kabisa inayohitajika ili biashara yako iweze kufanikiwa.

Kuanzia sasa, futa dhana kwamba wewe ni mmiliki wa biashara na unaweza kufanya utakavyo.
Kisha jenga dhana kwamba wewe ni mwajiriwa kwenye biashara kama mkurugenzi mkuu na unapaswa kufuata taratibu zote za kuiendesha biashara hiyo kwa mafanikio makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe