Rafiki yangu mstoa, wiki iliyopita tulijifunza jinsi ya kukabiliana na magumu na tuliona kwamba magumu ni sehemu ya maisha.

Na magumu hayo huwa yanatuumiza sana pale hatuyategemei kwani huwa yanatokea kwa mshtukizo kama vile ajali, kitu ambacho huwa kinatuumiza sana.

Ili kuondokana na hali hiyo, wastoa walikuwa wanajiandaa na zoezi la kukabiliana na magumu kabla hujayafikia.

Kujiandaa na magumu kabla hujayafikia ndiyo msingi pekee wewe kama mstoa unapaswa kuuishi.

Namna ya kujiandaa na magumu?
Unajipa taswira ya magumu yanayoweza kutokea. Kwa mfano, kama una gari binafsi na umezoea kutembelea kila siku, siku moja unaliacha unatumia usafiri wa umma.
Kama umeajiriwa, igiza kama vile umefukuzwa kazi, siku ikija kutokea haitokuumiza wala kupaya mshtuko.

Kwahiyo namna hiyo, pale magumu yanapotokea yanakuwa siyo kitu kigeni kwako bali kitu ambacho tayari ulishakiona na kukitarajia.

Magumu ambayo ulishayapitia katika picha yanapotokea hayakushangazi na kujikuta huna cha kufanya, bali unakuwa na maandalizi kabisa ya namna ya kuyakabili.

Mfano ukiondokewa na mtu wako wa karibu ghafla itakuuma sana kuliko ukiondokewa na mtu wako wa karibu ambaye ameumwa kwa muda mrefu na afya yake ilizorota.

Mtu anapokuwa anaumwa kwa muda mrefu tunakuwa tumeshapata picha kwamba huenda atakufa, hivyo anapokufa haiwi mshtukizo sana kwetu.

Kwenye kila eneo la maisha yako, pata picha kile unachokipenda, unachokihitaji na kukitegemea kimeondolewa kabisa, hapo utaiandaa akili yako ili pale yanayotokea kweli usiumie sana.

Pia, unapojiandaa na magumu inakufanya uvithamini zaidi vile unavyomiliki na hata watu wako wa karibu utawathamini zaidi wakiwa hai ili hata wakifa usiwe na majuto kwamba waliondoka mapema kwa sababu uliwatumia vizuri wakati wako hai.

Na unapoianza siku yako, tegemea kabisa kwamba utakutana na watu mwenye yabia ambazo zinaweza kukukera. Ukishakuwa na picha hiyo, hata mtu akija kukukera kweli hata huumi, kwani ulitegemea hilo kutokea.

Magumu ni njia ya asili kutupima.
Mwanafalsafa Seneca anaema kama ambavyo dhahabu huwa inaimarishwa kwa kupitishwa kwenye moto, hata
Binadamu huwa tunaimarishwa kwenye magumu.

Kumbe basi, magumu ndiyo njia ya asili ya kutuimarisha na kutupima kama kweli tuko imara kwa ajili ya kuyakabili maisha au la.

Mtu ambaye hajapitia magumu kwenye maisha, hawezi kuwa na furaha kwa sababu hajajua na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yake.

Kwenda na maisha ya furaha tu bila magumu na kuona maisha ni rahisi siku ukija kukutana na magumu, utapata anguko kubwa kwa sababu huna maandalizi.

Kwenye magumu kuna fursa nzuri ndani yake kwa sababu hakuna jambo lolote linalotokea ambalo halina faida kabisa.

Wajibu wako mkubwa kama mstoa ni kujiuliza kwenye kila gumu kuna faida gani ndani yake. Ni fursa gani nzuri ambazo tunaweza kuzitumia kwa manufaa zaidi.

Kumbuka, kadiri ya Seneca, anasema siyo kile kinachotokea bali tunavyovipokea ndivyo vinavyoleta madhara au manufaa kwetu.

Ukiona magumu unayopitia yamekuja kukutesa, utaona mateso kweli. Lakini tukiona magumu yamekuja kutufanya kuwa imara, basi tutakuwa imara zaidi.

Hatua ya kuchukua leo; Kwenye kila ugumu unaopitia kwenye maisha yako, geuza kila ugumu na uwe na manufaa kwenye maisha yako.
Kwenye kila gumu, kuwa na mtazamo chanya na utaona mazuri kwenye kila kinachotokea zaidi.

Rafiki na Mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy