3006; Haifanyiki.

Rafiki yangu mpendwa,
Asili ina kanuni ya visababishi na matokeo.
Kanuni hiyo inasema kwa kila matokeo unayoyaona, kuna visababishi vyake.
Hivyo basi, kama kuna matokeo ulitegemea kuyaona ila hayaonekani, ni kwamba hakuna visababishi.

Waswahili wanasema ukiona vyaelea ujue vimeundwa.
Mambo hayatokei tu kwa bahati au ajali, bali huwa yanasababishwa.

Na hapo ndipo nataka kuzungumza vizuri na wewe, ili uweze kukaa upande sawa.
Umekuwa unajifanganya sana na pia umekuwa unadanganywa na wengine juu ya hatua wanazochukua.

Unajiambia umefanya kila kitu lakini matokeo hayaji kama ulivyotegemea.
Watu unaojihusisha nao wanakuambia wamefanya kila kitu ila hawapati matokeo.
Jibu moja rahisi kabisa ni hili; hujafanya na hawajafanya.
Wala usitake kuumiza kichwa kwamba kwa nini umefanya au wamefanya na matokeo hayaji.
Jua bila ya shaka yoyote kwamba chochote kilichopaswa kufanyika ili kuzalisha matokeo, hakijafanyika.

Matokeo yanazalishwa na hatua ambazo zimechukuliwa.
Ukienda kwenye shamba na kukuta mahindi yamestawi vizuri, huhitaji hata mtu akuambia nini kimetokea.
Unajua kabisa kuna mbegu za mahindi zilipandwa hapo, zikapata maji, mbolea na kupaliliwa vizuri.
Na kama kuna shamba la pembeni ambalo halina mahindi ya aina hiyo, unajua kabisa kwamba kuna vitu havijafanyika. Labda mbegu hazikupandwa, au maji hayakupatikana au mbolea au hayakupaliliwa.

Kama hakuna matokeo, kuna sababu hizi nne;
Moja ni kitu hakijafanyika kabisa.
Mbili ni kitu hakijafanyika kwa wingi.
Tatu ni kitu hakijafanyika kwa usahihi.
Na nne ni kitu hakijafanyika kwa msimamo.
Kitu chochote kikifanyika kwa wingi, usahihi na msimamo, lazima kitazalisha matokeo yanayotegemewa.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye fedha.
Fedha ni matokeo, ili uzipate lazima kuwe na visababishi.
Lazima ufanye mambo ambayo yanavuta fedha kuja kwako.
Na lazima uyafanye kwa wingi, usahihi na msimamo ndiyo matokeo yaweze kuonekana, yaani fedha ziweze kuja kwako.

Changamoto kubwa kwenye maisha na inayowazuia watu wengi wasifanikiwe ni kutaka matokeo bila ya visababishi.
Watu wanahangaika sana kutafuta njia za mkato za kupata kile wanachotaka bila ya kuweka juhudi.
Hakuna kitu kama hicho, asili haina njia za mkato. Lazima uweke visababishi ndiyo upate matokeo. Na siyo tu kuweka mara moja, bali kuweka kwa wingi, usahihi na msimamo.

Tuchukulie mfano kwenye mauzo, watu wamekuwa wanalalamika kwamba wanaweka juhudi sana lakini mauzo hayapatikani.
Kwamba wanapiga simu sana na kukutana na wateja, ila hawakubali kununua.
Mpaka sasa tayari unalijua jibu, kuna kitu hakifanyiki.
Labda juhudi hizo haziwekwi kwa wingi na kama zinawekwa kwa wingi basi siyo kwa usahihi na kwa msimamo.
Ukianzia hapo utaweza kuona nini hakifanyiki na ukiwezesha kifanyike matokeo yatakuja.

Asili inajiendesha kwa kanuni zake yenyewe.
Kama hutazijua na kuzifuata kanuni hizo, utahangaika sana lakini hutapata matokeo unayotarajia kupata.
Kama matokeo hayapatikani, jua kuna vitu havifanyiki.
Jua ni vitu gani na uvifanye ili uweze kuzalisha matokeo unayoyataka.
Tusijidanganye wala kukubali kudanganywa kirahisi.
Matokeo yanatengenezwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe