3053; Turudi kwenye misingi.

Rafiki yangu mpendwa,
Iwapo unajenga nyumba ya ghorofa, lakini kila unapojaribu kwenda ngazi za juu zaidi unakwama, hapo inabidi urudi kwenye msingi.
Unapaswa kuangalia msingi mzima ambapo ghorofa hiyo imejengwa na kama utagundua msingi siyo sahihi basi unapaswa kuuboresha kwanza kabla hujaendelea.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kila safari ya mafanikio kwenye maisha yako.
Unaweza kuwa unajua kile unachotaka na ukawa tayari unaweka juhudi ili kukipata.
Lakini licha ya juhudi zote unazoweka, bado inakuwa vigumu kupiga hatua.

Changamoto hii ni kubwa zaidi kwa wale ambao tayari wana timu kwenye biashara zso.
Timu inakuwepo na hatua zote muhimu zinafanyiwa kazi.
Lakini tatizo kubwa linabaki pale pale na hakuna hatua kubwa zinazokuwa zimepigwa.

Na hii inaanzia pale ambapo kiongozi anaona hawezi kufanya yale ambayo wafanyakazi wanayafanya.
Tunaona jukumu letu kuu ni kuwaelekeza yale wanayopaswa kufanya.
Na kweli tunawaelekeza vizuri, lakini inapokuja kwenye kufanya, huwa hawafuati maelekezo tuliyowapa, bali wanaiga yale ambayo unayafanya.

Kwa kifupi unaweza kuongea sana, lakini watakachofanya watu siyo kile unachosema, bali kile unachofanya.
Watu wanakuiga kuliko wanavyokusikiliza.

Hivyo basi, kama juhudi tunazoweka ili kukuza biashara yako hazileti matokeo unayoyataka, ni vyema kuingia ndani na kupambana kuijenga biashara yako.
Ni muhimu urudi kwenye misingi yako yote ambayo uliitumia wakati unaanza na ukaweza kupiga hatua kubwa.

Ni wakati sasa wa kurudi kwa kina ndani ya biashara yako, ufanye kwa vitendo na kuongoza kwa mfano kama ulivyojitoa wakati unaanza.
Kwa kufanya hivyo, timu yako itasukumwa kuwa bora zaidi kupitia yale wanayofanya au wale ambao wanaona hawawezi kwenda na kasi hiyo wanajiweka pembeni.

Unapokuwa hukifanyi kitu kwa karibu ni rahisi sana watu kukudanganya.
Lakini pale unapokuwa mfanyaji mkuu, watu hawawezi kuja na mambo ya uzushi kwako.

Kuna maeneo mengi ya kufanyia kazi kwenye biashara yako.
Lakini eneo moja muhimu sana ambalo unapaswa kulijua kwa kina na kulifuatilia kwa karibu kwenye biashara yako ni mauzo.
Na hapo ndipo unapopaswa kuweka juhudi zako zote, kuhakikisha unaijenga biashara yako kuwa mashine ya mauzo.

Kwa kujenga misingi sahihi ya mauzo kwenye biashara yako, unaipa biashara hiyo nafasi nzuri ya kukua.

Tayari tunao mchakato sahihi wa mauzo, ambao ukifanyiwa kazi unapelekea mauzo kukua zaidi kwenye biashara.

Rai yangu kwako ni wewe kurudi kwenye misingi sahihi ya kujenga na kukuza biashara yako.
Kwa kukaa vyema kwenye mchakato sahihi, kunazalisha matokeo bora kabisa.

Haijalishi biashara yako imekuwa kubwa kiasi gani.
Wala haijalishi imeajiri wafanyakazi wangapi.
Kama wewe mmiliki wa biashara hautakaa kwenye misingi sahihi, kazi yako itakuwa mara mbili. Yaani utawaajiri watu na bado utalazimika kurekebisha kazi zao.

Kuna majukumu makubwa mawili ambayo nataka uyashike kwa kina kwenye biashara yako kwa sasa.
Jukumu la kwanza ni kuwa meneja mkuu wa biashara, hapo unahakikisha kila kitu kinatekelezwa kama kilivyopangwa.
Jukumu la pili ni kuwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea. Kwa kuwa vizuri kwenye mauzo unatengeneza nafasi za ukuaji zaidi.

Usiruhusu sababu zozote zile kukuzuia kutekeleza majukumu hayo makubwa mawili.
Hayo ndiyo kipaumbele cha kwanza kwako hivyo unapaswa kutatekeleza kwa msimamo kila mara bila kuacha.

Lengo letu ni kujenga uhuru kutoka kwenye biashara zetu.
Lakini hatuwezi kufika huko kama misingi haijakaa sawa.
Turudi kwanza kwenye misingi ili kuweza kusimama imara na kuendesha biashara yenye mafanikio.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe