3008; Shughuli muhimu zaidi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna shughuli nyingi sana unazojihusisha nazo kwenye maisha yako ya kila siku.
Lakini shughuli iliyo muhimu zaidi kuliko zote ni ile ya kujiingizia kipato.
Hiyo ndiyo shughuli muhimu kwa sababu ndiyo msingi mkuu wa maisha yako.

Kuingiza kipato ndiyo msingi wa kuyaendesha maisha yako.
Ndiyo kunakuwezesha kula, kuvaa, kuwa na malazi na kuweza kutunza familia.
Ukikosa kipato, mambo mengi sana kwenye maisha yako yanavurugika na unakosa umakini mzuri.

Cha kushangaza sasa, shughuli hii muhimu sana kwenye maisha ya kila mtu, watu wamekuwa hawaipi uzito wa kutosha.
Watu wengi wamekuwa wanaichukulia kawaida tu na matokeo yake ni kuingiza kipato cha kawaida na maisha yao kuwa magumu.

Halafu kuna wale ambao wanaipuuza kabisa shughuli hiyo, kwa kujidanganya kwamba fedha siyo kila kitu, kwamba kuna mambo mengine muhimu kwenye maisha kuliko fedha.
Watu hawa hujifariji na mengine wanayojihusisha nayo ambayo hayaingizi fedha. Na maisha yao huwa magumu sana.

Ni dhambi kubwa sana na kutokujitendea haki pale unapojidanganya kwamba fedha siyo muhimu kwako wakati bado hujawa na uhakika wa kipato.
Kama hujafika hatua ya kifedha ambapo maisha yako yote yaliyobakia unaweza kuyaendesha vizuri hata kama hafanyi kazi ya kukuingizia kipato moja kwa moja, basi kipaumbele cha kwanza kwako kinapaswa kuwa kuingiza fedha.
Usijidanganye kwa kitu kingine nje ya hapo, usiwe na unafiki wowote.
Weka kipaumbele chako kwa usahihi na kifanyie kazi.

Fedha inagusa kila eneo la maisha yako, hivyo kama haijawa na utulivu, maisha yako hayawezi kuwa na utulivu.
Na kujidanganya kwamba unajenga utulivu wa maisha nje ya fedha ni kuzidi kujipoteza.

Ukweli ni kwamba, usipoingiza kipato cha uhakika na usipojijengea utajiri na uhuru wa kifedha, unajiweka kwenye hatari ya kupoteza vitu vyote muhimu kwenye maisha yako.

Lengo lako kuu kwenye maisha ni kuwa tajiri (kuweza kununua chochote unachotaka) na kufikia uhuru wa kifedha (kuweza kuishi vizuri hata kama hafanyi kazi moja kwa moja).
Lengo lolote jingine kabla ya kufikia haya makuu ni kujidanganya na kujipoteza.
Na shughuli muhimu zaidi kwenye maisha ni ile inayokufikisha kwenye lengo hilo kuu, ambayo ni kuingiza kipato.

Shughuli hiyo kuu kwenye biashara inahusisha mauzo, ambayo ndiyo njia pekee ya kuingiza fedha kwenye biashara.
Hiyo inaturudisha kwenye msingi huo mkuu kwamba kuuza ndiyo shughuli kuu kwenye maisha.
Ni kupitia kuuza ndiyo utaweza kujenga maisha yoyote unayoyataka.
Kama kuna kitu hakipo sawa kwenye maisha yako, unaweza kukiweka sawa kwa kuuza zaidi.

Hili linatufikisha wapi basi, MAUZO NDIYO SHUGHULI KUU KWENYE MAISHA YAKO.
Kwa kuwa njia kuu kwetu kuingiza kipato ni kupitia kuuza vitu mbalimbali, mauzo yanakuwa ndiyo shughuli kuu kwenye maisha yetu.
Na hivyo tunawajibika kuwa wauzaji wazuri sana.

Ni muhimu uwe na njia sahihi ya kujipima kwenye shughuli hii kuu na kupiga hatua kubwa zaidi kadiri unavyokwenda.
Lazima uweze kupima pale ulipo sasa na kule unakopaswa kufika ili kupata utajiri na uhuru wa kifedha.

Hakuna kitu kama masikini mwenye furaha,
Au masikini mwaminifu.
Furaha na uaminifu haviwezi kukaa pamoja na umasikini.
Ni kujidanganya tu na kujipa moyo.
Na zaidi kuficha huzuni na maovu nyuma ya hilo.
Ni wajibu wako namba moja kuwa tajiri na kufikia uhuru wa kifedha.
Na shughuli muhimu zaidi kwako ni ile ya kuingiza fedha, ambayo ni mauzo.

Ninachotaka kusema mabibi na mabwana ni hiki, uza zaidi.
Utauza zaidi kwa kuwafikia watu wengi zaidi na kuwashawishi zaidi.
Utauza zaidi na zaidi kwa kuwahudumia watu wako zaidi na kuwafuatilia zaidi.
Una changamoto yoyote kwenye maisha yako, rudi kwenye mauzo ili kuweza kuitatua.

Usichanganye vipaumbele.
Kama hujafikia utajiri na uhuru wa kifedha, hilo ndiyo linapaswa kuwa kipaumbele namba moja kwako, mengine yote yanaweza na yanapaswa kusubiri.
Weka vipaumbele vyako sawa na usiwasikilize wanaokushauri kinyume na hilo, wana ajenda zisizo sahihi na maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe