3014; Kama hushindwi, unashindwa.

Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu huwa tunaepuka sana kushindwa.
Hiyo ni kwa sababu tumekuzwa tukiaminishwa kwamba kushindwa ni kubaya.
Tumeaminishwa anayeshindwa anakuwa na matatizo fulani.

Tangu utotoni, kushindwa kumekuwa kukiadhibiwa kwa namna mbalimbali.
Hilo limetujengea hofu kubwa kwenye kushindwa.
Na hofu hiyo imepelekea tusiwe tayari kujaribu vitu vipya, kwa kuwa hatutaki kushindwa.

Ili pia tusishindwe, tumekuwa tunajiwekea ndoto na malengo madogo sana.
Japo ndani yetu tunaweza kuwa tunataka zaidi, hatuthubutu kwenda na kile tunachotaka, kwa sababu tunahofia kushindwa.

Tunaweza kuona kutokushindwa ni ushindi mkubwa, kwa sababu jamii haipati nafasi ya kutukosoa na kutubeza kwenye kushindwa kwetu.
Lakini kwa uhasilia, kutokushindwa ni kushindwa.

Kama hushindwi kwenye maisha yako, maana yake hafanyi vitu vipya na vikubwa.
Unafanya vitu vidogo na vya kawaida sana, kitu kinachokukwamisha kupata matokeo makubwa na ya tofauti.

Hakuna kitu kinacholevya kama ushindi.
Ushindi unaleta kiburi na majigambo.
Ushindi unafanya mtu ajione tayari anajua na kuweza kila kitu, hivyo kutokuwa tayari kujifunza.
Hayo ndiyo yanayopelekea wengi kushindwa vibaya baada ya kuwa wamepata ushindi kidogo.

Kushindwa ni mwalimu mzuri sana.
Kushindwa kunaleta unyenyekevu.
Kushindwa kunafanya mtu ajione kuna mengi hajui hivyo anapaswa kujifunza.
Hayo ndiyo yanayopelekea watu kupata ushindi baada ya kuwa wameshindwa.

Ni muhimu uwe na ndoto na malengo makubwa,
Ambavyo vitakusukuma ufanye zaidi ya ulivyozoea.
Hilo litakuweka kwenye mazingira ya kushindwa.
Kitu ambacho kitakusukuma uwe bora zaidi na kuweza kufikia ndoto na malengo makubwa uliyonayo.

Na pale unapofikia ndoto na malengo hayo, usibweteke, badala yake weka ndoto na malengo mengine makubwa zaidi na pambana kufanyia kazi.

Kila wakati hakikisha unakuwa kwenye hali ya kujisukuma zaidi ili kuweza kupata matokeo makubwa zaidi.
Ukibweteka na matokeo yoyote unayoyapata, kwa kujiona tayari umeshashinda, unakuwa umejiweka kwenye nafasi ya kushindwa zaidi.

Kushindwa ni ushindi mkubwa kama utatumia vizuri.
Ondoa kila hofu ya kushindwa na mara zote kuwa katika hali ya kufanya mapya na makubwa ambayo hujawahi kuyafanya.
Unaposhindwa unajifunza na kuwa bora zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe