3042; Ipende kazi.

Rafiki yangu mpendwa,
Tunaishi kwenye zama ambazo kila mtu anatafuta njia ya mkato na ya haraka ya kufanikiwa isiyohusisha ufanyaji wa kazi.

Kazi imekuwa inachukuliwa kama kitu cha mateso na kinachofanywa na wale wasiojielewa.
Lakini licha ya watu kutafuta njia za kukwepa kazi, hakuna ambaye amewahi kufanikiwa bila kuipenda kazi na kuwa tayari kuweka juhudi kwenye kazi kwa muda mrefu.

Ukweli ni kwamba, mafanikio na kazi ni mapacha ambao hawawezi kutenganishwa.
Inapokuja kwenye mafanikio, siyo tu kazi ni muhimu, bali ni hitaji la msingi.
Hakuna mafanikio makubwa yanayoweza kupatikana bila kazi ya uhakika kuwekwa.

Ni lazima uweke kazi ndiyo uweze kupata kitu chochote unachotaka.
Japo kazi unayopaswa kuweka inaweza kuwa ngumu na ya kuchosha, bado ni kitu cha lazima kufanya, hakuna namna unaweza kukwepa kazi.

Kazi ni muhimu sana kwenye mafanikio yako, iwe unapenda kuweka kazi au hupendi.
Na kama ilivyo kwenye mambo yote ya maisha, ili kupata chochote tunachotaka, lazima tuwe tayari kufanya kila kinachopaswa kufanyika.

Sasa kwa kuwa kazi ni lazima ifanyike, haina maana yoyote kutokuipenda, kwa sababu huna namna ya kuiepuka.
Kwa kuwa ni kitu cha lazima kwako kufanya ili upate unachotaka, ni vyema ukachagua kuipenda kazi.

Hapo kwenye kuchagua kuipenda kazi ndiyo panaweza kuonekana pagumu, kwa sababu ya jinsi kazi zimekuwa zinaumiza na kuchosha.
Lakini ni jambo linalowezekana kama tutachagua kubadili mtazamo tulionao juu ya kazi.

Kila mtu anapaswa kuipenda sana kazi, kwa sababu kazi ina manufaa mengi sana kwa kila mtu.

Ni kupitia kazi ndiyo unaweza kujua ukomo ambao umejiwekea na kuweza kwenda zaidi ya hapo. Unajiona jinsi ulivyo na uwezo wa kufanya makubwa kuliko ulivyozoea.

Kupitia kazi unapata fursa ya kufungua ubunifu mkubwa ulio ndani yako kutokana na kutafuta suluhisho la matatizo yanayokuwa yanakukabili kwenye safari yako ya mafanikio.

Kuipenda kazi kunajenga mtazamo chanya ambao unasambaa kwa wale wote unaokuwa unashirikiana nao, kitu kinachowafanya nao wawe tayari kujifunza zaidi. Unapokipenda kitu, unakuwa na shauku kubwa nacho na shauku ni rahisi kuambukiswa.

Na la muhimu kabisa la kukumbuka mara zote ili uweze kupenda na kuzingatia kazi ni mafanikio siyo tu sisi tumepata nini, bali pia tumetoa nini kwa ajili ya wengine.
Ni kupitia kazi ndiyo unakuwa na mchango bora kwenye maisha ya wengine, kuyafanya maisha yao kuwa bora zaidi.
Kadiri unavyoyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi, ndivyo pia maisha yako yanakuwa bora. Kwa sababu hiyo, kazi haikwepeki.

Kuna watu wanadhani wakishapata mafanikio, hawahitaji tena kuweka juhudi kwenye kazi.
Na wale wanaoenda na mtazamo huo ndiyo huwa wanapata anguko kubwa baada ya mafanikio.
Hiyo ni kwa sababu wakati wanapokuwa wanaanza wanakuwa wanajituma sana kwenye kazi, kitu kinachowajengea mafanikio ya wastani.
Wakishapata mafanikio hayo, wanajiona hawastahili tena kuteseka na kazi, hivyo wanapunguza juhudi walizokuwa wanaweka kwenye kazi.
Matokeo yake ndiyo yanakuwa anguko ambalo wengi wenye mtazamo wa aina hiyo huwa wanalifikia.

Kujenga mafanikio kazi inahitajika sana,
Na kuendelea kubaki kwenye mafanikio hayo lazima kuwe na uendelevu kwenye kazi.
Kwa kuwa hakuna kipindi ambacho kazi haitahitajika kwenye maisha yako, ni bora tu uchague kuipenda na uipende kweli kutoka moyoni.
Chuki na dharau yoyote utakayokuwa nayo kwenye kazi, itakuwa kikwazo kikubwa kwako kufanikiwa kwenye maisha yako.

Kuipenda kazi kutakutofautisha sana na kundi kubwa la watu wanaopoteza nguvu na muda kutafuta njia za mkato zisizohusisha kazi.

Huhitaji hata kuigiza kuipenda kazi yoyote unayoifanya.
Unachohitaji ni kuwaangalia wale ambao wananufaika moja kwa moja na kile unachofanya.
Utajionea mwenyewe jinsi ambavyo maisha ya wengine yanakuwa bora sana kupitia unachofanya.

Unapoacha kuangalia kazi kama mateso kwa upande wako na kuanza kuiangalia jinsi inavyokuwa baraka kwa wengine, huwezi kukosa sababu za kuipenda kazi yako.
Kwa kifupi ni kama huipendi kazi unayoifanya basi wewe ni mbinafsi, unajijali wewe tu na huwajali wengine.
Huwezi kupata mafanikio makubwa kwa kujijali wewe mwenyewe tu.

Kazi ni kitu kizuri,
Kazi ni kitu muhimu,
Kazi ni kitu cha kupendwa na kila mtu.
Na kufanya kazi kwa juhudi kubwa ni jambo la hekima sana kwenye maisha yetu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe