3028; Maamuzi ya mtu mmoja.

Rafiki yangu mpendwa,
Makosa mengi kwenye maisha huwa yanafanyika wakati wa kufanya maamuzi.
Na kadiri watu wengi wanavyohusika kwenye kufanya maamuzi, ndivyo nafasi za kufanya makosa zinavyokuwa nyingi.

Maamuzi bora ni yale yanayofanywa na mtu mmoja, ambaye ana uelewa wa kina kuhusu kile anachokiamulia.
Mtu huyo anaweza kuchukua maoni ya wengine, lakini ana uhuru wa kuamua kile kinachofaa na siyo kuamua ili kuwaridhisha wengine.

Kadiri maamuzi yanayotakiwa kufanywa yanavyokuwa makubwa na muhimu, ndivyo wengi huhofia kuyafanya peke yao na hivyo kutafuta kikundi cha watu cha kujificha nyuma yao.

Hivyo ndivyo kamati mbalimbali huzaliwa.
Kamati huwa zinaundwa ili kuelewa jambo kwa kina na kulifanyia maamuzi.
Lakini kwa bahati mbaya sana, siyo wote wanaokuwa kwenye kamati wanakuwa wametenga muda na kuelewa kwa kina kile wanachopaswa kuamua.

Hivyo unapofika wakati wa kufanya maamuzi, wanaishia kufuata mkumbo wa wengi wako upande gani.
Maamuzi ya kuangalia watu wengi wako upande gani hayajawahi kuwa maamuzi sahihi.
Na hilo ndiyo linafanya maamuzi yanayofanywa na kamati kutokuwa sahihi.

Wewe kama kiongozi mkuu wa biashara yako, unapaswa kuwa ndiye mfanyaji maamuzi mkuu kwenye biashara hiyo.
Hivyo epuka sana kujificha nyuma ya kamati au watu wengine.
Hakuna anayeweza kujali kuhusu biashara yako zaidi yako wewe mwenyewe.

Hili halimaanishi uwe na kiburi na usisikilize maoni ya wengine.
Sikiliza maoni ya wengine, ila yachuje kwa uhakika kabla hujayatumia kufanya maamuzi.
Maoni mengi unayokuwa unapewa na watu ni ya jumla na ya juu juu. Hayajazingatia jambo kwa kina na msingi wake.

Ni muhimu kushirikiana na wengine kwenye ujengaji na uendeshaji wa biashara yako.
Lakini wewe mwanzilishi, ambaye ndiye mbeba maono makubwa ya biashara yako, unapaswa kuwa ndiye mfanyaji maamuzi mkuu kwenye biashara.

Endelea kujinoa na kuwa bora kupitia maamuzi yote unayoyafanya.
Unapofanya maamuzi, andika sababu ulizotumia katika kuyafanya.
Kisha matokeo yanayopatikana, yapime pia na matarajio yako, na hapo utaweza kulinganisha matokeo yanayopatikana na matarajio yaliyokuwepo.
Unafanya hivyo siyo kwa ajili ya kujiumiza kwa matokeo ya tofauti unayokuwa umepata, bali kujiboresha ili wakati mwingine ufanye maamuzi bora zaidi.

Kila nchi ina raisi mmoja,
Lila jeshi lina jenerali mmoja,
Na kila kampuni ina CEO mmoja.
Haimaanishi kwamba watu hao waliopata hizo nafasi ndiyo wajanja kuliko watu wengine wote.
Bali inamaanisha ni watu ambao wamejitoa kuwajibika kwenye kile wanachoongoza.

Usipokuwa tayari kukosea,
Na usipokuwa tayari kujifunza na kulielewa eneo lako kwa kina,
Hutaweza kujijengea hali ya kujiamini na kufanya maamuzi sahihi.
Utajikuta ukihangaika na mambo mengi lakini ukikwepa kufanya maamuzi kwenye mambo ambayo ni muhimu.

Ni muhimu sana maamuzi yote makubwa yafanywe na mtu mmoja.
Mtu mwenye uelewa wa kina kwenye eneo hilo na ambaye anachukua maoni ya wengine na kuyachakata vyema.

Sisi viongozi wa biashara ndiyo watu sahihi wa kufanya maamuzi yote makubwa kwenye biashara.
Hivyo tunapaswa kuhakikisha kila wakati kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya maamuzi bora na yenye tija.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe