3036; Ndiyo ni Hapana kubwa.

Rafiki yangu mpendwa,
Wakati tupo kwenye msimu wa HAPANA, tukumbushane jambo muhimu sana kuhusu NDIYO na HAPANA.

Unaposema HAPANA kwenye kitu kimoja, unakuwa umekikataa kitu hicho kimoja tu.
Hilo linakupa fursa ya kuweza kuangalia mambo mengine mazuri yanayoendana na kile unachofanya na kuweza kuyasemea NDIYO.
Kwa maana hiyo basi, kusema HAPANA kunakuacha ukiwa huru zaidi.

Unaposema NDIYO kwenye kitu kimoja, unakuwa umekikubali kitu hicho kimoja, lakini pia unakuwa umevikataa vitu vingine vingi zaidi.
Kwa kusema NDIYO unakuwa umezikataa fursa nyingine nzuri zaidi zinazoendana na kile unachofanya.
Kwa kuwa muda unaoweka kwenye kile ulichosemea NDIYO, ni muda ambao huwezi kuupeleka kwenye kitu kingine.
Kwa maana hiyo basi, kusema NDIYO ni sawa na kusema HAPANA kubwa.

Utakuwa salama zaidi kwa kutumia HAPANA kuliko ndiyo.
Kwa sababu hata ukikosea, kwenye hapana una nafasi ya kujirekebisha, maana unakuwa umekataa kimoja tu, unaweza kusema ndiyo kwenye kingine.
Lakini ukikosea kwenye NDIYO, unakuwa umefunga milango mingi, huwezi kufanya mengine kwenye kipindi hicho kimoja.

Kuwa makini sana na matumizi yako ya NDIYO na HAPANA.
Ni bora utumie hapana zaidi kuliko ndiyo.

Nasisitiza sana hili kwa sababu kuna watu wengi huwa wanahofia kusema HAPANA kwa kuona watakosa fursa nzuri.
Mwishowe wanajikuta wamenasa kwenye fursa mbovu na kukosa fursa nzuri zaidi zinazokuwa zimekuja.

Richard Branson amewahi kusema fursa ni kama daladala, ukikosa moja, kuna nyingine inakuja.
Na mimi naongeza kwa kusema, ni bora ukose daladala moja, kuliko uipande wakati haiendi kule unakotaka kwenda.
Kwani nauli uliyonayo ni ya safari hiyo moja tu, ukishaitoa hutaweza tena kupata daladala nyingine.

Ni bora useme HAPANA kwenye fursa usiyokuwa na uhakika nayo na uikose hata kama umekosea, kuliko useme NDIYO na uipate na iwe siyo sahihi kwako.
Kwa kusema NDIYO kwa fursa moja isiyo sahihi, unakuwa umesema HAPANA kwa fursa nyingi sahihi kwako.

Ni muhimu sana kuzijua rasilimali tulizonazo kwa uhaba na kuzilinda sana.
Muda, nguvu na umakini wetu, ni vitu ambavyo hupaswi kukosea kuvitoa au kuviwekeza kwenye kitu.
Ndiyo unaweza kuja kukataa chochote baadaye, lakini utakuwa umejiingiza kwenye migongano isiyokuwa na tija.
Maana kusema NDIYO halafu baadaye uje useme HAPANA kwa kitu ambacho tayari ulishakikubali kunafanya watu wakuone mbabaishaji na usiyeaminika.

Watu watakuamini na kukuheshimu kwa kusema HAPANA tangu awali kuliko ukianza kwa kusema NDIYO halafu ukaja kusema HAPANA.
Unapowaambia watu hapana tangu awali wataumia, lakini unakuwa hujawapotezea muda kwa kuwapa matumaini yasiyo sahihi.
Hilo litawafanya wakuheshimu.

Lakini ukiwaambia watu NDIYO, kwanza unakuwa umewapa matumaini na wanaweka mategemeo makubwa kwako.
Unapokuja kugeuka na kusema HAPANA, unavunja matumaini na mategemeo wanayokuwa wameweka kwako.
Hilo siyo tu litawachukiza, bali pia litawafanya wakudharau na kutokukuamini. Wakati mwingine hawatakuwa na imani na mambo unayoahidi, hata kama unayamaanisha kweli.

Sema HAPANA zaidi ya unavyosema NDIYO.
Ni salama kukosea kwenye HAPANA kuliko kukosea kwenye NDIYO.
Linda sana rasilimali zako muhimu zisipotee hovyo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe