3030; Unafanya ambavyo hawafanyi.

Rafiki yangu mpendwa,
Imezoeleka kwamba, kama unataka kufanikiwa, angalia yale ambayo waliofanikiwa wanayafanya kisha na wewe uyafanye.

Kwamba mafanikio huwa yanaacha alama, kama utaangalia waliyofanya waliofanikiwa na wewe ukayafanya, utafanikiwa sana.

Ni kweli kwamba mafanikio huwa yanaacha alama.
Lakini kwenye kufanya yale ambayo waliofanikiwa wanayafanya, kuna ugumu mkubwa.
Hiyo ni kwa sababu tayari kila mtu ametingwa na mambo mengi ya kufanya.

Kila mtu, hata ambaye hajafanikiwa, tayari siku yake nzima imejaa mambo mbalimbali ya kufanya.
Hivyo kudhani mtu atapata nafasi ya kuweka yale ambayo waliofanikiwa wanayafanya ni kujidanganya.

Njia bora ya kujifunza kwa waliofanikiwa siyo kwa kuangalia wanayofanya kisha kuyaiga, badala yake ni kuangalia yale ambayo hawayafanyi kisha kuacha kuyafanya pia.

Kwa kuwa tumeona tayari kila mtu ametingwa na mambo mengi, njia ya kupunguza mambo ya kufanya ina nguvu kubwa.
Kwa kuondoa mambo mengi unayofanya ambayo hayana tija, unabaki na uwanja mpana wa kuweza kufanyia kazi yale yaliyo muhimu zaidi na yanayokupeleka kwenye mafanikio makubwa zaidi.

Watu wamekuwa wakilalamika kwamba hawana muda wa kufanya mambo muhimu.
Lakini ukiangalia siku zao nzima, tayari wametingwa na mengi wanayofanya.

Hiyo ina maana kwamba, ukipunguza mambo mengi unayofanya kwa sasa na kubaki na machache muhimu, utaweza kupata muda wa kufanya mengine muhimu unayotaka kufanya.

Muda wa kufanya chochote muhimu kabisa unachotaka kufanya upo, unachohitaji ni kuacha kufanya baadhi ya vitu unavyofanya sasa ambavyo siyo muhimu zaidi, ili ubaki na muda wa kufanya yaliyo muhimu.

Kuna zoezi moja rahisi sana kwako kufanya kama unataka kupunguza mambo mengi unayoyafanya.

Fungua ukurasa mpya kwenye kijitabu chako kisha ugawe sehemu mbili.
Upande wa kushoto orodhesha mambo yote ambayo umeyafanya ndani ya siku saba zilizopita. Andika yote kabisa bila kuacha hata moja.
Upande wa kulia andika malengo yako makubwa unayoyafanyia kazi.
Kisha chora mstari kutoka kwenye kila ulichofanya kwenda kwenye lengo ambalo kinatimiza.
Kwa vitu ambavyo vimekosa mstari unaoenda kwenye lengo, ndiyo unavyopaswa kuacha kuvifanya mara moja.
Hivyo ndiyo vitu vinavyokufanya utingwe sana wakati hakuna mafanikio makubwa unayoyapata.

Tayari kuna mambo mengi sana unayoyafanya ambayo hayana mchango wowote kwako kufanikiwa.
Anza kwa kuyatambua na kuacha kuyafanya mara moja ili utoe mwanya wa kufanya vizuri yale yaliyo muhimu na yenye tija.

Wakati wote ambao upo hai, unao muda wa kutosha kufanya chochote muhimu unachopaswa kufanya.
Pa kuanzia ni kuacha kufanya mengi unayofanya sasa, yasiyokuwa na tija.

Na kila unapowaangalia wale waliofanikiwa kuliko wewe, usijiulize nini wanafanya ambacho wewe hufanyi, bali jiulize ni vitu gani wewe unavyofanya ila wao hawafanyi?
Kujiuliza swali hilo kunakupa fursa ya kuyatambua yale yasiyo muhimu na kuachana nayo ili kuweza kuhangaika na yaliyo na umuhimu kubwa.

Punguza sana mambo unayofanya ili akili yako iweze kukaa kwa umakini kwenye yale yaliyo muhimu zaidi kufanya.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe