3032; Ua ndoto zao.

Rafiki yangu mpendwa,
Tupo kwenye msimu wa HAPANA, msimu wa kusema hapana kwenye kila kitu isipokuwa kujenga biashara yako kuu na kufanya uwekezaji.

Kitu kimoja kikubwa ambacho utakutana nacho mara kwa mara kwenye msimu huu wa HAPANA ni lawama za watu wengine.

Kwa kuwa ulishawazoesha watu kwa namna fulani huko nyuma, kitendo cha kuwaambia HAPANA kwa mambo ambayo huko nyuma ulikuwa unayakubali, wataona umebadilika.

Hilo litawaumiza sana na hivyo kukupa lawama kwamba hujali au unajiona ni bora zaidi.

Kinachowafanya watu wakulaumu ni ndoto walizonazo kuhusu wewe.
Kila mtu kwenye maisha yako kuna ndoto kubwa aliyonayo kuhusu wewe, ambayo inahusisha yeye kupata manufaa fulani.

Yaani iko hivi, kila mtu anataka uwe vile anavyotaka yeye, ili aweze kujinufaisha kupitia wewe.
Unapokataa kuwa vile wanavyotaka, ndipo unapoibua lawama kwa wale ambao walishajipanga kunufaika kupitia wewe kuishi vile wanavyotaka wao.

Njia pekee ya wewe kufikia ndoto zako kubwa ni kuwa tayari kuua ndoto ambazo wengine wanazo juu yako.
Ndoto ambazo watu wako wa karibu wanazo kuhusu wewe ni zile ambazo zina manufaa fulani kwao wenyewe, bila kujali kama una ndoto nyingine kubwa.

Ni wajibu wako kuua ndoto zote ambazo watu wanazo kwako ili uweze kupigania ndoto yako kuu kwenye maisha yako.

Katika kufanya hayo, lazima uwe na ngozi ngumu sana.
Lazima uwe tayari kupokea lawama nyingi ambazo watu wako wa karibu watazileta kwako.
Ni lazima sana uchague kuwa wewe ili uweze kufikia ndoto kubwa ulizonazo na kuepuka mitego ambayo watu wengine wamekuwekea ili uwanufaishe wao.

Kwenye hii safari ya mafanikio, lawama hazikwepeki.
Mafanikio makubwa unayoyataka yatahitaji mabadiliko makubwa kwenye maisha yako, kuanzia kwenye fikra zako mpaka matendo yako.

Mabadiliko yoyote utakayoyafanya kwenye maisha yako lazima yataibua lawama kwa wengine. Hiyo ni kwa sababu mabadiliko yako yanavuruga manufaa ambayo walikuwa wanayapata.

Watu wanataka uendelee kwenda vile ulivyozoea kwenda, kwa sababu tayari wameshaweka njia za kunufaika na mwenendo wako.
Ni lazima uwe jasiri kuua ndoto za wengine juu yako ili kuruhusu ndoto kubwa ulizonazo ndani yako uweze kuzifikia.

Lawama nyingi utazipata mwanzoni kwa kuwa utakuwa umetikisa maisha ya wengine kwa namna fulani.
Lakini hupaswi kukata tamaa na kurudi nyuma ili kuwafurahisha.
Unapaswa kuendelea na mabadiliko uliyoanzisha, kwa sababu utakapoyapata mafanikio makubwa unayoyapigania, wale waliokuwa wanakulaumu kwa mabadiliko unayofanya watakuwa wa kwanza kukusifia.

Wajibu wako namba moja kwenye maisha yako ni kuijua na kuipambania ndoto kubwa ya maisha yako.
Ndoto nyingine zote ambazo watu wanazo juu yako unapaswa kuziua kwa kuzipuuza.
Hilo haitakuwa rahisi, litaleta kila aina ya ugomvi na lawama.
Hayo yasikutetereshe hata kidogo.
Kuwa imara ili uweze kusimamia na kuzifikia ndoto zako kubwa na hapo utakuwa na fursa ya kuwa na manufaa kwa wengi zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe