Misingi Mikuu Kumi Ya Falsafa Ya Ustoa.

Ustoa ni falsafa ya vitendo iliyoanzia Ugiriki ya kale na baadaye kuhamia Roma ya kale.
Falsafa hii ilianzishwa na Zeno ambaye alikuwa mfanyabiashara na kwenye moja ya safari zake za kibiashara meli yake iliharibika na kupata hasara kubwa.

Ni katika kutafuta namna ya kujiliwaza kutokana na hasara hiyo ndipo aliingia eneo lililokuwa na maandiko ya wanafalsafa mbalimbali waliokuwa wametangulia kama Socrates.
Zeno alivutiwa na baadhi ya misingi ya kifalsafa aliyokuwa anajifunza hivyo akawa anakutana na baadhi ya watu kujadili misingi hiyo.
Mikutano yao ilikuwa inafanyika chini ya mti ulioitwa Stoa na hapo ndipo jina la Wastoa lilipopatikana.

Falsafa hii ilikubalika na kupendwa na wengi kwa sababu ilikuwa falsafa ya vitendo ya kuwawezesha watu kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha huku wakibaki imara bila kutetereka.
Walioielewa falsafa hii waliweza kusimamia kile walichoamini bila ya kuvurugwa na chochote.

Falsafa ya Ustoa imekuwa na wanafalsafa wengi mashuhuri, lakini kuna wachache ambao wanakumbukwa sana mpaka leo kutokana na misimamo yao na kazi za kifalsafa walizoziacha.
Baadhi ya wanafalsafa hao ni kama;

1. Cato; huyu alikuwa mwanaharakati aliyepinga utawala wa kimabavu wa Julius Caesar na kuwa tayari kufa kuliko kukubaliana na kisichokuwa sahihi. Moja ya matukio muhimu yanayokumbukwa kuhusu yeye ni siku moja akiwa amekaa njiani kumpinga, Caesar alikuja kwake na kumwambia amwombe chochote anachotaka kwani ana nyuvu ya kumpa. Caesar alidhani Cato angemwomba amsamehe ili awe na maisha mazuri, lakini Cato akamwambia; naomba usogee, kwani unaniziba nisipate jua.

2. Seneca; huyu alikuwa mwandishi, mfanyabiashara na mshauri wa viongozi wa Roma. Alikuwa mmoja wa watu matajiri sana kwa kipindi hicho. Lakini kutokana na misimamo yake ya kifalsafa alifukuzwa Roma mara mbili na mwisho akalazimisha kujiua na Mtawala Nero, ambaye alikuwa mwanafunzi wake. Seneca alikuwa tayari kujiua kwa kusimamia misingi ya Ustoa. Wakati anajiua, watu wake wa karibu walikuwa wanasikitishwa, yeye akawa anawatia moyo.

3. Epictetus; huyu alizaliwa kama mtumwa na enzi za Roma ya kale watumwa hawakuwa wanahesabiwa kama watu kamili. Waliteswa na kunyanyaswa, huku wakiuzwa kama bidhaa. Kupitia kujifunza na kufundisha falsafa ya Ustoa, Epictetus aliweza kununua uhuru wake. Lakini pia aliweza kuwa mshauri wa viongozi mbalimbali. Akiwa mtumwa, siku moja aliyemmiliki alimpiga na kumvunja mguu, Epictetus alicheka na kumwambia; unaona, nilikuambia ukiupiga mguu utaumia. Alibaki na kilema cha maisha, lakini hakikumuumiza kwa sababu ya kuielewa na kuiishi falsafa ya Ustoa.

4. Marcus Aurelius; huyu alikuwa mtawala wa Roma, akihesabiwa kama mmoja wa watawala bora wa mwisho wa Roma. Marcus alipokea utawala akiwa bado ni kijana mdogo na asiye na uzoefu, lakini falsafa ya Ustoa ilimsaidia sana kuwa kiongozi bora. Kipindi cha uongozi wake Roma ilikumbwa na changamoto nyingi ikiwepo vita na mlipuko wa ugonjwa wa tauni. Aliweza kuyakabili hayo yote akiwa imara kwa kuiishi misingi ya Ustoa. Pamoja na kuwa kiongozi mkubwa, kila siku Marcus aliandika mawazo yake kwenye kijitabu cha siri kwake. Hakuyaandika ili yaje kusomwa na mtu, bali aliyaandika kwa ajili ya utulivu wake wa nafsi. Baada ya kufariki kwake maandiko hayo yalipatikana na yamekuwa moja ya vitabu bora kabisa vya falsafa. Maandiko hayo yanaitwa Meditations na yamekuwa msingi muhimu wa viongozi wa kale na sasa.

Kupitia Wastoa hao wachache wa kale, tunaona jinsi falsafa ya Ustoa ilivyo ya watu wengi na inavyowafanya kuwa imara.

Kwenye zama hizi falsafa hii ya Ustoa imepata sana umaarufu kwa viongozi, wanajeshi, wachezaji na wajasiriamali wakubwa.
Hiyo ni kwa sababu tasnia hizo zina msongo mkubwa na falsafa ya Ustoa ina njia bora za kukabiliana na msongo wa kila aina.

Hapa tunakwenda kujifunza misingi mikuu 10 ya Ustoa ambayo mtu yeyote akiifuata ataweza kuwa na maisha bora na kukabiliana na chochote.

1. ISHI KULINGANA NA ASILI.

Lengo kuu la falsafa ya Ustoa ni kuishi kwa kuendana na kukubaliana na asili.
Kuishi kulingana na asili inamaanisha kuielewa asili yetu binadamu na kuishi kama binadamu.

Kinachotutofautisha sisi binadamu na wanyama wengine ni uwezo wetu mkubwa wa kufikiri. Wanyama wengine wote wanaendeshwa kwa hisia na machale, lakini sisi binadamu tuna akili inayoweza kuhoji, kufikiri na kufanya maamuzi.

Japo maamuzi yetu mengi wanadamu yanachochewa na hisia, tunapaswa kutumia fikra zetu kufanya maamuzi ya kimantiki.

Hivyo falsafa ya Ustoa inatutaka kutumia akili zetu kufikiri na kufanya maamuzi sahihi badala tu ya kuendeshwa na hisia kama walivyo wanyama wengine.

Kwa kila jambo unalofanya, tumia akili yako kufikiri kwa kina na kufanya maamuzi badala ya kukubali kusukumwa tu na hisia. Makosa mengi tunayofanya kwenye maisha huwa yanaanzia kwenye maamuzi tunayofanya kwa hisia bila kutumia akili kufikiri kwa kina.

2. ISHI KWA MAADILI.

Falsafa ya Ustoa ina maadili makuu manne ambayo kila mtu anapaswa kuyazingatia katika kuyaishi maisha yake.
Anayeweza kuyaishi maadili hayo kwa ukamilifu ndiye anayekuwa na maisha bora na tulivu, bila kujali anapitia nini.
Maadili hayo manne ni kama ifuatavyo;

а. Hekima au Akili;
Hii inahusisha kutumia akili, fikra, mtazamo na uelewa katika kufanya maamuzi bora.

b. Haki au Usawa;
Hii inahusisha kuwa mwema, kujali na kuwatendewa watu kwa usawa bila upendeleo.

с. Ujasiri au Ushujaa;
Hii inahusisha kujiamini, ung’ang’anizi, uaminifu na uhalisia.

d. Nidhamu au Kiasi;
Hii inahusisha kuwa na mipango, kujidhibiti, unyenyekevu na kusamehe.

Kwenye falsafa ya Ustoa, maisha mazuri ni kuishi kwa kuzingatia maadili hayo. Na maisha mabaya ni kupuuza maadili hayo.

Ili uwe na maisha bora, ishi kwa maadili hayo manne ya Ustoa.

3. HANGAIKA NA UNAYOWEZA KUYADHIBITI, KUBALI USIYOWEZA KUYADHIBITI.

Kuna mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu wa kuyadhibiti na kuna ambayo yapo nje ya uwezo wetu.
Tunapaswa kujihangaisha na yale tunayoweza kuyadhibiti, huku tukipokea na kukubali yale yaliyo nje ya uwezo wetu kudhibiti.

Watu wengi wamevurugwa kwenye maisha kwa sababu wanasumbuka na mambo ambayo yapo nje ya uwezo wao, ambayo hawawezi kuyadhibiti.
Kabla hujaruhusu jambo lolote likuvuruge jiulize kama lipo ndani ya uwezo wako wa kulidhibiti au nje ya uwezo wako.

Kama mvua inanyesha na wewe hukutaka mvua, huna namna ya kubadili, hivyo kuhangaika na hilo hakutakusaidia.

Tunavyoweza kudhibiti ni vile vinavyoanzia ndani yetu, kwenye fikra na matendo yetu.
Chochote nje yetu hakipo ndani ya udhibiti wengine.

Mfano watu wengine wanakuchukuliaje, hilo ni jambo ambalo halipaswi kukusumbua kwa sababu lipo nje kabisa ya uwezo wako.
Unapaswa kuyaishi maisha yako na kuwaacha watu wawe na fikra walizochagua kuwa nazo juu yako.

4. TOFAUTISHA WEMA, UBAYA NA ISIYOJALI.

Vitu vyote kwenye maisha vimegawanyika kwenye makundi matatu, wema, ubaya na isiyo na tofauti, yaani siyo njema wala mbaya.

Wema unatokana na maadili makuu manne ya Ustoa ambayo ni Hekima, Haki, Ujasiri na Nidhamu.
Ili kuwa mwema unapaswa kuyaishi maadili hayo.

Ubaya unatokana na kwenda kinyume na maadili hayo manne ya Ustoa, ambapo ni Upumbavu, Udhalimu, Woga na Tamaa mbaya.
Unapoenda kinyume na maadili makuu ya Ustoa unakuwa mwovu.

Isiyojali ni mambo ambayo siyo mema wala mabaya. Haya ni mazuri mtu akiwa nayo lakini hata asipokuwa nayo bado maisha yake hayapaswi kuathiriwa.
Kwenye falsafa ya Ustoa, isiyojali ni yote yaliyo kati ya wema na ubaya, kama; maisha, kifo, umaarufu, raha, maumivu, afya, maradhi, utajiri, umasikini na mengine.

Unajionea hapo kwa nini Ustoa unaweza kumpa mtu utulivu, kwa sababu vitu vinavyowahangaisha wengi kwenye maisha kama afya, utajiri, umaarufu na raha kwa Wastoa siyo vitu ambavyo vinawahangaisha sana. Wanapambana kuwa navyo, lakini hata wakivikosa maisha yao hayatetereki.
Mstoa akishakuwa na Hekima, Haki, Ujasiri na Nidhamu, maisha ni mazuri kwake bila ya kujali kipi kingine anacho au amekosa.

5. CHUKUA HATUA.

Falsafa nyingi huwa ni za mijadala isiyokuwa na ukomo. Maswali kama nini maana ya maisha, nini kinatokea baada ya kifo na mengine, yamekuwa na mijadala mikali kwa wanafalsafa.

Lakini falsafa ya Ustoa siyo ya mijadala ya aina hiyo, bali ni falsafa ya kuchukua hatua na kuwa na maisha bora.

Na kuchukua hatua kwenye ustoa ni kuishi kulingana na maadili makuu manne ambayo ni Hekima, Haki, Ujasiri na Nidhamu.
Yaweke maadili hayo kwenye vitendo na utaweza kuwa na maisha bora sana.

6. IGIZA UMEKUMBWA NA MABAYA.

Kwenye maisha, huwa watu wanapitia mabaya mbalimbali. Haya yamekuwa chanzo cha maisha ya wengi kuvurugika.
Kinachofanya mabaya yaharibu maisha ya wengi ni kukosekana kwa maandalizi ya mabaya hayo.
Wakati mambo yanaenda vizuri, watu huwa wanajisahau na kudhani yataenda hivyo milele.
Ni pale mabaya yanapojitokeza ghafla ndipo maisha hubadilika na kuvurugika.

Kuepuka hilo, Wastoa wamekuwa wakijiandaa kwa mabaya kwa kuyaigiza. Hapa wanayaishi maisha kama vile wanapitia mambo mabaya. Hilo linawafanya kuwa imara hata pale mabaya yanapotokea, yanakuwa hayawashangazi, kwani ni kitu walichokitegemea.

Kama ambavyo mwili hujengewa kinga pale unapopata magonjwa, ndivyo pia maisha yanajengewa kinga pale unapoigiza umekumbwa na mabaya.

Hakuna kitu chochote kinachoweza kutokea kwa Mstoa kikamshangaza au kumuumiza. Hiyo ni kwa sababu alishafikiria na kuigiza kila kibaya kinachoweza kutokea.

Hili ni zoezi muhimu la kila mtu kufanya. Mara kwa mara jichukulie umepoteza kila kitu na kila mtu uliyenaye kwenye maisha yako, kisha yaishi maisha yako kama ndiyo unaanza upya kabisa.
Pale inapotokea umepoteza chochote, huumizwi, kwa sababu ni kitu ambacho umeshaweza kuiishi mara kwa mara.

7. FANYA SEHEMU YAKO.

Kuna vitu unavyokuwa unataka kupata kwenye maisha yako.
Na ukachukua hatua za kuhakikisha unavipata.
Lakini pamoja na kuchukua hatua hizo, bado matokeo hayapo kwenye udhibiti wako.

Badala ya kuumia pale unapochukua hatua na usipate matokeo uliyotegemea, wewe furahia kwa kukamilisha sehemu yako.

Ukishafanya kile kilicho ndani ya udhibiti wako, kuwa tayari kupokea matokeo yoyote yanayokuja bila kuumizwa nayo.
Kwa kuendelea kufanya yaliyo ndani ya uwezo wako, matokeo mazuri yatakuja kwa wakati wake.

8. IPENDE ASILI (AMOR FATI)

Kuna mambo yanaweza kutokea kwa namna ambayo hukutegemea yatokee.
Wengi huumizwa na kuvurugwa na yale yanayokuwa yametokea, hasa wanapoyaona ni mabaya.

Kwa Wastoa, hakuna chochote cha nje ambacho ni kibaya, hivyo siyo tu wanapokea kila kinachowatokea, bali pia wanakipenda.
Kwa sababu wanaamini kila kitu kinatokea kwa sababu.
Na wataweza kukitumia vizuri kile kinachotokea kama watakipenda.

Hata wakutane na kitu kinachoonekana kibaya kiasi gani, Wastoa huwa wanakikubali na kukipenda na kisha kujiuliza wanawezaje kukitumia kupiga hatua zaidi.

Hivyo ndivyo unavyopaswa kuyaendesha maisha yako, penda kila kinachotokea kwako na kitumie kuwa bora zaidi.
Kumbuka wema ni Hekima, Haki, Ujasiri na Nidhamu.
Na unaya ni Upumbavu, Udhalimu, Woga na Tamaa mbaya.
Mengine yote ni ya kuyapokea na kuyapenda kama yanavyokuja kwako na kuyatumia kwa ubora.

9. GEUZA VIKWAZO KUWA FURSA.

Mtazamo sahihi wa Kistoa ni kwamba vikwazo unavyokutana navyo ndiyo fursa kubwa kwako. Kile kinachozuia njia kinakuwa ndiyo njia yenyewe.

Huwa hatuyaoni mambo kama yalivyo, bali huwa tunayaona jinsi tulivyo sisi wenyewe.
Hivyo kwa kujijengea mtazamo sahihi wa kutafuta fursa kwenye kila kikwazo, tutaweza kuona na kutumia fursa nyingi zaidi.

Kwa kila kikwazo unachokutana nacho, jiulize ni fursa gani iko nyuma yake na kuwa tayari kuifanyia kazi, utaweza kufanya makubwa sana.

10. KUWA NA UWEPO WA KIAKILI.

Ili kuweza kuiishi falsafa yoyote ile kwa ukamilifu, lazima uwe na uwepo wa kiakili.
Hii inamaanisha kuweka umakini wako wote kwenye kile fikra zako na matendo yako.
Kadiri unavyokuwa na umakini wa kifikra, ndivyo unavyoelewa kwa kina na kuweza kufanya maamuzi ambayo ni sahihi.

Eneo muhimu la kuwa na umakini ni kwenye fikra na hisia. Unapaswa kufikiri kuhusu fikra unazokuwa nazo, hapo utaweza kuzielewa kwa kina na kufanya maamuzi sahihi.
Lakini pia unapaswa kuweka umakini wako kwenye hisia unazokuwa nazo, kujua chanzo chake na kuona nguvu ya hisia hizo ndani yako, hiyo inakuzuia usifanye maamuzi mabovu.

Kwa mfano pale unapokuwa na fikra hasi kuhusu jambo fulani, unapaswa kutambua kwamba una fikra hasi na kujua chanzo chake.
Kadhalika unapokuwa na hisia fulani, ziwe ni chanya (kama furaha) au hasi (kama huzuni) unapaswa kujijua una hisia hizo na kujua chanzo chake.
Kwa kuwa na umakini wa hali hii, itakuwezesha kufanya maamuzi ambayo ni bora na sahihi kwako.

Hii ndiyo misingi mikuu kumi ya falsafa ya Ustoa ambayo ukiweza kuielewa na kuiishi utaweza kuwa na maisha bora na yenye utulivu mkubwa.

Karibu tuendelee kujifunza na kuiishi misingi hii ili kujenga maisha bora.

Kocha.