3031; Muda wa kutosha kwenye kazi.

Rafiki yangu mpendwa,
Tupo kwenye msimu wa HAPANA, kipindi cha kusema HAPANA kwa mengine yote isipokuwa kujenga biashara zetu kuu na kufanya uwekezaji.

Lengo kuu la kuingia kwenye msimu huu wa HAPANA ni kuondokana na mambo ambayo huwa yanakuwa usumbufu kwetu na kupunguza muda wetu wa kuweka kazi.

Katika kusoma vitabu, nimekutana na barua fupi ambayo Steve Jobs aliandika kwa wafanyakazi wake mwaka 1986.
Barua hiyo imeelezea kwa ufupi dhana hii ya HAPANA ili kupata muda wa kutosha kuweka kazi.

Nitashirikisha hapa jinsi barua hiyo ilivyokuwa inaeleza, ili tuweze kujifunza na kuchukua hatua kuwa bora zaidi.

N E X T

1 7 M a r c h 1 9 8 6

M E M Ο

Kampuni yetu imejengwa kwenye msingi mkuu kwamba watu wazuri wachache wanaweza kuzalisha matokeo bora sana kama hawatasumbuliwa na;
a) kulazimika kushawishi kundi kubwa la watu kuhusu nini ni sahihi, na
b) kama wanaweza kuweka muda wao mwingi kwenye kazi zinazozalisha badala ya kusimamia wengine ambao hawawezi kufanya kazi zao vizuri.

Ili kusimamia msingi huo, napendekeza mambo haya mawili;
1) Kila mtu anahitaji muda wa kufanya kazi bila kusumbuliwa. Mikutano mbalimbali ya nje na ndani inakula muda mwingi wa kazi. Hivyo napendekeza siku ya alhamisi kuwa siku ambayo hakuna mikutano ya aina yoyote ile. Iwe ni siku ya kujifungia na kila mtu kufanya kazi yake kwa ukimya.
2) Tupitie uhitaji wetu wa watu ili kuwa na tahadhari kwenye kuajiri. Niwakumbushe kuna mstari mwembamba sana kwenye kuajiri ambao ukiuvuka unaishia kuwa na watu wengi na hapo kazi yako kubwa inakuwa kuwasimamia badala ya kuzalisha. Tusiruhusu hilo kutokea, ni bora kuwa na watu wachache hata kama itamaanisha kufanya kwa uchache. Tujenge kampuni yetu taratibu na kwa umakini.

Tutajadiliana zaidi juu ya haya kwenye mkutano wa kesho.
Asanteni.

Steve Jobs

Kuna mambo mengi sana ya kuondoka nayo kwenye barua hii fupi ya Steve Jobs.
Lakini kubwa sana ambalo napenda kila mmoja wetu kulifanyia kazi kwenye huu msimu wa HAPANA tuliopo ni kutenga muda wa kutosha wa kufanya kazi bila ya usumbufu.

Ukikagua unavyofanya kazi sasa, utagundua muda mwingi wa kazi unaingiliwa na usumbufu wa kila aina.
Kuanzia simu yako ambayo ina kila aina ya fursa ya usumbufu, ukienda kwa wengine, ni usumbufu kila kona.

Unaweza kutenga masaa 10 ya kufanya kazi kwa siku, ukaishia kufanya kazi ya uhakika kwenye masaa 2 tu.
Unakuwa na siku ndefu na yenye uchovu, lakini hakuna matokeo makubwa unayozalisha.
Hiyo ni kwa sababu masaa 8 katika 10 ya kufanya kazi, umeyatumia kwenye usumbufu.
Na hapa usumbufu tunamaanisha yale yote ambayo hayachangii moja kwa moja kwenye lengo lako kuu.

Hapa ni mapendekezo makubwa ninayokupa ya kutenga na kupangilia muda wako vizuri ili uweze kuzalisha matokeo bora.

1. Tenga masaa 10 ya kazi ya uhakika kwenye kila siku yako.

2. Masaa 2 yatumie kujenga na kupitia mifumo mbalimbali ya kuendesha biashara yako.

3. Masaa 2 yatumie kwenye kujenga timu yako ya biashara, kupitia vikao muhimu na timu yako na hata kwa mtu mmoja mmoja.

4. Masaa 4 kujenga wateja wakubwa kwenye biashara yako ambao watakuwa wa uhakika.

5. Masaa 2 ya kupitia taarifa na ripoti mbalimbali pamoja na kuboresha mikakati inayofanyiwa kazi kwenye biashara.

Hayo ni masaa 10 ya kuweka kwenye kazi kwa uhakika. Kwenye masaa hayo 10 unafanya hayo tu uliyopanga na kutokuruhusu usumbufu wowote, hasa wa simu na mikutano mbalimbali.
Mengine yote unayokuwa unahitaji kufanya, unayafanya kwenye hiyo hiyo siku yako, ila nje ya masaa hayo 10.

Unahitaji muda kwa ajili ya kujifunza, angalau masaa 2 kila siku.
Unahitaji muda kwa ajili ya mikutano ya nje.
Na unahitaji muda kwa mambo binafsi, kama kula, kutoka sehemu moja kwenda nyingine n.k.
Ili siku yako iweze kuwa bora na ukamilishe yote unayotaka kukamilisha, siku yako inabidi isiwe chini ya masaa 16 ya kazi.

Na ndiyo maana unaona msimu wa HAPANA unahitajika sana, maana ukishaondoa masaa 16 ya kazi, unabaki na 8 tu ambayo ndiyo unahitaji kulala humo humo na kuipa familia na watu wa karibu.
Bila ya kusema HAPANA kwenye kila kitu, hayo hayatawezekana.

Na pendekezo kubwa zaidi ninalokupa ni kuchagua siku moja kwenye wiki ambayo hiyo utaifunga yote kabisa kwa ajili ya kutekeleza mipango ya wiki ambayo imeshindwa kukamilika kwa sababu mbalimbali.
Ukishaipangilia wiki yako, hakikisha unakazana kuikamilisha.
Hivyo tenga siku moja ya wiki ambapo utakamilisha yote ambayo yamekwama kukamilishwa.
Siku hiyo inakuwa ni ya kazi ya uhakika kwa masaa yote 16 bila kuruhusu usumbufu wowote ule.
Siku hiyo unakuwa hupatikani kabisa kwa namna yoyote ile.

Haya ni mambo yanayokutaka ujitoe kweli kweli, lakini ambayo matokeo yake ni mazuri sana unapoyafanya kwa msimamo.

Tukae kwenye msimu huu wa HAPANA kwa uhakika ili kuweza kuzalisha matokeo makubwa na bora sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe