3029; Msimu wa HAPANA.

Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna neno moja lenye nguvu kubwa sana kwenye safari yako ya mafanikio kama neno HAPANA.
Hapana siyo tu neno, bali ni sentensi inayojitosheleza.

Ili uweze kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako na kufika kule unakotaka kufika, lazima useme HAPANA kwa mambo mengi sana.

Kusema HAPANA ni rahisi kueleza, lakini ngumu sana kutekeleza, hasa pale tunapohitajika kusema HAPANA kwenye vitu ambavyo tumeshazoea.
Pia kusema HAPANA ni rahisi pale inapokuwa mara moja moja, lakini ngumu sana pale inapokuwa kwenye mengi na kwa muda mrefu.

Kwenye safari kubwa ya ubilionea ambayo tupo, siyo tu tunahitaji kusema HAPANA kwenye baadhi ya vitu, bali tunahitaji kusema HAPANA kwenye kila kitu isipokuwa yale tu yanayotufikisha kwenye lengo.

Na hapo ndipo tunahitaji kuingia kwenye msimu muhimu sana wa maisha yetu, MSIMU WA HAPANA.
Msimu wa HAPANA ni kipindi cha maisha ambapo tunasema hapana kwa mambo yote ambayo hayana mchango kwenye lengo kuu tulilonalo, yaani yote kabisa.
Umakini wetu wote unakwenda kwenye yale tu yanayotufikisha kwenye lengo kuu tulilonalo.

Msimu wa HAPANA ni kipindi ambacho kinahitaji ujasiri wa hali ya juu, kwani mengi unayohitaji kuyakataa tayari ni mazoea kwenye maisha yako.

Kwenye huu msimu wa HAPANA, siyo tu unasema HAPANA kwa yale ambayo ni usumbufu, bali pia unasema HAPANA kwa yale ambayo ni mazuri kwenye maisha yako, lakini hayana mchango kwenye malengo makubwa uliyonayo.

Hapa kuna maeneo matano ya maisha yako ambayo unapaswa kuyasemea HAPANA kwenye huu msimu wa HAPANA;

Moja; Hapana kwa familia.

Hapana kubwa na ngumu unayopaswa kusema kwenye maisha yako ni kwa familia yako.
Familia yako ina tabia ya kutaka kukupangia ni namna gani uende na maisha yako.
Inaweza kufanya hivyo kwa nia njema kabisa, kwa sababu haitaki uumie, lakini nia hiyo njema haiwezi kukufikisha kwenye mafanikio makubwa unayoyataka.

Hivyo ni lazima useme HAPANA kwa mambo mengi ambayo familia yako inataka kwako, ambayo hayaendani na lengo lako kubwa.
Ni vigumu kusema HAPANA kwa familia kwa sababu ina tabia ya kutumia hatia kukufanya ukubaliane nayo.
Pale unapochagua kufanya mambo yako unaonekana kama mtu usiyejali familia.
Lakini ukweli ni kwamba utakuwa na manufaa makubwa sana kwa familia yako pale utakapopata mafanikio makubwa.
Hivyo kubali lawama na hatia za muda mfupi ili uweze kupata mafanikio makubwa ya muda mrefu.

Mbili; Hapana kwa marafiki.

Marafiki ni kundi jingine ambalo unahitaji kusema HAPANA sana kwenye huu msimu ambao tupo.
Marafiki zako, ambao ni watu wa karibu sana kwako wana ushawishi mkubwa sana kwako.
Watu hao ni rahisi kukuondoa kwenye mambo yaliyo muhimu kwako na kukupeleka kwenye mambo ambayo siyo muhimu.

Pale unapochagua kuweka muda wako wote kwenye malengo yako makubwa, marafiki zako watakuwa wa kwanza kukulaumu kwamba huwajali tena.
Watakuonyesha kwamba umebadilika.
Hupaswi kujali hilo wala kuhofia kuwapoteza marafiki kwa sababu kubwa tatu;
1. Marafiki wa kweli watakuelewa na kuheshimu maamuzi yako, hivyo watakuunga mkono na kuendelea kuwa wa msaada kwako kufikia ndoto zako.
2. Hata kama marafiki zako hawatakuelewa, utakapofanikiwa, bado watakuwa wanakuhitaji sana, hivyo hakuna utakachopoteza.
3. Na hata kama utawapoteza marafiki wako kwenye msimu wa HAPANA, kwenye safari yako ya mafanikio utatengeneza marafiki wengine wanaoendana na aina mpya ya maisha yako.

Usiogope kusema HAPANA kwa marafiki zako wa karibu katika hiki kipindi.

Tatu; Hapana kwa fedha.

Kusema HAPANA kwenye fedha ndiyo eneo jingine gumu sana na ambalo wengi huwa wanashindwa.
Na hili linachanganya kidogo, japokuwa mafanikio makubwa unayoyapigania yanahusisha fedha, inabidi useme HAPANA kwenye fedha.

Hapa inamaanisha kusema HAPANA kwenye vifursa vidogo vidogo vinavyojitokeza vya kuingiza fedha, lakini haviendani na lengo kuu ulilonalo.
Kuna fursa zinaweza kujitokeza mbele yako za kuingiza fedha, lakini ukizifanyia kazi unakuwa umetoa muda na umakini wako kwenye lengo lako kuu.
Ndiyo utapata fedha kidogo kwenye fursa hizo, lakini unakuwa umejizuia kupata fedha nyingi zaidi kwenye fursa kubwa zaidi za baadaye.

Hivyo unapaswa kuwa na ujasiri wa kusema HAPANA kwenye fursa mbalimbali za kuingiza fedha zinazojitokeza mbele yako kila mara.
Weka akili, muda, nguvu na umakini wako wote kwenye lengo kuu unalofanyia kazi na matokeo utakayoyapata yatakuwa makubwa sana.

Huwa nasema, hela ndogo ni adui wa hela kubwa. Unapohangaika na fursa ndogo ndogo zinazokuingizia fedha kidogo, unakuwa umejizuia kwenye fursa kubwa zinazoweza kukuingizia fedha nyingi.
Usikimbizane na kila fursa inayoweza kukuingizia kipato, kataa fursa ndogo ndogo na nyingi zinazokujia ili ukae kwenye fursa yako kuu.

Nne; Hapana kwa matukio ya kijamii.

Kuna matukio mengi ya kijamii ambayo huwa yanachukua muda, nguvu na umakini wako mwingi.
Kuanzia burudani na starehe mbalimbali ambazo umeshazizoea, mpaka kwenye mambo unayohusiana na wengine kwenye jamii.
Hapa ni mambo kama sherehe, michezo, vikundi mbalimbali na matukio mengine yanayotaka muda wako.

Unahitaji kusema HAPANA kwa mambo yoyote yale ambayo yanachukua muda wako ambao ungeweza kuutukia kwenye lengo lako kuu.
Sema HAPANA kwa michezo mbalimbali unayopenda kuifuatilia.
Sema HAPANA kwa sherehe mbalimbali unazoalikwa kushiriki.
Huhitaji kuwa kwenye kila kamati, kila kikundi na mikusanyiko mingine ya kijamii.

Jamii inaweza kukufanya ujione una hatia kwa kukataa kuendana nayo kwenye kila kitu, lakini utakapopata mafanikio makubwa, utakuwa wa msaada mkubwa kwa jamii hiyo hiyo.
Hivyo usihangaike kuiridhisha jamii kwa kuenda vile inataka uende, pambania mafanikio yako makubwa na hayo yatakupa heshima kubwa kwenye jamii yako.

Tano; Hapana kwa tamaa za mwili.

Halafu sasa kuna kusema HAPANA kwenye tamaa za mwili.
Mwanafalsafa Seneca amewahi kusema; mwili inabidi uteswe ili uweze kuwa na utii kwenye akili.
Kama hutaweza kuutesa mwili wako, jua pia hutaweza kufikia mafanikio makubwa unayoyataka.

Na huutesi mwili wako kwa kuumiza kwa makusudi, bali unautesa kwa kuuambia HAPANA kwa tamaa mbalimbali ambazo mwili wako unakuwa nazo.

Sema HAPANA kwa tamaa ya kupata vilevi na mambo mengine ya kuburudisha mwili.
Sema HAPANA kwa tamaa ya kupumzika pale ambapo hujaweka kazi ya kutosha.
Sema HAPANA kwa tamaa ya kufanya mapenzi mara kwa mara hasa na watu wasio wenza wako halali.
Sema HAPANA kwenye tamaa ya kula vitu vitamu na mara kwa mara.

Mwili ni wako, unatakiwa uutumie kufika kule unakotaka kufika na siyo ukutumie wewe kuhangaika na tamaa mbalimbali.
Kama hutaweza kudhibiti mwili wako kwa kujiambia HAPANA, hutaweza kufanya makubwa.

Rafiki yangu mpendwa na Bilionea uliye Mafunzoni, tumeuanza rasmi MSIMU WA HAPANA.
Msimu huu utakwenda mpaka pale wote tutakapokuwa tumefanikiwa kujenga biashara zinazoweza kujiendesha zenyewe bila ya uwepo wetu wa moja kwa moja.

Kabla ya kufikia hatua hiyo, mambo yote ni HAPANA, isipokuwa tu kwenye biashara moja tunayojenga na kwenye uwekezaji tunaoendelea kufanya kidogo kidogo kila mara.
Kwa kipindi chote, akili yako, muda wako, nguvu zako na umakini wako wote unaweka kwenye kujenga biashara yako kuu na kufanya uwekesaji.
Mengine yote yasiyokuwa na mchango kwenye hayo mawili, jibu lake ni HAPANA.
Hiyo ni HAPANA ambayo haina mjadala.

Unahitaji kuwa imara sana kwenye huu msimu wa HAPANA, kwa sababu hakuna atakayekuelewa.
Utakutana na changamoto nyingi na hata kushindwa, lakini usirudi nyuma.
Huu ndiyo msimu wa kukaa kwenye mchakato kwa asilimia 100 bila kuyumba na kuambatana na watu sahihi kama kuwa hapa kwenye programu ya BILIONEA MAFUNZONI.

Uzuri ni kwamba, ukishapata mafanikio makubwa, kila mtu atakuja kwako, atakusifia na kuona umefanya vyema.
Ila kabla hujayapata mafanikio hayo, kila unachofanya unakosea.
Kubali hilo ili uweze kufika unakotaka kufika.

Rafiki, hebu fikiria ni hatua kubwa kiasi gani utakazopiga kwenye maisha yako kama kila siku kuanzia saa 10 alfajiri mpaka saa 2 usiku unaweka muda, nguvu, akili na umakini wako wote kwenye kujenga biashara yako kuu na kujenga uwekezaji?
Kwa hakika ni hatua kubwa mno mno.
Hivyo basi, kubali kukaa kwenye msimu huu wa HAPANA.

Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini orodha ya mambo ambayo kuanzia sasa ni HAPANA kwenye huu msimu wa HAPANA.
Orodhesha yote mazuri uliyokuwa unayafanya ila hayana mchango kwenye lengo na kuanzia sasa acha kuyafanya.
Karibu kila mmoja kushirikisha hayo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe