3022; Kushindwa kabla ya kuanza.

Rafiki yangu mpendwa,
Kufanya jambo lolote jipya na kubwa kwenye maisha yako, huwa kunaambatana na hatari ya kushindwa.

Hatari ya kushindwa huwa inakuwa kubwa pale mtu unapokuwa unafanya kwa mara ya kwanza.
Kukosa uzoefu kunapelekea mtu kufanya makosa mengi yanayomuathiri.

Lakini kushindwa huwa kunakuwa ni kwa uhakika, kabla hata ya kuanza, pale ambapo mtu anaiga na kutaka kuwa kama mtu au watu fulani.

Iko hivi rafiki, wakati unaanza kufanya kitu chochote, kuna watu ambao huwa unajifunza kutoka kwao.
Wengi, kutokana na ubobezi wa yule wanayejifunza kutoka kwake, wanatamani sana wangekuwa kama yeye.

Kinachotokea ni mtu kupoteza muda na nguvu kutaka kuwa kama mtu fulani, kitu ambacho hakiwezi kutokea.

Ukianza tu ukiwa na lengo la kutaka kuwa kama mtu fulani, unaanza ukiwa umeshindwa.

Hiyo ni kwa sababu pamoja na ufanano wetu binadamu, kila mmoja ana kitu ambacho ni cha kipekee kabisa, ambacho hakiingiliani na vitu vingine vyovyote.

Wajibu wako mkubwa ni kujua kile ambacho ni cha kipekee kwako na kisha kukitumia kwenye mambo yote unayofanya.

Lile eneo ambalo uko bora kuliko wengine, unapaswa kulitumia vizuri kujitofautisha kwenye chochote unachofanya.

Weka utu na utofauti wako kwenye kila unachofanya, lengo likiwa ni kujitofautisha na wengine wanaofanya kitu hicho.

Usiingie kufanya chochote kwa lengo la kuwa kama wale unaowakubali.
Bali ingia ukiwa na lengo la kufanya kwa ubora wa hali ya juu kabisa, ukiwa umeweka upekee ulio ndani yako.

Kitu kingine kinachofanya kuiga kuwe hatari ni mabadiliko yanayokuwa yanaendelea.
Kitu chochote kilichofanya kazi vizuri jana, kinaweza kisifanye kazi vizuri leo au kufika hatua ya kutokufaa kabisa kesho.

Mambo yanabadilika kwa kasi kubwa kiasi kwamba mtu asipobadilika anaachwa nyuma haraka sana.
Hata wale unaowaona wamefanikiwa sana na kutaka kuwa kama wao, kama wakifilisika na kuhitajika kuanza upya, hawatarudia yote waliyofanya huko nyuma.
Badala yake watabadili na kuboresha ili kuendana na hali halisi ilivyo.

Hivyo ndivyo mafanikio yanavyojengwa kwenye kila ngazi ya maisha, kuendana na hali halisi ilivyo.
Kutaka kurudia kile ambacho tayari ni cha uhakika ni kuchagua kushindwa kabla hata hujaanza, kwa sababu mambo hayaendi jinsi ambavyo unataka wewe yaende.

Ni vizuri sana kuwa na mashujaa kwenye maisha yetu,
Watu ambao kwa kuwaangalia tunapata matumaini kwamba chochote kikubwa tunachotaka kukifikia kinawezekana.
Ubaya ni pale tunapotaka kuwa kama mashujaa wetu, hapo ndiyo tunakuwa tumeshindwa kabla hata ya kuanza.
Kila mtu ana upekee wake ambao hauwezi kuigwa na wengine.

Unapowaangalia mashujaa wako, angalia jinsi ambavyo kila mmoja kuna kitu cha kipekee anacho.
Matumizi sahihi ya kitu hicho cha kipekee ndiyo yanakuwa yamemweka mtu kwenye nafasi ya kufanya makubwa kuliko wengine.

Anza na ushindi, siyo kwa kuwa kama wengine, bali kwa kujitambua na kuwa wewe.
Kuna nguvu kubwa sana kwenye kuwa wewe, nguvu ambayo wengi hawaifikii na kuweza kuitumia.
Ifikie na kuitumia nguvu hiyo ili uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Na hapo ndipo mafanikio yanapokuwa magumu kwa wengi, hawapati nafasi ya kujitambua wao wenyewe na kufikia na kutumia uwezo mkubwa wa ndani.
Wanachokuwa wanafanya ni kuiga yale wengine wanafanya, kwa namna wanavyoyafanya na hilo kuwa kikwazo kwao.

Unaweza kuiga njia mbalimbali zinazofanya kazi kwa watu wengine.
Lakini mwisho wa siku lazima uzifanyie kazi kwa namna ya kipekee kwako ili uweze kupata matokeo yaliyo bora kabisa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe