3033; Wasiwe na pengine pa kwenda.

Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio makubwa unayoyataka kwenye maisha yako, yatatokana na watu.
Unahitaji sana watu ili kuweza kufikia ndoto kubwa ulizonazo.
Na kadiri ndoto zako zinavyokuwa kubwa, ndivyo unavyowahitaji watu wengi na kwa muda mrefu.

Lakini changamoto moja kubwa kwenye watu ni huwa hawaeleweki. Unaweza kuwapata watu na kuwapa kile wanachotaka, lakini bado wakakuacha na kwenda kwa wengine.
Hilo huwa linakatisha tamaa na kuona watu hawawezi kuaminika.

Kabla hatujaangalia ni kwa namna gani unaweza kuwafanya watu wakae na wewe kwa muda mrefu, tuangalie kwanza aina ya watu unaowahitaji kwenye safari yako ya mafanikio.

Kuna aina kubwa tatu za watu unaowahitaji kwenye safari yako ya mafanikio.
Moja ni watu wa kushirikiana nao, hawa ni wale wanaokuunga mkono kwenye kile unachofanya. Mfano watu wanaokuwa tayari kuwekeza kwenye biashara yako.
Mbili ni wafanyakazi ambao wanatekeleza majukumu yote muhimu kwenye biashara yako.
Na tatu ni wateja ambao wananunua kile mnachouza kwenye biashara yako.

Unahitaji sana watu bora kwenye maeneo yote matatu ili uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Lakini kama ambavyo tumeshaona, mara nyingi watu huwa hawakai.
Unaweza kuwapata hao bora, lakini baada ya muda wanakuacha na kwenda kwingine.

Swali ni unawezaje kuwafanya watu bora wabaki na wewe kwa muda mrefu ili uweze kupata mafanikio makubwa?

Jibu ni moja, wafanye wasiwe na pengine pa kwenda.
Wape vitu ambavyo hawawezi kuvipata mahali pengine popote isipokuwa kwako.
Kwa washirika wape manufaa ambayo hawawezi kuyapata mahali pengine popote.
Kwa wafanyakazi wape mazingira bora ya kufanya kazi ambayo hawawezi kuyapata mahali pengine.
Na kwa wateja wape huduma bora kabisa ambayo hawawezi kuipata mahali pengine popote.

Kikubwa sana ni kuwafanya watu wasiwe na sababu ya kutaka kuondoka kwako na kwenda kwingine.
Hilo litawezekana kama utaondoa mazoea kwenye kila eneo la biashara yako na maisha yako.

Iko hivi, sisi binadamu huwa tunazoea vitu haraka sana.
Wakati tunawatafuta watu, huwa tunawaahidi vitu vingi.
Na wakati tunawashawishi wakubaliane na sisi, huwa tunawapa vitu vizuri ambavyo hawawezi kuvipata mahali pengine.

Cha kushangaza ni wakishakubaliana na sisi, tunaacha kuwapa vitu hivyo vya tofauti na kuleta mazoea.
Tunaweka mazoea ambayo yanawachosha watu na kuwafanya watafute mahali pengine ambapo watapata mambo mapya.

Hivyo ni muhimu sana uvunje kila aina ya mazoea kwa watu unaohitaji kwenda nao kwa muda mrefu.
Kila wakati kuwa na mambo mapya ya kuwavutia kuendelea kuwa na wewe.
Wafanye wakose sababu ya kutaka kwenda mahali pengine.
Na hata ikitokea wameenda pengine, wafanye watake kurudi kwako kwa yale unayokuwa unawapa ambayo hawataweza kwenda kuyapata kwingine.

Na mambo ya kufanya ili watu wabaki na wewe haimaanishi upande wa fedha pekee, japo huo ni muhimu.
Wengi hudhani ili washirika wabaki na wewe, lazima uwape faida kubwa kwenye uwekezaji wao.
Ili wafanyakazi wabaki na wewe, lazima uwalipe mshahara mkubwa.
Na ili wateja wabaki na wewe, lazima uwauzie kwa bei ndogo kuliko wengine.
Ndiyo fedha ina umuhimu sana, lakini siyo peke yake.

Unaweza kuwapa watu faida kubwa na bado wasiwe tayari kushirikiana na wewe.
Unaweza kuwalipa wafanyakazi mshahara mkubwa na bado wakaondoka na kwenda kutafuta kazi pengine.
Na unaweza kuwapa wateja bei ndogo kabisa na bado wakaenda kununua pengine ambapo bei siyo ndogo kama yako.

Unapojihusisha na watu, kitu kikubwa kabisa unachopaswa kufanya ni kuwafanya wajisikie vizuri.
Wafanye wajione wapo sehemu salama na inayowapa nafasi ya kutoa mchango wao kwenye kitu chenye manufaa makubwa.
Hilo huwafanya watu wajivunie kuwa sehemu hiyo kutokana na fursa ya kufanya makubwa wanayoipata.

Kwa washirika wafanye waone kwa kushirikiana na wewe wanapata nafasi ya kuwa sehemu ya mambo makubwa yanayokwenda kufanyika.
Kwa wafanyakazi wafanye waone wanaenda kujenga kitu kinachokweda kufanya makubwa na hivyo kuwa sehemu ya historia.
Na kwa wateja wafanye waone wanakwenda kumiliki kitu ambacho hakipatikani kwa urahisi kila mahali.

Wewe mmiliki na kiongozi wa biashara kama kiungo kikuu cha watu kwenye biashara yako, unahitaji kufanya kazi kubwa na ya ziada ya kuwafanya watu watake kuja kwenye biashara yako na wakishakuja watake kuendelea kubaki.

Utaweza kukamilisha hilo kwa kujenga biashara ambayo ni bora na ya kipekee kabisa, ambayo inatoa fursa zisizoweza kupatikana kwingine.

Ni lazima uwe mbunifu kila wakati na kuchukua hatua za hatari.
Ni lazima uondokane na mazoea na kila wakati kuwa mbele ya wengine, kwa kuona fursa ambazo bado hazijafikiwa na kutumiwa na wengine.

Hayo yote yatawezekana kama utaifanya biashara yako kuwa kipaumbele cha kwanza kwako.
Kama utaweka umakini wako wote kwenye biashara yako, utaona fursa nyingi za kuifanya kuwa biashara bora kabisa kuwahi kutokea na kuwavutia watu bora kuja na kubaki.
Haya yote yanahitaji sana kazi kwa upande wako.
Kazi ambayo haina mwisho wala mapumziko.

Kazi namba moja kwako kwenye biashara inakuwa ni kupata watu bora na kuwafanya waendelee kubaki kwenye biashara yako.
Hiyo ni kwa washirika, wafanyakazi na wateja.
Ukiweza kutatua eneo la watu, utaweza kujenga biashara kubwa na bora kabisa.

Kuna njia za mkato ambazo watu huwa wanazitumia.
Moja ni ya tamaa, ambapo watu wanapewa kitu cha kuwafanya wasitake kuondoka.
Na mbili ni ya hofu, ambapo watu wanapewa mikataba ambayo hawapaswi kuivunja.
Njia hizi zinaweza kuwafanya watu waendelee kuwepo, lakini siyo wale bora.
Kwani walio bora wanaweza kupata tamaa kubwa zaidi pengine na kuvunja mkataba wowote unaoweza kuwa umewapa, kwani hata gharama za kuvunja mkataba huo zitakuwa tayari kulipwa na wengine wanaowataka.

Wafanye watu bora waje na kukaa kwenye biashara yako kwa muda mrefu kwa kuwapa fursa ya kuwa sehemu ya kujenga historia kubwa kwenye maisha yao.
Jenga biashara bora na ya kipekee kabisa, ambayo inawapa watu fursa nyingi ambazo hawawezi kuzipata mahali pengine.
Na kila wakati endelea kuwa bora na kubadilika ili kuondoa mazoea ambayo huwa yanawachosha watu.

Watu bora hawapatikani kirahisi na kuwatunza inahitajika kazi.
Kuwa tayari kuweka kazi hiyo ili uweze kujenga biashara kubwa na yenye mafanikio.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe