3023; Tatizo na suluhisho.

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna kauli inayosema, ukiwa na nyundo, kila kitu kinaonekana kama msumari ambao utashawishika kuugonga na nyundo hiyo.

Hiyo ina maana kwamba unapokuwa na suluhisho fulani ambalo unalikubali na kulipenda sana, ni rahisi kuona kila tatizo linaweza kutatuliwa na suluhisho hilo.

Unapokuwa unapenda suluhisho ulilonalo, unajikuta ukitafuta matatizo ambayo suluhisho hilo linaweza kutatua.
Hiyo inapelekea uhangaike na matatizo ambayo hayana tija kwako, hasa kwenye malengo unayokuwa nayo.

Mbaya zaidi, unapokuwa unapenda suluhisho ulilonalo, unalazimisha kila tatizo liweze kutatuliwa na suluhisho hilo. Kinachotokea ni unatatua vibaya matatizo ambayo ni muhimu kwa kule unakoelekea.

Kwenye safari yako ya mafanikio makubwa, unachohitaji siyo suluhisho la kila tatizo, bali kuweza kuyajua matatizo muhimu na kuyatatua kwa usahihi.
Na hilo litawezekana kama utabadili mtazamo wako kutoka kwenye kutatua tatizo kwenda kwenye kutafuta tatizo.

Hivi ndivyo unavyoweza kutekeleza hilo;

Elezea mafanikio; jua kwa hakika matokeo unayotaka kupata mwishoni.

Tambua matatizo; orodhesha vikwazo vyote vinavyokuzuia kufikia matokeo ya mwisho unayoyataka.

Weka vipaumbele; pangilia orodha ya matatizo hayo kwa umuhimu wake, ukianza na yaliyo muhimu zaidi.

Rejea; chagua tatizo la juu kisha jiulize, “Ni tatizo gani ninalojaribu kutatua?”
Usikimbilie kwanza kutatua tatizo, bali anza kwa kulielewa tatizo kwa kina, jwa kuandika njia tofauti tofauti za kuliona tatizo.

Unapoanza na suluhisho, unakuwa na njia moja pekee ya kutatua tatizo, kitu ambacho kinakuwa siyo sahihi.
Unapoanza na tatizo, unakuwa na njia nyingi za kutatua tatizo, kitu kinachokupa njia bora ya kutatua tatizo.

Kwenye safari ya mafanikio, huwa tunayaona matatizo tunayokutana nayo kama ndiyo kikwazo cha kufanikiwa.
Lakini hilo siyo kweli, kikwazo cha mafanikio yetu ni suluhisho tunalokuwa nalo, ambalo tunalazimisha litatue kila tatizo.
Kwa kuwa tuna nyundo, kila kitu kinaonekana msumari na hapo tunajikuta tukitatua kwa namna isiyo sahihi.

Kuwa na suluhisho linalotatua vizuri tatizo moja, haimaanishi litaweza kutatua kila tatizo.
Jifunze kuanza kila tatizo upya ili kulielewa na kulitengenezea suluhisho sahihi ndiyo uweze kupata kile unachotaka.

Kikwazo kikubwa cha mafanikio kwa walio wengi siyo kushindwa kutatua matatizo makubwa wanayokutana nayo, bali kushindwa kuyaelewa kwa kina matatizo hayo na kujua utatuzi wake sahihi.

Kuanzia sasa anza na tatizo kabla ya suluhisho na fikra zako zitakuwa huru kulielewa tatizo na kulitengenezea suluhisho sahihi.

Na kila unapokuwa na nyundo, jikumbushe siyo kila tatizo ni msumari wa kugonga, mengine ni ya kukata.
Anza na tatizo ili kupata suluhisho sahihi, badala ya kuanza na suluhisho na kulazimisha litatue kila tatizo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe