3034; Fanya kwa ajili yako.

Rafiki yangu mpendwa,
Huenda umewahi kutumia muda na nguvu zako kufanya kitu kwa ajili ya wengine.
Ukitegemea kwamba watakushukuru kwa namna ulivyojitoa.
Au watakulipa fadhila kwa uliyowafanyia.

Lakini matokeo yanakuwa ni tofauti kabisa.
Watu unaokuwa umejitoa kufanya vitu kwa ajili yao hawajali kabisa.
Hawakushukuru kwa namna ulivyojitoa.
Lakini pia hata pale unapokuwa na shida fulani na kuwaomba wakusaidie, wanashindwa kufanya hivyo.

Hali kama hizi zinakatisha tamaa na wakati mwingine kuona haina haja ya kujisumbua kuwasaidia wengine.

Lakini hupaswi kufikia hatua hiyo kwenye maisha yako.
Chochote unachoamua kufanya kwenye maisha yako, anza kukifanya kwa ajili yako mwenyewe.

Fanya kitu kwa sababu inakufanya ujisikie vizuri kwa kukifanya.
Na pia fanya kitu kwa sababu inakupa fursa ya kuonyesha thamani uliyonayo.

Kufanya kitu chochote kwa kutegemea uliowafanyia wakushukuru au kukulipa fadhila ni kujiandaa kuumizwa.

Ubinafsi ni asili yetu binadamu.
Kinachowafanya watu wasijali unayofanya kwa ajili yao na wala kulipa fadhila ni ubinafsi wanaokuwa nao.

Hivyo na wewe pia tumia ubinafsi kwenye yale unayofanya, ila kwa namna ambayo ni bora.
Tumia ubinafsi kwa kufanya kitu kwa ajili ya wengine, lakini kwa sababu inakufanya wewe ujisikie vizuri.
Pia tumia ubinafsi kwenye kufanya kitu kwa ajili ya wengine, lakini kwa sababu inakupa fursa ya kuonyesha thamani unayoweza kutoa.

Fanya kwa sababu unataka kufanya na siyo kwa sababu unategemea unaowafanyia wakushukuru au kukulipa fadhila.

Usijiwekee mategemeo yasiyo halisi, chochote unachofanya kifanye kwa sababu zako za ndani na siyo sababu za nje.

Kila unachofanya, angalia kinakusogezaje karibu zaidi na malengo makubwa uliyonayo kwenye maisha yako.
Kama hakina mchango, achana nacho.

Kama unafanya kitu chochote ili upendwe na watu unajiandaa kuumizwa na kukatishwa tamaa.
Watu huwa hawatabiriki.
Wale wale wanaokusifu na kukubali leo, ndiyo watakaokuponda na kukukataa kesho.

Chochote unachofanya, fanya kwa sababu ni fursa ya kuonyesha thamani kubwa unayoweza kutoa na fursa ya kusogea zaidi kwenye malengo makubwa unayokuwa nayo.

Manufaa makubwa unayopaswa kuyategemea kwenye chochote unachofanya yanapaswa kuwa ni kitendo cha kufanya kitu hicho.
Hiyo pekee inapaswa kuwa ndiyo sababu kuu ya wewe kufanya.

Hata pale unaposema unafanya kwa ajili ya kuwasaidia wengine, hakikisha unafanya kwa sababu inakusaidia na wewe mwenyewe pia.

Chochote unachofanya ambacho hakina manufaa ya moja kwa moja kwako kitakuumiza.
Kama unajitoa kafara kwa ajili ya wengine, itakuumiza sana pale unapokuja kugundua wengine hao hawajali sana kile ulichofanya kwa ajili yao kama ulivyotegemea wajali.

Lakini kama umejitoa kafara kwa ajili ya kufikia hatua fulani, kuifikia hatua hiyo kutakuwa na manufaa makubwa kwako bila kujali wengine wanachukuliaje.

Hili ni jambo muhimu sana la kutafakari kwa kina na kuelewa kwenye hii safari kubwa ya mafanikio tuliyopo.
Maana usipokuwa na vipaumbele sahihi kwako, utaishia kufanya mengi yasiyokuwa na tija kwako.

Na mwisho kabisa, inapokuja upande wa kazi au biashara, mara zote hakikisha unalipwa kile unachostahili kulipwa.
Usijidanganye kwamba unatoa msaada kwa kuwafanyia watu kitu bila kulipa, inashusha thamani yako na kutokukulipa kwa namna yoyote ile.

Kuna njia nyingi za kuwasaidia watu wengine, lakini inapokuja kwenye kazi au biashara yako, hakikisha kila mtu analipa kila anachopaswa kulipa.

Utagundua, wale ambao hawakulipi kwa namna wanavyopaswa kulipa ndiyo ambao wanaishia kukusumbua sana kwa kutokujali na kukosa shukrani.
Ndiyo ambao pamoja na mengi unayokuwa umeyafanya bado wataona hujafanya chochote.
Kwa sababu hawajaingia gharama yoyote, wanakuwa hawathamini sana.

Mtake kila mtu alipie kwenye kazi na biashara yako ili aweze kuielewa thamani unayompa.
Na kama unataka kuwasaidia watu, fanya hivyo nje ya kazi na biashara yako.

Nikupe mfano mzuri ambao utakuamsha sana.
Makampuni yanayotengeneza bidhaa za kifahari, huwa yanakuwa na bidhaa zenye makosa madogo madogo ambazo hawawezi kuzipeleka kwa wateja.
Zinakuwa ni bidhaa zinazoweza kutumika vizuri tu, ila kwa makosa madogo yanayokuwepo, wanakuwa hawataki kubaribu majina yao.

Unajua huwa wanazifanyia nini bidhaa hizo ambazo zina makosa? Huwa wanaziharibu kabisa.
Kumekuwa na kilio cha wengi kwamba makampuni hayo yawe yanagawa bidhaa hizo kwa masikini wasiojiweza kama sehemu ya kusaidia.
Lakini makampuni hayo huwa yapo radhi kutoa misaada kwa kutumia faida wanayoingiza kwenye mauzo yao kuliko kwa kutoa bure bidhaa zao.
Kuna somo kubwa sana hapo la kutunza thamani ya kile unachozalisha.
Ukikigawa hovyo unashusha thamani yake na kuharibu soko lake.

Chochote unachofanya, fanya kwa ajili yako, fanya kimkakati ili kufika kule unakotaka kufika.
Hakuna anayejali kuhusu malengo yako kuliko wewe mwenyewe.
Yape hayo kipaumbele kikubwa kwenye kila kitu unachopanga kufanya.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe